Ujenzi daraja la Kigongo – Busisi kukamilika Aprili 30

Mwanza. Serikali imesema ujenzi wa daraja la Magufuli (Kigongo – Busisi) utakamilika rasmi Aprili 30, 2025 na kuanza kutumika rasmi.

Hata hivyo, hadi kufikia Aprili 10, 2025, magari yataanza kupita upande mmoja wa barabara kwenye daraja hilo lenye urefu wa kilomita tatu ambalo ujenzi wake kwa sasa umefikia asilimia 97.

Daraja hilo linaunganisha barabara kuu ya Usagara – Sengerema – Geita, ya kilomita 90 ambayo ni sehemu ya barabara iliyopo kwenye ushoroba wa Ziwa Victoria, inayoanzia Sirari mpakani mwa Tanzania na Kenya hadi Mutukula, mpakani mwa Tanzania na Uganda.

Kwa sasa, sehemu ya barabara hiyo, eneo la Kigongo – Busisi inaunganishwa kwa kutumia vivuko vikubwa vitatu vya Mv Mwanza, Mv Misungwi na Mv Sengerema.

Kutokana na idadi kubwa ya magari yanayopita kwa siku, abiria na magari hulazimika kutumia takriban saa mbili au zaidi kuvuka kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine, huku muda wa kuvuka ukielezwa kupungua kufika wastani wa dakika tatu hadi nne.

Akizungumza Machi 22, 2025 wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ilipofanya ukaguzi wa ujenzi wa daraja hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dk Charles Msonde amesema Aprili 10, 2025, magari yataruhusiwa kuanza kupita upande mmoja wa daraja ambao utakuwa umekamilika kwa asilimia 100.

“Hadi Aprili 30, 2025, daraja hili litakuwa limekamilika lote na kuanza kutumika rasmi kwa magari na watembea kwa miguu,” amesema Dk Msonde.

Dk Msonde amesema daraja hilo ambalo ujenzi wake umegharimu Sh610 bilioni, limefikia asilimia 97.

Kuhusu usalama, Dk Msonde amesema utaimarishwa kwa kufungwa kamera za CCTV, sambamba na kuwepo kwa geti mwanzo na mwisho wa daraja.

Akizungumzia gharama za kuvuka kwenye daraja hilo mara litakapoanza kutumika, Dk Msonde amesema bado wapo kwenye hatua za uchakataji wa kipi kilipiwe na kipi kisilipiwe katika uvukaji darajani hapo.

“Bado tunajifunza kwa wenzetu wa vivuko, Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa), hili la gharama bado lipo kwenye hatua za uchakataji hadi kufikia Aprili 30, 2025, kila kitu kitajulikana,” amesema.

Dk Msonde amesema daraja hilo litatoa huduma kwa majira yote ya mwaka kwa saa 24 kila siku.

“Litasaidia kumaliza msongamano wa magari uliokuwa unatokea wakati vivuko vinahudumia na kupunguza muda wa safari na kuboresha usafiri kwa magari yanayotumia barabara hii ya ushoroba wa Ziwa Victoria,” amesema.

Amesema pia litachochea uchumi katika ukanda wa Ziwa Victoria na Taifa kwa ujumla kwani mazao ya wakulima na ya samaki yatafika sokoni kwa wakati.

“Litasaidia pia kuongeza kasi ya mwingiliano wa watu kutoka upande mmoja kwenda mwingine ikiwamo kwenye huduma muhimu kama za afya ukizingatia kuwa Hospitali ya Bugando ndio rufaa inayotegemewa Kanda ya Ziwa,” amesema.

Pia, linatajwa kuwa kiungo muhimu kwa Mkoa wa Mwanza ambao ndiyo kitovu cha biashara kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa, lakini pia kuingia na kutoka katika nchi za jirani au za maziwa makuu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya PIC, Augustine Vuma Holle amepongeza hatua ya ujenzi ulipofika na kuitaka Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara (Tanroads) kuhakikisha asilimia tatu zilizosalia zinakamilika kwa wakati.

“Hizi asilimia tatu zilizosalia mzikamilishe kwa wakati ili ifikapo Aprili 30, wananchi waanze kulitumia daraja hili na kuondokana na adha ya kuvuka kwa muda mrefu,” amesema Holle.

Pia  ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na kueleza  iliupokea mradi huo ukiwa umefikia asilimia 25 kutoka kwa mtangulizi wake, hayati John Magufuli na sasa umefikia asilimia 97.

Awali, meneja wa Tanroads Mkoa wa Mwanza, Pascal Ambrose amesema hadi sasa ujenzi wa daraja (main structure) umekamilika zilizobaki ni kazi chache.

Amezitaja kazi hizo kuwa ni uwekaji wa kingo za daraja, usimikaji wa taa za barabarani na mfumo wa kuzuia radi na ujenzi wa tabaka la lami (SP12.5) kwenye daraja na barabara unganishi.

Daraja hilo lenye upana wa mita 28.45, lina njia mbili za magari zenye upana wa mita saba kwa kila upande.

Pia, lina njia ya waenda kwa miguu upana wa mita 2.5 kwa kila upande, maegesho ya dharura upana wa mita 2.5 kwa kila upande, sehemu inayotenganisha pande za barabara na kingo za usalama wa daraja kwa watembea kwa miguu na magari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *