
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema ujenzi wa daraja la Jangwani litakalokuwa na urefu wa mita 390 unatarajiwa kuanza rasmi mwezi ujao.
Ujenzi wa daraja la Jangwani utagharimu Sh97.1bilioni, ukikamilika utaondoa adha ya kukatika kwa mawasiliano ya kuingia katika jiji la Dar es Salaam, utahusisha pia barabara za maingilio za urefu wa mita 700.
Tayari mkataba kati ya Serikali na mkandarasi atakayetekeleza mradi huo (China Communications Construction Company Limited), umeshasainiwa tangu Oktoba 22, 2024 na ujenzi wake utachukua miezi 24 hadi kukamilika kwake.
Chalamila amebainisha hayo leo Ijumaa Aprili 18, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mkoa huo, ikiwemo ulinzi na usalama, pamoja changamoto za miundombinu.
Amesema mkandarasi akishasaini mkataba aanzi kazi moja kwa moja kufanya kazi bali anapewa muda wa angalau miezi minne wa kukusanya vitendea kazi kwa ajili ya ujenzi huo, pia anatumia fursa hiyo kuchukua mkopo benki ili kuwezesha ujenzi kufanyika kwa ufanisi.
Katika maelezo yake, Chalamila amesema mkandarasi atakayetekeleza mradi huo, ameanza kujenga kempu kwa ajili ya kutunza vifaa vitakavyotumika katika ujenzi wa daraja la Jangwani.
“Nimezungumza na Waziri wa Ujenzi (Abdallah Ulega) mapema mwezi wa tano mtamuona mkandarasi anaanza shughuli zake. Lakini kwa sasa hivi kwa wale mliotembea eneo lile mtaona mkandarasi ameshaanza ujenzi wa eneo atakalotunza vifaa vyake.
“Rais Samia Suluhu Hassan amedhamilia kwa dhati kwamba mwaka huu, daraja la Jangwani litaanza kujengwa na panapo maajiliwa hakutakuwa na kilio cha Watanzania na wakazi wa Dar es Salaam kuhusu Jangwani,” amesema Chalamila.
Changamoto za miundombinu
Katika mkutano huo, Chalamila amekiri hali ya miundombinu kwenye mkoa huo, bado si mzuri hasa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, akitolea mfano barabara ya kutoka Mombasa hadi Moshi Bar.
Barabara nyingine ni za Saranga, Kimara, Kigamboni, Goba-Kinzudi ambapo hali yake siyo nzuri kutokana na kuahiribiwa na mvua nyingin zinazonyesha.
“Katika hili Tarura (Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini), ina bajeti ya kuboresha barabara zilizoharibiwa, tunaamini baada ya mvua kukata jambo hili litafanyika,” amesema Chalamila.
Kuhusu barabara za Mradi wa Uboreshaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP), awamu ya pili walikubaliana hadi Febrauri mwaka huu, ujenzi uwe umeanza, lakini ukweli uliopo baadhi ya wananchi wana malalamiko kuhusu fidia.
“Hizi ni barabara ambazo Serikali imetafuta fedha kupitia Benki ya Dunia (WB), hivyo wananchi wakiibua malalamiko benki ya dunia inakuwa makini na hawezi kuendelea hadi wasikilizwe na kupatiwa majawabu,” amesema.
“Zipo barabara ambazo utata huo umeshatenguliwa, tayari zimeshaanza kujengwa ikiwemo ya Kimara -Bonyokwa ambayo imeshaanza kujengwa,” amesema Chalamila.
Mbali na hilo, Chalamila amesema karibu kilomita 88 za barabara za DMDP makandarasi wameanza kazi ya ujenzi, huku barabara zingine mikataba yake ikiendelea kusaini kadri muda unavyozidi kwenda.
Aonya wanaochezea amani
Kwa mujibu wa Chalamila, ameona kuna ujumbe mfupi unaosambaa katika mitandao ya kijamii, zingine zinatishia uwepo wa vurugu ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, ametumia nafasi hiyo, kuwaonya wanaofanya hivyo, kuacha.
“Hakuna mtu yeyote atakaye vuruga amani ya mkoa wa Dar es Salaam, jana kupitia Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam (Jumanne Muliro) aliitoa maelezo kadhaa kuhusu usalama wa mkoa huu,”amesema Chalamila.
Jana Kamanda Muliro alionya wananchi kujitokeza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aprili 24, 2025 wakati Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akifikishwa mahakamani hapo, akisisitiza atakayejitokeza atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, leo Ijumaa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimelaani hatua hiyo, kikisema ni kinyume cha sheria na inalenga kudhoofisha demokrasia.
“Tunaitafsiri kauli hii kama mpango wa wazi wa kuminya haki za wananchi, kuingilia uhuru wa mahakama, kuzuia ushiriki wa umma katika mchakato wa haki,”amesema Brenda Rupia ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema.
Akikazia tamko la Kamanda Muliro, Chalamila amesema, “hakuna mtu yeyote, chama siasa wala taasisi ya dini au isiyo ya dini na mtu binafsi atakayeweza kuvuruga amani iliyojengwa katika misingi ya uongozi.
“Tunafahamu wapo baadhi ya watu wenye malalamiko yao, lakini wazingatie sheria na utaratibu wa kuyafikisha kwenye vyombo au ofisi zinazohusika na masuala yao. Kuanzia sasa hadi kuandele Dar es Salaam itaendelea kuwa kioo cha amani,” amesema Chalamila.