
Kahama. Serikali mkoani Shinyanga imekiri kuwepo kwa wimbi la biashara za magendo zinazoingia kutoka nchi jirani kwa njia za ‘panya’, hali inayohatarisha ustawi wa viwanda vya ndani.
Hali hiyo pia inatajwa kuikosesha Serikali mapato kutokana na bidhaa hizo kutolipiwa kodi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha amekiri changamoto hiyo usiku wa kuamkia leo Machi Mosi, 2025 wakati wa utoaji tuzo kwa walipakodi bora 2023/24 katika mkoa huo na mkoa wa kikodi wa Kahama.
Hiyo ni baada ya taarifa ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Yusuph Mwenda kuonyesha kuota mizizi kwa changamoto hiyo nchini.
“Ni kweli hapa Kahama na Shinyanga tumepakana na nchi za jirani, kuna bidhaa zinazotoka nchi jirani na watu wengine wanaziingiza bila kuzilipia kodi, mimi nafikiri huo ni uhalifu, tunaomba mamlaka zetu zikishirikiana na TRA kulishughulikia hili.”
“Kwa kweli ni dhambi kubwa sana kuingiza mali kutoka nchi nyingine, na kuisaidia nchi hiyo kupiga hatua kwa gharama ya sisi kuendelea kudidimia, hili kwa kweli ni onyo.”
Akimwakilisha Mwenda, Mkurugenzi wa Tehama wa TRA, Emmanuel Nnko ametahadharisha kuwa bidhaa za magendo zinahatarisha afya za walaji.
Nnko amesema katika mwaka 2023/24, mamlaka hiyo kwa mkoa wa kikodi Kahama na Shinyanga ilifanikiwa kukusanya Sh34.15 bilioni sawa na asilimia 132.05 ya lengo la kiasi cha Sh25.78 bilioni iliyopangwa kukusanywa.
Amesema katika kipindi cha Julai 2024 hadi Januari 2025, Mkoa wa Shinyanga na mkoa wa kodi Kahama umefanikiwa kukusanya Sh36.78 bilioni sawa na asilimia 114.03 ya lengo la kukusanya Sh32.25 bilioni .
Nnko amesema licha ya changamoto zilizopo, kiwango hicho kikubwa cha makusanyo ni matokeo ya kuwa na walipakodi wazalendo na waliohamasika katika kuunga mkono juhudi za Serikali kuliletea Taifa maendeleo.
Mlipakodi, Abdulrahman Mohamed ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira kwa wafanyabiashara, hali inayowawezesha kulipa kodi.