
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kwamba watu wawili wameambukizwa aina mpya ya virusi vya homa ya nyani, “Mpox” nchini Uingereza baada ya kukutana na mgonjwa aliyerejea nchini humo kutoka Afrika. Hayo yanatambuliwa kuwa maambukizi ya kwanza ya ugonjwa huo nje ya Bara Afrika.
Shirika hilo lilisema katika taarifa yake ya jana Jumanne kwamba watu hao wawili walioambukizwa homa ya nyani wanaishi katika nyumba moja na mtu aliyepimwa na kukutwa na ugonjwa huo muda mfupi baada ya kutembelea nchi kadhaa za Afrika.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, hizi ni “kesi mbili za kwanza za maambukizi ya Mpox barani Ulaya na za kwanza kuwahi kuripotiwa nje ya Afrika tangu Agosti 2024.”
Kwa upande wake, Shirika la Usalama wa Afya la Uingereza limesema kuwa watu walioambukizwa wanapata matibabu katika Hospitali ya Guy’s na St. Thomas huko London, na kuonya juu ya uwezekano wa kesi zingine kuonekana katika nyumba iliyotajwa hapo awali.
Takwimu za Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Umoja wa Afrika (Africa CDC) zinaonyesha kuwa zaidi ya watu elfu moja wamefariki dunia kutokana na homa ya nyani barani Afrika, ambapo takriban maambukizo 48,000 yamerekodiwa tangu Januari mwaka huu.