Uingereza inakabiliwa na deni la Pauni trilioni 18 za fidia ya utumwa

Nchi za Afrika na Caribbean zinafuatilia mpango ambao unaweza kuigharimu Uingereza pauni trilioni 18 kutokana na nafasi yake ya kihistoria katika biashara ya utumwa.

Baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia, nchi nyingi zilizokuwa makoloni ya Uingereza barani Asia, Afrika na Caribbean zilipata uhuru na kuanza kutekeleza mipango ya kufungua mashtakka dhidi ya historia ya ukoloni wa serikali ya London.

Mwelekeo huo umepata nguvu mpya hasa katika miaka ya hivi karibuni baada ya kifo cha Elizabeth II (Malkia wa zamani wa Uingereza) na kutokana na kuundwa vuguvugu la kupinga ubeberu kama vile “Black Lives Matter”.

Katika mkondo huo, wakuu wa nchi 56 za Jumuiya ya Madola, ambao wanakutana Samoa tangu wiki iliyopita, wanasisitiza kwamba wakati umefika wa kuanza mazungumzo “ya maana, halisi na ya heshima” kuhusu mipango na malipo ya fidia kutoka Uingereza.

Viongozi hao walitaka kuchapisha taarifa tofauti kuhusiana na suala hili, lakini baada ya mashauriano ya kina na maafisa wa London, kwa sasa, wametosheka kuongeza kifungu hicho kwenye taarifa ya mwisho ya mkutano huo.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, ambaye pia ameshiriki mkutano wa Samoa, amesema anaelewa hisia kali za washiriki kuhusu historia ya utumwa, lakini kuna ulazima wa kukubali ukweli na kuvuka kipindi kilichopita.

Hadi sasa Uingereza imekuwa ikipinga matakwa ya fidia ya kipindi cha utumwa na ukoloni wake, na ofisi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo ilitangaza kabla ya mkutano wa kilele wa mwaka huu huko Samoa kwamba suala la fidia haliko katika ajenda.