Uhusiano wa Niger na nchi za Ulaya wazidi kuharibika, EU yamwita balozi wake

Umoja wa Ulaya (EU) umemuondoa balozi wake aliyekuweko Niamey, mji mkuu wa Niger kutokana na kushadidi mvutano na uongozi mpya wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Serikali ya Niger inalalamika kwamba nchi za Ulaya zinataka kuidhibiti nchi hiyo kupitia misaada ya kibinadamu.

Siku ya Ijumaa, serikali ya mpito ya Niger iliulaumu Umoja wa Ulaya kwa kutenga Euro milioni 1.3 katika misaada ya kibinadamu bila kushauriana na serikali hiyo.

Taarifa ya serikali ya Niger imemshutumu balozi wa EU kwa kuchochea machafuko kupitia kuzihonga fedha asasi zisizo za kiserikali na kupuuza sheria za ndani ya Niger za kuweko uwazi na haki ya serikali ya kusimamia masuala ya taifa zima.

Umoja wa Ulaya unaendelea kupuuza haki ya kujitawala Niger na imekataa kupitishia misaada yake katika kanali zilizoainishwa. Baada ya kushinikizwa na serikali ya Niger ili uheshimu sheria za nchi hiyo, Umoja wa Ulaya umekataa na umeamua kumuondoa balozi wake mjini Niamey. 

Serikali ya Niger imesema kuwa, madai ya Umoja wa Ulaya ya kudai ina dhamira ya kusaidia raia si ya kweli bali lengo lake hasa ni kuishinikiza serikali ya nchi hiyo kupitia asasi za kijamii na kupindisha sheria za nchi. Umoja wa Ulaya umedai kuwa misaada ya kibinadamu haipaswi kuingizwa kwenye masuala ya kisiasa suala ambalo limepingwa vikali na serikali na Niger ambayo imesema kuwa, kila nchi ina haki ya kuweka sheria za kusimamia mambo yake na misaada kutoka nje imewekewa kanali maalumu ambazo Umoja wa Ulaya unazidharau na hautaki kuheshimu sheria za nchi hiyo.