Uhusiano wa Iran na Tunisia wazidi kuimarika, Tunis yataka safari za moja kwa moja za ndege

Balozi wa Tunisia mjini Tehran ametaka kuweko safari za moja kwa moja za ndege baina ya Tehran na Tunis hasa kwa vile uhusiano wa nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unazidi kuimarisha siku baada ya siku.

Balozi Imad Al-Rahmuni ametoa mwito huo hapa Tehran wakati aliponana na Hossein Pourfarzaneh, kaimu wa mkuu wa Shirika la Usafiri wa Anga la Iran na sambamba na kuelezea kufurahishwa kwake na namna uhusiano wa nchi yake na Iran unavyozidi kuimarika amesema kuwa, kuna udharura wa kuweko safari za moja kwa moja za ndege baina ya Tehran na Tunis ili kuimarisha zaidi uhusiano wa kidugu uliopo baina ya pande mbili.

Balozi wa Tunisia mjini Tehran amehimiza pia kufanyika vikao vya pande mbili vya kufuatilia makubaliano yaliyofikiwa kwenye mazungumzo ya huko nyuma na kuhakikisha kwamba, kila kinachokubaliwa kwenye vikao hivyo vya pamoja kinatekelezwa kivitendo.

Kwa upande wake, kaimu mkuu wa Shirika la Usafiri wa Anga la Iran amesisitizia wajibu wa kuwepo ushirikiano zaidi baina ya nchi yake na Tunisia hasa katika suala la usafiri na uchukuzi akisema kwamba iwapo hilo litafanyika, litafungua uwanja wa ushirikiano zaidi katika nyuga nyinginezo zote zikiwemo za kiufundi, kielimu na kadhalika.