
Uhispania imekataa kuruhusu meli 2 za Marekani kutia nanga kwenye bandari yake kwa sababu zimebeba silaha kwa ajili ya utawala wa Kizayuni wa Israel unaofanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina na Lebanon.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uhispania imesema, meli ya “Maersk Denver” ambayo iliondoka New York mnamo Oktoba 31 na “Maersk Seletar” iliyondoka New York yarehe 4 Novemba ikielekea bandari za Israel, hazitaruhusiwa kutia nanga kwenye bandari za Uhispania.
Mbunge Enrique Santiago wa Uhispania hapo awali alimtaka Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo kuchukua hatua kuhusiana na meli mbili za mizigo za Marekani zinazotarajiwa kuwasili kwenye bandari ya Algeciras tarehe 9 na 14 mwezi huu zikiwa njiani kuelekea Israel.
Wizara ya Ulinzi ya Uhispania tarehe 1 Novemba iliashiria ahadi ya nchi hiyo kwa ajili ya amani ya Palestina na Lebanon na kushikamana serikali ya Madrid na sheria za kimataifa na kutangaza kwamba, makampuni ya kijeshi ya utawala wa Israel yamepigwa marufuku kushiriki katika maonyesho ya zana za kijeshi ya Madrid 2025 .
Marekani na baadhi ya washirika wake wa Kimagharibi wanaendelea kuupatia utawala wa Kizayuni wa Israel silaha zinazotumiwa katika mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza na Lebanon.