
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania amesisitiza ulazima wa kusitishwa haraka iwezekanavyo mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na jeshi la Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na Lebanon.
José Manuel Albares, ametoa wito wa kukomeshwa mashambulizi ya mabomu yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko Lebanon na Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa, uharibifu na vifo katika eneo la Magharibi mwa Asia (Mashariki ya Kati) lazima ukomeshwe haraka.
Katika ujumbe alioweka kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X, Albares amelaani mashambulizi ya kinyama ya jeshi la utawala wa Kizayuni unayoyafanya huko Ukanda wa Gaza na Lebanon, ameandika: “tunataka usitishaji mapigano utekelezwe nchini Lebanon na Ukanda wa Gaza na kuchungwa sheria za kimataifa”.
Kwa mujibu wa tangazo la Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza, watu 43,846 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 103,000 wamejeruhiwa kutokana na mashambulizi ya jeshi la Israel huko Gaza yaliyoanza Oktoba 7 mwaka jana na yakiwa yangali yanaendelea hadi sasa.
Kadhalika, watu 3,481 wameuawa shahidi kutokana na muendelezo wa mashambulizi na jinai zinazofanywa na jeshi la utawala katili wa Kizayuni dhidi ya Lebanon.