Mwanasheria nguli kwenye ukanda wa Afrika Mashariki ambaye pia ni mwanasiasa kutoka Kenya, Martha Karua, sambamba na wanaharakati na wanasheria wengine, wamenyimwa kibali na idara ya uhamiaji kuingia nchini Tanzania, ambako waliwasili hivi leo kujiandaa kuhudhuria kesi ya Tundu Lissu.
Imechapishwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kupitia ukurasa ukurasa wake wa kijamii, Martha Karua amethibitisha kuzuiliwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, akiwa pamoja na wakili wa masuala ya haki za binadamu kutoka kenya, Lynn Ngugi na mwanachama wa chama cha wanasheria wa Afrika Mashariki, Gloria Kimani.
Kwa mujibu wa maelezo yao, baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Dar Es Salaam, pasi zao za kusafiria zilichukuliwa na maofisa wa idara ya usalama, kabla ya baadae kutaarifiwa kuwa hawaruhusiwi kuingia Tanzania, bila hata hivyo idara ya uhamiaji kutoa sababu za kuwazuia.
Hata hivyok kuzuiwa kwao kunahusishwa na ushiriki wao katika kufuatilia mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, ambaye ameendelea kusota rumande.
Aidha karua ameandika kwenye ukurasa wake wa X na kuambatanisha picha jongeo kuwa ‘Tunasubiri kurejeshwa nyumbani baada ya kufanikiwa kuchukua mabegi yetu’.
Awali Martha Karua, alihoji ni vipin serikali ya Tanzania inaamua kuwazuia raia wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kinyume na itifaki ya mkataba uliounda Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao unahamasisha uhuru wa raia wa jumuiya kuingia na kutoka nchi moja hadi nyingine kwa uhuru.

Alipohudhuria kwa mara ya kwanza kesi ya Tundu Lissu, mwezi uliopita, Martha Karua na wanasheria wengine wakigeni, walizuiwa nje ya mahakama ambako kesi ya Lissu ilikuwa inasikilizwa, kitendo ambacho kilikashifiwa.
Kufuatia kuzuiliwa kwao kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, tayari watetezi wa haki za binadamu wa ndani na nje ya Tanzania, wamelaani kitendo kilichofanywa na mamlaka za Tanzania, wakimataka rais Samia Suluhu Hassan, kuagiza wanasheria hao kuruhusiwa kuingia Tanzania bila vikwazo.
Tangu kukamatwa kwa Tundu Lissu mwezi uliopita akituhumiwa kwa makosa ya uhaini ambayo ikiwa atakutwa na hatia adhabu yake ni kunyongwa, mashirika ya ndani na yale ya kimataifa, yameionyooshea kidole Serikali ya Tanzania, kwa kujaribu kuminya maoni ya watu wachache pamoja na kuingilia uhuru wa mahakama.
Katika mfululizo wa matamko waliyoyatoa ikiwemo lile la bunge la umoja wa Ulaya, wameitaka Serikali ya rais Samia, kuacha kuingialia uhuru wa mahakama na uhuru wa watu, wakisisitiza mamlaka kuruhusu watu kufanya siasa kwa uwazi.
Aidha waliitaka serikali kufanya mazungumzo na Chadema ili kufikia muafaka kuhusu madai yao ya kutaka kuzuia uchaguzi wa mwezi Octoba mwaka huu hadi pale kutakapofanyika marekebisho ya sheria za uchaguzi.
Tundu Lissu, ambaye mwezi Januari mwaka huu alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa Chadema, amekuwa akisisitiza msimamo wa chama chake kupitia kauli mbiu ya “hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi” akisema watatumia raia wa nchi hiyo kuzuia uchaguzi, huku akikiri kweli msimamo wao hauna tofauti na uasi.
Lissu alikamatwa akiwa katika mfululizo wa kampeni za chama hicho kuwahamasisha raia kudai mabadiliko, ambapo baadae akafunguliwa mashtaka ya kuchapisha habari za uongo na kuandaa uasi, kesi ambayo mwenyewe amesema imechochewa kisiasa.
Tayari kesi hii imevuta hisia za watu wengi ambapo hata kumeshashuhudiwa mvutano wa kisheria ambapo awali waendesha mashtaka walitaka kesi yake iendeshwe kwa njia ya mtandao, pendekezo lililopingwa na upande wa utetezi ambao ulisema kukukubali kesi kusikilizwa kwa mtandao ni kumnyima haki mteja wao.
Lissu anatarajiwa kufikishwa mahakamani mei 19 mwaka huu, ambapo kwa mujibu wa amri ya mahakama, atapaswa kuletwa mahakamani.
Awali Tundu Lissu, alitishia kususia ushiriki wa vikao vya kesi yake na hata kuanza mgomo wa kula kushinikiza kesi yake kusikilizwa katika mahakama ya wazi.
Kuelekea kesi hii, viongozi wa chama chake wametoa wito kwa wafuasi wao kujitokeza mahakamani kumuunga mkono mwenyekiti wao, wito ambao hata hivyo umekutana na upinzani toka kwa idara za usalama ambazo zimeonya dhidi ya kufanyika kwa vurugu zozote baada ya awali wafuasi wa Chadema kukamatwa, kupigwa na hata kutekwa nje ya majengo ya mahakama.