
Mgonjwa wa pili wa Ebola, mtoto wa miaka 4, amefariki nchini Uganda, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema, likinukuu wizara ya afya ya nchi hiyo.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Kifo hicho kinafanya idadi ya wagonjwa waliothibitishwa nchini Uganda kufikia 10.
Nchi hiyo ya Afrika Mashariki ilitangaza kuzuka kwa ugonjwa huo wa kuvuja damu unaoambukiza sana na ambao mara nyingi huwa mbaya sana mwezi Januari baada ya kifo cha muuguzi wa kiume katika Hospitali ya taifa ya Mulago katika mji mkuu wa Kampala.
Ofisi ya WHO nchini Uganda iliandika kwenye mtandao wa X usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili kwamba wizara iliripoti “mgonjwa wa pili aliyeambukizwa virusi vya Ebola katika hospitali ya Mulago, ambaye ni mtoto mwenye umri wa miaka 4 na nusu, ambaye aliaga dunia” siku ya Jumanne.
Mulago ndiyo hospitali pekee ya taifa iliyotengewa wagonjwa wa Ebola.
Wizara ilisema mnamo Februari 18 kwamba wagonjwa wote wanane wa Ebola waliokuwa chini ya uangalizi wameruhusiwa lakini angalau watu 265 walibaki kwenye karantini kali mjini Kampala na miji mingine miwili.
Dalili za Ebola ni pamoja na homa, maumivu ya kichwa na misuli. Virusi huambukizwa kwa kugusana na majimaji ya mwili yaliyoambukizwa.