
Utafiti mpya wa mashirika ya kibinadamu nchini Uganda, unaonesha kuwa Watu waliohamishwa kupisha ujenzi wa bomba la mafuta la Afrika Mashariki, EACOP, wamelalamikia kutorudishwa na ulipwaji wa fidia.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Bomba hili la mafuta ghafi la Afrika Mashariki litakapokamilika, litasafirisha mafuta kutoka maeneo ya Tilenga na Kingfisher magharibi mwa Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Mradi huu wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Uganda, kampuni ya mafuta ya Ufaransa ya TotalEnergies na kampuni ya mafuta ya taifa la China, unatajwa na Uganda kama mageuzi kwa uchumi wa nchi, licha ya kuwa tangu awali umekabiliwa na ukosoaji kuhusu athari za mazingira na watu wanaoishi kwenye eneo la mradi.
Takriban watu 13,000 nchini Uganda na Tanzania wamelazimika kuyahama makazi yao kupisha mradi huo, huku wale waliolazimika kuhama walipewa chaguo la makazi mapya au fidia ya pesa taslimu.
Hata hivyo Shirika la Haki Defenders Foundation na Chuo Kikuu cha Sheffield wametoa ripoti bada ya kuwahoji watu 100 ikiwa ni pamoja na wale ambao ardhi yao ilichukuliwa kwa nguvu, wamebaini kuwa licha ya mazingitaio ya sheria za ndani na kimataifa, fidia inayotolewa ni ndogo.
Aidha wale waliokubali kupewa maeneo, walijengewa nyumba zinazofanana bila hata hivyo serikali kuzingatia ukubwa wa familia, huku maeneo ya makazi mapya yakiwa hayana miundombinu ya msingi, watu wakilazimika kusafiri umbali mrefu kupata maji, masoko na vifaa vya matibabu.
Jumla ya mapipa bilioni 6 ya mafuta ghafi yaligunduliwa magharibi mwa Uganda mwaka 2006 ambapo kulingana na uchambuzi wa Taasisi ya Uwajibikaji wa Hali ya Hewa, kusafirisha, kusafisha na kuchoma mafuta kungezalisha tani milioni 379 za kaboni duniani katika kipindi cha miaka 25 cha uendeshaji wa bomba hilo.