Uganda: Kizza Besigye asitisha mgomo wa njaa na hivyo kuzua wasiwasi miongoni mwa wafuasi wake

Baada ya zaidi ya wiki moja ya mgomo wa kula, mpinzani wa kihistoria nchini Uganda Kizza Besigye ameanza tena kula, kulingana na mkewe. Mgomo wake ulichochewa baada ya mamlaka kukataa kuhamishia kesi yake katika mahakama ya kiraia, licha ya uamuzi wa Mahakama ya Juu mwishoni mwa mwezi wa Januari.

Imechapishwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Kutokana na uhamasishaji katika ngazi ya kitaifa – pamoja na wito wa kuachiliwa kwake ukiongozwa na watu kama Bobi Wine – na uhamasishaji wa kimataifa, Kizza Besigye hatimaye alifikishwa mbele ya mahakama ya kiraia siku ya Ijumaa ambapo alishtakiwa kwa uhaini mkubwa.

Licha ya mabadiliko haya ya mahakama, washirika wake wa karibu hawana matumaini, kama Harold Kaija, katibu mkuu wa People’s Front for Freedom, chama kipya kilichoanzishwa na Besigye, mgombea wa urais mara nne nchini Uganda, alipohojiwa na Christina Okello wa timu ya wahariri wa RFI kanda ya Afrika.

“Tunafarijika kwamba amesitisha mgomo wake wa kula. Siku ya Ijumaa alifika mahakamani akiwa kwenye kiti cha magurudumu, akiwa mnyonge sana, na ungeweza kuona ni mgonjwa. Siku chache zilizopita, tuliwasilisha ombi la kupinga uhalali wa kuzuiliwa kwake, lakini hakimu alitupilia mbali, hata baada ya kuona udhaifu wa Dk Besigye, kuamuru arudi gerezani badala ya kumpeleka hospitali.

Ingawa mahakama za kiraia hutoa mfano wa haki, Rais Museveni anadhibiti kila kitu katika nchi hii. Mtu anapaswa tu kuangalia mashtaka dhidi ya Dk Besigye: awali, yalikuwa mashtaka ya uhaini ambayo yalijumuisha madai ya kupatikana na silaha, wakati shtaka jipya ni mashtaka makubwa ya uhaini, bila kutaja silaha. Marekebisho haya dhahiri yanaonyesha hatua inayokusudiwa kuongoza taratibu za kisheria.

Kwa hivyo tuna matumaini kwa takriban 30% kuhusu matokeo ya kesi hii, na tunaacha 70% iliyobaki mikononi mwa Mungu. “