Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda na aliyewahi kuwa mgombea wa urais Kizza Besigye ameanza kususia chakula kulingana na taarifa ya mawakili wake.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Besigye amekuwa akizuiliwa kwa kipindi cha miezi kadhaa tangu kutekwa akiwa katika nchi jirani ya Kenya.
Mpinzani huyo ambaye aliwahi kuwa daktari wa binafasi wa rais Yoweri Museveni amekuwa akikabiliwa vikali na serikali tangu kujiunga na upinzani miaka 25 iliopita.
Katika kipindi hicho amewania katika uchaguzi mkuu wa urais mara nne bila ya kufanikiwa.

Alitekwa nyara akiwa jijini Nairobi mwezi Novemba mwaka uliopita na amekuwa akikabiliwa na mashataka ya uhaini katika mahakama ya kijeshi.
Kulingana na wakili wake Elias Lukwago, Besigye, 68, alianza kususia chakula siku ya Jumatatu kutokana na kile anachosema hakuwa na namna nyengine.
Besigye amekuwa akisubiri uamuzi wa mahakama ya kijeshi kuhusu madai anayokabiliwa nayo tangu mwezi Novemba licha ya uamuzi wa mahakama mwezi uliopita kwamba ilikuwa ni kinyume cha sheria kwa kesi za kiraia kusikilizwa katika mahakama ya kijeshi.
Lukwago amesema mteja wake pia ameamua kususia kula chakula kama njia moja ya kuonyesha kutoridhishwa na kuendelea kuzuiliwa kwake kinyume na sheria.
Kando na mashtaka ya uhaini anayokabiliwa nayo, Besigye pia anatuhumiwa kwa kuchochea machafuko wakati alipoongoza maandamano ya kupinga kupanda kwa gharama ya maisha mwaka wa 2022.
Rais Yoweri Museveni ametupilia mbali uamuzi wa mahakama wa mwezi uliopita kuhusu kesi za kiraia kusikilizwa katika mahakama ya kijeshi.
Soma piaUganda : Besigye kuendelea kuzuiliwa licha ya uamuzi wa mahakama