
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye amefunguliwa mashtaka ya uhaini, ikiwa ni sehemu ya msururu wa matatizo ya kisheria yaliyotokana na tuhuma alizozodaiwa kupanga kumuondoa kwa nguvu kiongozi huyo wa muda mrefu wa nchi hiyo.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Besigye, mgombea urais mara nne katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki, aliketi kwenye kiti cha magurudumu alipokuwa akikabiliwa na mashtaka katika chumba cha mahakama katika mji mkuu, Kampala. Uhaini unaadhibiwa na kifo nchini Uganda.
Besigye amekuwa kizuizini tangu Novemba 16, alipotoweka katika mji mkuu wa Kenya Nairobi. Siku kadhaa baadaye, alifikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi mjini Kampala kujibu mashtaka ya kutishia usalama wa taifa.
Mwezi uliopita, Mahakama ya Juu ilisitisha kesi yake ya kijeshi, ikisema mahakama za kijeshi haziwezi kuwahukumu raia. Familia ya Besigye, wafuasi na wengine walitaka aachiliwe mara moja, lakini alizuiliwa katika gereza lenye ulinzi mkali na baadaye akagoma kula.
Besigye ameonekana kuwa dhaifu wakati alipofikishwa mahakamani hivi majuzi, na hivyo kuzua hofu kwamba madhara yoyote aliyofanyiwa gerezani yanaweza kuzua machafuko mabaya. Raia wengi wa Uganda wanazitaka mamlaka kumwachilia huru kwa misingi ya kibinadamu.
Shirika la kimataifa la Haki za Binadamu la Amnesty International pia lilitoa wito wa kuachiliwa kwa Besigye, likisema “kutekwa nyara kwake kunakiuka wazi sheria za kimataifa za haki za binadamu na utaratibu wa kumrejesha nyumbani na dhamana yake ya kesi ya haki.”
Hii ni mara ya pili kwa Besigye kufunguliwa mashtaka ya uhaini kwa madai ya kujaribu kupindua serikali. Kesi ya kwanza, iliyoletwa mwaka 2005, haikufaulu. Wakati huu, yeye na wengine wanatuhumiwa kuhudhuria mikutano katika miji ya Ulaya na kwingineko ambapo Besigye anadaiwa kuomba “msaada wa kijeshi, kifedha na vifaa ili kupindua serikali ya Uganda kama ilivyotolewa na sheria,” kulingana na mashtaka.
Mawakili wa Besigye wanasema mashtaka hayo yamechochewa kisiasa.
Lakini Rais Yoweri Museveni alisema mpinzani wake wa kisiasa lazima ajibu kwa “makosa makubwa sana anayodaiwa kupanga”. Museveni alikataa wito kutoka kwa baadhi ya watu wa kutaka kusamehewa na badala yake alitoa wito wa “kusikizwa kwa kesi haraka ili ukweli uweze kufichuliwa.”
Kesi ya Besigye inafuatiliwa kwa karibu na Waganda wenye wasiwasi kuhusu hila za kisiasa kabla ya uchaguzi wa rais mwaka ujao. Ingawa Museveni anatazamiwa kugombea tena kiti cha urais, baadhi ya waangalizi wanaamini kuwa anaweza kung’atuka na kuachia nafaasi kwa mwanawe, Muhoozi Kainerugaba, kamanda mkuu wa jeshi katika mapinduzi yasiyo na umwagaji damu.
Wengi wanatarajia mpito wa kisiasa usiotabirika kwa sababu Museveni hana mrithi wa wazi ndani ya safu ya chama tawala cha National Resistance Movement (NRM).
Besigye, daktari ambaye alistaafu kutoka jeshi la Uganda akiwa na cheo cha kanali, ni mwenyekiti wa zamani wa chama cha Forum for Democratic Change, ambacho kilikuwa kundi kuu la upinzani nchini Uganda kwa muda mrefu. Yeye ni mkosoaji mkali wa Museveni, ambaye aliwahi kuwa msaidizi wake wa kijeshi na daktari wa kibinafsi.
Uganda haijawahi kushuhudia marais wakikabidhiana madaraka kwa amani tangu uhuru kutoka kwa wakoloni miongo sita iliyopita.