Uganda imetuma wanajeshi wake jijini Juba, nchini Sudan katika kile mkuu wa majeshi ya nchi hiyo Muhoozi Kainerugaba, amesema wamekwenda kulinda usalama, kuepusha kutokea machafuko mapya, hasa wakati huu ambao rais Salva Kiir na makamu wake Riek Machar wakionekana kutofautiana.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Haya yanajiri baada ya Mvutano kuzidi kati ya Kiir na Naibu wake Riek Machar, na kuzua hofu kuwa makubaliano yao ya mkataba wa amani wa mwaka 2018 huenda yakaysambaratika na nchi kurejea kwenye vita.
Hata hivyo Jenerali Kainerugaba hajatoa maelezo kwa nini Uganda imeamua kutuma vikosi vyake katika nchi hiyo Jirani lakini ameonya tishio lolote la kumuondoa Salva Kiir ni sawa na kutangaza vita dhidi ya Uganda.
Sudan Kusini haijazungumzia tangazo hilo la kupata msaaada wa kijeshi kutoka Uganda.

Wiki iliyopita, Naibu Mkuu wa Jeshi la Sudan Kusini pamoja na mawaziri wawili, wote ni washirika wa Machar, walikamatwa na vikosi vya usalama.
Kukamatwa kwa viongozi hao kulifuatia mapigano katika jimbo la Upper Nile kati ya vikosi vya serikali na waasi wa White Army, ambao walikuwa washirika wa karibu wa Machar wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilizuka 2013 baada ya mivutano ya madaraka kati yake na Kiir.