
Rais wa zamani wa Ufilipino Rodrigo Duterte amekamatwa leo Jumanne, Machi 11, baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa Manila kwa waranti wa kukamatwa kilichotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa vita vyake vikali dhidi ya dawa za kulevya.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Rais wa zamani wa Ufilipino Rodrigo Duterte amekamatwa Jumanne katika uwanja wa ndege wa Manila kwa hati ya kukamatwa iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu kutokana na vita vyake vikali dhidi ya dawa za kulevya.
Makundi ya haki za binadamu yanakadiria kuwa makumi ya maelfu ya watu maskini waliuawa na polisi na makundi ya kujilinda, mara nyingi bila ushahidi wowote kwamba walikuwa wakihusishwa na dawa za kulevya. Mahakama ya ICC imefungua uchunguzi kuhusu kampeni hiyo iliyoanza mwaka 2016 na ambayo inasema huenda ikajumuisha uhalifu dhidi ya binadamu.
Kwa sasa Rodrigo Duterte yuko kizuizini
“Mapema leo asubuhi, polisi ya kimataifa ya Interpol huko Manila imepokea nakala rasmi ya hati ya kukamatwa iliyotolewa na ICC,” ofisi ya rais imesema katika taarifa. “Kwa sasa yuko chini ya ulinzi.” “Rais huyo wa zamani na kundi lake wako katika afya njema na wanachunguzwa na madaktari,” chanzo hicho kimeongeza.
Kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 79 alikuwa akirejea kutoka safari fupi huko Hong Kong na alikuwa ametoka tu kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Manila. Akizungumza mbele ya maelfu ya wafanyakazi wa Ufilipino mjini Hong Kong siku ya Jumapili, rais huyo wa zamani (2016-2022) alilaani uchunguzi huo, akiwaita wachunguzi wa ICC “watoto wa makahaba” huku akikiri “atakubali” iwapo atakamatwa.
Ufilipino iliondoka ICC mwaka 2019 kwa amri yake, lakini mahakama hiyo yenye makao yake mjini Hague, nchini Uholanzi, imesema ina mamlaka juu ya mauaji yaliyotokea kabla ya nchi hiyo kujiondoa, pamoja na mauaji katika Jiji la Davao wakati Rodrigo Duterte alipokuwa meya wa mji huo kabla ya kuwa rais.
Maelfu waliuawa
Zaidi ya watu 6,000 waliuawa katika operesheni za kupambana na dawa za kulevya chini ya uongozi wa Duterte, kulingana na data rasmi iliyotolewa na Ufilipino. Waendesha mashtaka wa ICC wanakadiria idadi ya vifo kuwa kati ya 12,000 na 30,000.
Rais huyo wa zamani anasalia kuwa mtu maarufu sana na watu wengi nchini Ufilipino ambao waliunga mkono marekebisho yake ya haraka ya uhalifu. Anasalia kuwa kikosi chenye nguvu cha kisiasa na yuko mbioni kurudisha kiti chake cha umeya katika uchaguzi wa katikati ya muhula mwezi Mei.
Akijieleza kuwa muuaji, Rodrigo Duterte amewaagiza maafisa wake wa polisi kuwapiga risasi watu wanaoshukiwa kuhusika na biashara ya dawa za kulevya ikiwa maisha yao yako hatarini. Altetea kwa dhati vita vyake vya mauaji dhidi ya dawa za kulevya mwezi Oktoba, kama sehemu ya kikao chake cha Bunge la Seneti kilichochunguza mauaji ya watu wengi katika kipindi hicho. “Usihoji sera zangu, kwa sababu siombi msamaha, wala visingizio. “Nilifanya nilichopaswa kufanya na, mkiamini au la , nilifanya kwa ajili ya nchi yangu,” Rodrigo Duterte alisema.