
Rais wa zamani wa Ufilipino Rodrigo Duterte siku ya Ijumaa Machi 14, 2025, amefikishwa kwa mara ya kwanza mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) huko Hague. Anashutumiwa kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa kuamuru mauaji ya makumi ya maelfu ya watu nchini Ufilipino kwa jina la “vita vyake dhidi ya dawa za kulevya.” Familia za wahasiriwa zilikusanyika kutazama kesi ya Duterte kwa nji ya video na wengine walikuwepo Hague.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Kutoka kwa mwanahabari wetu huko Manila, Nemo Lecoq-Jammes
Kwenye mapaja ya wanawake wanane walioketi mbele ya televisheni kubwa kuna picha za wapendwa wao waliouawa chini ya amri ya Duterte: “Huyu ni mume wangu, alikuwa na umri wa miaka 34 alipofariki. “
Duterte alishiriki kesi hiyo kwa njia ya video kwa sababu ya uchovu na ugonjwa. Wanawake waliokuwepo katika chumba cha mahakama wamesema ni mkakati wa kuteswa.
Jane Lee alipoteza mume wake, aliuawa miaka minane iliyopita. Leo, hisia zake zimechanganyika: “Siwezi kuamini kuwa Duterte ni dhaifu sasa. Hakufika hata mahakamani kutokana na hali yake ya afya mbaya. Lakini pamoja na familia nyingine, bado tuna furaha sana, kwa sababu angalau alikamatwa na yuko Hague, katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu. “
Kesi hiyo ilisikilizwa haraka. Ilidumu kama dakika ishirini tu, na rais wa zamani ilibidi tu kuthibitisha utambulisho wake. Lakini Kristina Conti, wakili wa familia za wahasiriwa wa vita dhidi ya dawa za kulevya, amesema siku hii ni ya kihistoria: “Ni ofisi ya mwendesha mashtaka, dhidi ya Rodrigo Duterte. Ni ukweli kwa njia moja, kwa sababu inaonyesha kweli kwamba sasa ni suala la kisheria. Ambapo hapo awali, tuliiita “hali ya Ufilipino.”
Kesi inayofuata ya Rodrigo Duterte imepangwa kufanyika Septemba huko Hague. Hadi wakati huo, waathiriwa wanatumai hataruhusiwa kurejea Ufilipino. Kampeni ya rais huyo wa zamani dhidi ya dawa za kulevya, iliyozinduliwa mwaka 2016, iligharimu maisha ya maelfu ya watu nchini humo: angalau vifo 6,000, kulingana na data ya Ufilipino, na kati ya vifo 12,000 na 30,000 kulingana na makadirio ya waendesha mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).