Ufaransa yapiga marufuku bendera ya Palestina katika mechi ya soka kati ya nchi hiyo na Israel

Mamlaka za Ufaransa zimetumia kisingizio cha fujo zilizotokea wiki iliyopita nchini Uholanzi, kupiga marufuku watazamaji kubeba bendera ya Palestina kwenye mechi ya soka baina ya nchi hiyo na utawala wa Kizayuni wa Israel itakayochezwa siku ya Alkhamisi katika kitongoji cha Paris.

Gavana wa Paris Laurent Nunez ameviambia vyombo vya habari vya Ufaransa: “ni bendera za Ufaransa na Israel pekee na jumbe zinazounga mkono timu ndizo zitazoruhusiwa. Viwanja sio mahali pa jumbe za kisiasa, hii ni sheria”.

Imeelezwa kuwa maafisa wa masuala ya usalama katika uwanja wa michezo wa Stade de France watawafanyia upekuzi mashabiki na kukagua vitambulisho vyao mara mbili kwenye uwanja huo ulioko Saint-Denis, kitongoji cha kaskazini mwa Paris; na yeyote atakayekaidi hataruhusiwa kuingia uwanjani.

Polisi waliovalia nguo za kawaida watashika doria katika uwanja wakati wote wa mechi, na stendi za karibu na uwanja zitaachwa tupu. Kikosi maalumu cha polisi, RAID, kitasimamia usalama wa wachezaji wa timu ya utawala wa Kizayuni.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari nchini Ufaransa, Rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron yeye mwenyewe amepanga kuhudhuria mechi hiyo, ambayo itafanyika wakati utawala wa Kizayuni wa Israel unaendeleza mashambulio ya kinyama katika Ukanda wa Ghaza, ukiwa hadi sasa umeshawaua shahidi zaidi ya Wapalestina 43,000 na kuwajeruhi wengine karibu 103,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Itakumbukwa kuwa, siku ya Alkhamisi iliyopita mashabiki wa timu ya Maccabi Tel Aviv walizusha fujo na machafuko nchini Uholanzi kwa kuwashambulia waungaji mkono wa Palestina na kuwachokoza kabla na wakati wa mechi ya soka ya Ligi ya Ulaya UEFA kati ya timu hiyo ya Kizayuni na Ajax Amsterdam ya Uholanzi.

Jumla ya watu 63 walikamatwa mjini Amsterdam kuhusiana na machafuko ya kabla na baada ya mechi hiyo…/