Alhamisi wiki iliyopita, miaka miwili tangu kupitishwa kwa mageuzi yenye utata ya kuongeza umri wa kustaafu, Bunge la Kitaifa la Ufaransa lilipiga kura kufuta mageuzi hayo.
Hata hivyo, wakati habari ilizusha utata kisiasa kwa sababu chama cha siasa kali za National Rally kiliusadia upinzani wa mrengo wa kushoto kupata wingi katika kura hiyo, uamuzi huo haujakuwa na matokeo yoyote ya kisheria.
Hali hii inaashiria namna serikali ya Rais Emmanuel Macron imeendelea kukwama katika juhudi zake za kusukuma mbele mageuzi ya kimuundo tangu uchaguzi wa bunge wa majira ya joto mwaka jana, ambapo haikupata wingi wa moja kwa moja bungeni.
Lakini tofauti na hali hiyo, kwenye eneo la sera za kumbukumbu, wabunge wamepiga hatua kubwa. Wiki iliyopita, sambamba na azimio juu ya umri wa kustaafu, wamepitisha pia maandiko matatu yenye malengo ya kurekebisha au kutambua upya matukio ya kihistoria.
Alfred Dreyfus apandishwa cheo baada ya kifo
Mnamo Juni 2, bunge la Ufaransa lilipiga kura kwa kauli moja kumpandisha cheo baada ya kifo Alfred Dreyfus kuwa brigedia jenerali. Afisa huyo wa Kiyahudi alihukumiwa kimakosa mwaka 1894 kwa tuhuma za uhaini, kwa msingi wa ushahidi wa kughushi uliodai kuwa alikuwa ametoa siri za kijeshi kwa Ujerumani.
Baada ya kuhukumiwa, Dreyfus alifungwa kwa miaka minne kwenye gereza maarufu la Devil’s Island, nje ya pwani ya Guiana ya Kifaransa.
Kesi hiyo ilikuwa na athari pana hata kwenye diplomasia ya wakati huo, kwa kuwa chimbuko la Dreyfus kutoka familia ya Kiyahudi wa Alsace-Lorraine — eneo lililotwaliwa na Ujerumani — lilimfanya kuwa shabaha ya chuki za kitaifa zilizokithiri Ufaransa.
Mwandishi mashuhuri Émile Zola aliandika insha yake maarufu “J’accuse…!” akimtetea Dreyfus, hatua iliyochangia pakubwa kusafishwa kwa jina lake na kurejeshewa heshima ya kijeshi mwaka 1906. Hata hivyo, baada ya kushiriki Vita ya Kwanza ya Dunia kama luteni kanali, Dreyfus hakuweza kurejea kwa cheo chake cha awali.
Kupandishwa kwake cheo baada ya kifo bado kunasubiri idhini ya Seneti. Mbunge wa Alsace, Charles Sitzenstuhl, kutoka chama cha Renaissance cha Rais Macron, aliwasilisha pendekezo hilo huku akionya: “Chuki dhidi ya Wayahudi iliyomkumba Dreyfus si jambo lililopitwa na wakati,” alisema.
Utambuzi wa waliorejea kutoka Indochina
Siku moja baada ya kura ya Dreyfus, Bunge la Kitaifa lilipitisha pia sheria ya kutambua na kufidia waliorejea Ufaransa kutoka Indochina ya Kifaransa, baada ya kumalizika kwa utawala wa kikoloni katika mataifa ya Vietnam, Laos na Cambodia mwaka 1954.
Takriban watu 44,000 walihamishiwa Ufaransa, wakiwemo maafisa wa kikoloni, wanajeshi na familia zao, pamoja na washirika wa Kifaransa na wanawake wa huko waliounganishwa nao.
Kati yao, watu 4,000 hadi 6,000 walihifadhiwa kwenye kambi za muda zisizo na huduma bora, huku wakikumbwa na sera za kudhalilisha kama marufuku ya kutoka nje na kumiliki bidhaa za kifahari.
Sheria mpya, iliyopendekezwa na Chama cha Kisoshalisti, sasa inatoa fidia ya kifedha kulingana na muda mtu alivyokaa kambini. Inakadiriwa kuwa hadi watu 1,600 wanaweza kunufaika.
Je, fidia kwa Haiti?
Mnamo Juni 5, Bunge la Ufaransa lilipitisha azimio linalolenga kutambua “deni la mara mbili” kwa Haiti linalotokana na makubaliano ya mwaka 1825.
Mwaka huo, Ufaransa iliilazimisha Haiti — iliyojitangazia uhuru mwaka 1804 — kulipa faranga za dhahabu milioni 150 kama masharti ya kutambuliwa rasmi na kufidia hasara ya mali za kikoloni, ikiwemo mapato kutoka kwa watumwa.
Haiti ililazimika kulipa deni hilo kwa miongo kadhaa, hali iliyochangia kudidimia kwa uchumi wa nchi hiyo na kusababisha umaskini wa muda mrefu.
Azimio hilo, lililowasilishwa na Chama cha Kikomunisti, linatoa wito wa kutambua, kulipa na kufidia deni hilo. Hata hivyo, halijajumuisha hatua mahsusi za kisiasa au makubaliano ya kifedha. Chama cha National Rally kilipiga kura kupinga azimio hilo.
Historia ndefu ya siasa za kumbukumbu
Ufaransa ina historia ya kushughulikia siasa za kumbukumbu. Mwaka 2001, sheria maarufu ya Taubira ilitambua biashara ya watumwa na utumwa kama uhalifu dhidi ya ubinadamu, na mada hiyo ikaingizwa kwenye mtaala wa shule.
Mnamo Oktoba 2006, bunge lilipitisha mswada wa kufanya kuwa kosa la jinai kukana mauaji ya halaiki ya Waarmenia ya mwaka 1915, lakini sheria hiyo haikupata nguvu ya kisheria baada ya kushindwa kupitishwa na Seneti.
Jitihada nyingine chini ya Rais Nicolas Sarkozy pia ziligonga mwamba baada ya Baraza la Katiba kuamua kuwa sheria hiyo ingewawanyima watu haki ya kujieleza na kufanya utafiti.
Mfano mwingine ni wa wanajeshi wa kikoloni wa Kiafrika walioipigania Ufaransa kwenye vita kuu mbili, waliotajwa kama “Senegalese riflemen.”
Kwa miongo mingi walipokea pensheni ndogo zaidi ikilinganishwa na wenzao Wafaransa, hasa waliorejea barani Afrika baada ya ukoloni.
Ilikuwa mwaka 2009 ambapo Rais Sarkozy aliamua kupandisha pensheni zao hadi kufikia kiwango sawa.
Ishara ya ukomavu wa kijamii au maneno matupu?
Kuongezeka kwa hatua kama hizi kumewagawa wachambuzi wa siasa. Wapo wanaoziona kama ishara ya ukomavu wa kijamii na utayari wa kuchukua wajibu wa kihistoria.
Lakini wapo pia wanaoona kuwa katika bunge lililokwama kisiasa, ni rahisi kupitisha hatua za ishara kuliko mageuzi ya kweli kwenye sekta kama pensheni, elimu na bajeti.
Makala hii ilitafsiriwa kutoka Kijerumani