Uendelevu wa viwanda na fikra za mwalimu

Ukosefu wa ajira ni moja ya changamoto ambazo zinawakumba wakazi wa Tanga na vitongoji vyake. Tangu kipindi ambacho viwanda hivyo vilifungwa, waliokuwa wameajiriwa walijikuta wakipoteza ajira, huku wakiendelea kuishi maisha duni.

Gazeti la Mwananchi la Juni 17, 2024 lilimnukuu Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian akisema kuwa Serikali ya mkoa imekubaliana kuitisha kikao na wafanyabiashara walionunua viwanda ili kufahamu sababu zilizochangia kuvifanya viwanda hivyo kushindwa kufanya kazi.

Katika kikao hicho, Burian alisema iwapo wawekezaji watashindwa kutoa mikakati mizuri ya uendelezaji viwanda hivyo, ushauri unaweza kutolewa juu ya kubadilisha huduma na matumizi ya viwanda hivyo.

Alifafanua kuwa hatua hiyo itasaidia Tanga kuondokana na hali ya uwepo wa magofu sehemu ambazo wengine wameonesha nia ya kufanya uwekezaji wenye manufaa.

“Uwepo wa sera madhubuti katika usimamizi wa viwanda, hususan katika mipango ambayo inakuwa imewekwa na Serikali, ni moja ya mambo ambayo wadau wameyashauri kwa Serikali yao, hatua ambayo inaweza kusaidia kuviepusha viwanda hivyo na hatari ya kufungwa kwa mara nyingine,” alisema.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Zidumu Fikra za Baba wa Taifa, Dk Muzammil Kalokola anasema serikali inapaswa kurejea misingi iliyowekwa na Mwalimu Julius Nyerere kupitia Azimio la Arusha.

“Viwanda vyote tunavyozungumzia (Tanga) vilijengwa wakati wa Mwalimu Nyerere. Yeye aliweka misingi imara kuhusu masoko, utaalamu na mipango ya maendeleo,” anasema Dk Kalokola.

Kalokola amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuunda mazingira bora ya uwekezaji. Hatua hii itasaidia kuvutia wawekezaji wapya na kuimarisha viwanda vilivyopo.

Pia anasema kuna haja ya kuanzisha mikakati ya kutoa mafunzo kwa wafanyakazi ili kuongeza ujuzi na ufanisi katika uzalishaji wa bidhaa. Mafunzo haya yatasaidia viwanda kuendana na mahitaji ya soko la kisasa na kuongeza ushindani.

Mwenyekiti huyo anasema Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha sera zinazotumika zinawiana na mahitaji ya soko na mazingira ya biashara ya kisasa. “Hapa tatizo si kufufua viwanda hivyo vilivyokufa tu kama mkakati wa kuiokoa Tanga kwa sababu pengine kwa sasa hivi havina manufaa tena kama ilivyokuwa wakati huo ambapo hakukuwa na viwanda vingine vikubwa jijini Tanga,” anasema.

 Muda umepita. Kuingia kwa teknolojia mpya, bidhaa mpya na viwanda vingine kunafanya mazungumzo na mikakati iwe si kufufua viwanda hivyo tu, bali kujenga viwanda vingine kama inayoonekana katika mkakati wa kimkoa na kitaifa.

“Tukumbuke kuwa baadhi ya sababu ya kudodora kwa viwanda hivyo ilikuwa ni ushindani wa bidhaa za bei nafuu kutoka nje, ambapo biashara za chuma kutoka nje, hasa Asia ziliathiri uwezo wa kiwanda kushindana sokoni,” anasema

Sababu nyingine ni gharama kubwa za uzalishaji zikijumuisha umeme, upatikanaji wa malighafi kwa bei rahisi na changamoto za kiutawala jambo ambao liliongeza gharama za uzalishaji.

Sababu hizo pamoja na mlolongo wa kodi badobado zipo hivyo ufufuaji uende sambamba na kuangalia masuala hayo ili kuwawezesha wenye viwanda kuviendesha kwa ufanisi.

Kwa kushirikiana, wadau wote wanapaswa kuhakikisha kuwa viwanda vya Tanga vinakuwa na nguvu na vinaweza kuchangia kikamilifu katika uchumi wa taifa kwa njia endelevu. Hatua hizi si tu zitaokoa viwanda, bali pia, zitaleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa mkoa mzima wa Tanga na taifa kwa jumla.