
London, England. Leo na kesho ni kivumbi cha Ligi ya Mabingwa barani Ulaya ambako rekodi zinatarajiwa kuwekwa katika mechi mbalimbali za michuano hiyo mikubwa barani Ulaya.
Mechi kubwa zaidi kwa leo ni ile ya Bayern Munich na PSG itakayopigwa katika dimba la Allianz Arena, huko Munich kuanzia saa 5:00 usiku. Mechi hii inaonekana kuwa ni ya mabao kutokana na historia.
Tangu timu hizi zianze kukutana kwa mara ya kwanza mwaka 1994/95 hakuna mchezo wowote uliomalizika kwa sare.
Kiuumla zimekutana mara 13 na Bayern Munich imeshinda mechi saba wakati PSG ikishinda sita na mara ya mwisho kukutana ilikuwa msimu wa 2022/23 katika hatua ya 16 bora ambapo Bayern iliibuka na ushindi katika mechi zote.
PSG inaingia katika mchezo huu ikiwa na hali mbaya kwani inashika nafasi ya 25 katika msimamo na kwenye mechi nne ilizocheza hadi sasa imeshinda moja tu tofauti na wapinzani wao Bayern Munich ambayo inashikilia nafasi ya 17 baada ya kushinda mechi mbili kati ya nne.
Timu zote zinahitaji ushindi kwa namna yoyote kwa ajili ya kusogea nafasi za juu zaidi na ikiwa Bayern itashinda inaweza kupanda hadi nafasi ya nane juu kwa sababu itafikisha alama tisa sawa na Aston Villa na Borussia Dortmund.
Mbali ya mchezo huu ambao unaonekana kuwa utavutia watu wengi, leo kutakuwa na mechi mbalimbali za vigogo wengine.
Mechi za mapema itakuwa ni ile ya AC Milan itakayokuwa ugenini kuvaana na SK Slovan Bratislava, pia Sparta Praha itakayoikaribisha Atletico Madrid, mechi zote hizi zitapigwa saa 2:45 usiku.
Milan na Atletico zote zina pointi sita na hazijaanza vizuri michuano hii ambapo kwa sasa zipo katika nafasi za kucheza hatua ya mtoano kabla ya kuingia 16 bora.
Barcelona itakuwa nyumbani kuvaana na Brest katika mechi ambayo inatarajiwa kuwa na ushindani sana kutokana na viwango vya timu zote.
Brest imeonyesha ubora mkubwa tangu kuanza kwa michuano hii na sasa inashika nafasi ya nne wakati Barca ikiwa ya sita.
Ikiwa Barca itashinda inaweza kusogea hadi nafasi ya pili ingawa itategemea na matokeo ya timu nyingine na pia Brest ikipata ushindi inaweza hata kuishusha Liverpool ikiwa itapoteza.
Manchester City ambayo imepoteza mechi tano mfululizo katika michuano yote itakuwa na nafasi ya kujiuliza dhidi ya Feyenoord leo ambapo ikishinda inaweza kusogea juu zaidi kutoka nafasi ya 10 ilipo sasa.
Arsenal itakuwa na kibarua mbele ya timu ya zamani wa Ruben Amorim, Sporting Lisbon ambayo mechi iliyopita iliibamiza Man City mabao 4-1.
Vigogo wengine Inter Milan watakuwa nyumbani kucheza na RB Leipzig na mechi zote hizi zitachezwa saa 5:00 usiku ukiondoa zile mbili za mapema.
MECHI NYINGINE LEO
Leverkusen v RB Salzburg (Saa 5:00 usiku)
Young Boys v Atalanta (Saa 5:00 usiku)