
London, England. Kila mtu atavuna alichopanda. Ndicho unachoweza kusema juu ya mfumo mpya wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu na kwa kesho Jumatano zitapigwa mechi za mwisho za hatua ya makundi inayocheza kwa mfumo wa ligi ili kupata timu zitakazoingia kwenye raundi ya mtoano.
Kesho kila timu itacheza mechi yake ya nane kwenye hatua hiyo ya League Phase, hivyo viwanja 18 vya Ulaya vitawaka moto kwa muda mmoja ili kuepuka habari za kupanga matokeo kwenye mchakato wa kuwania tiketi ya mtoano kwenye hatua ya 16 bora.
Bado kuna vita kali ya kupambania kwenye michuano hiyo na timu nane za juu zitafuzu moja kwa moja kwenye hatua 16.
Timu ya kuanzia nafasi ya tisa hadi 24 kwenye msimamo zitacheza mechi ya mchujo, nyumbani na ugenini ili kupata nyingine nane zitakazokwenda kuungana na nane za juu kuunda timu 16 zitakazocheza kwenye hatua ya mtoano.
Msimamo unavyosoma vigogo Paris Saint-Germain na Manchester City vitakuwa kwenye hatari ya kushindwa kutinga hatua ya mtoano endapo kama zitashindwa kupata ushindi kwenye mechi zao za mwisho kesho.
Kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo, Liverpool na Barcelona ndizo pekee kimahesabu zimeshafuzu kucheza hatua ya 16, ambako miamba ya Anfield inayonolewa na Mdachi Arne Slot imenyakua pointi nyingi zaidi hadi kufikia sasa, ikiwa imeshinda mechi zote saba.
Hiyo kesho utakwenda kuwa usiku wa kibabe sana kwenye soka hilo la mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuna timu kibao zitaingia uwanjani zikitambua zitalazimika kushinda ili kuendelea kuwapo kwenye michuano hiyo.
Katika kuupamba usiku huo wa kibabe kabisa, hizi hapa mechi tano za kuzitolea macho katika mchakamchaka huo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya zikichezwa mechi zao za mwisho kukamilisha hatua ya League Phase.
- Brest vs Real Madrid
Baada ya kuanza vibaya, Real Madrid itahitaji kushinda mechi hiyo iliyobaki ili kuendelea kubaki kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na wenyewe ndiyo mabingwa watetezi. Kwa sasa kikosi hicho cha Kocha Carlo Ancelotti kinashika nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi, hivyo itahitaji ushindi ili kumaliza ndani ya nane bora kufuzu hatua ya mtoano moja kwa moja bila ya kuhitaji mechi za mchujo.
Los Blancos itahitaji kushinda mechi hiyo itakayopigwa Stade Brestois 29, lakini wapinzani wao ambao ni klabu ya Ufaransa, yenyewe ipo kwenye nafasi ya 13 katika msimamo, inahitaji kufuzu pia hatua ya 16 bora. Mechi hiyo inatazamiwa kuwa na upinzani mkali ndani ya uwanja.
2. Man City vs Club Brugge
Kiwango bora cha Manchester City chini ya Kocha Pep Guardiola kimeshuka sana msimu huu. Mabingwa hao wa Ligi Kuu England kwa sasa ipo nafasi ya 25 katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kipigo kutoka kwa PSG, Jumatano iliyopita. Kutokana na hilo, Man City inahitaji kuichapa Club Brugge kwenye mchezo wao wa mwisho utakaopigwa uwanjani Etihad ili kupata tiketi ya kuingia kwenye mechi za mchujo ili kukamatia tiketi ya mtoano.
Hata hivyo, Club Brugge nayo ina kitu cha kupambania kwenye mechi hiyo. Yenyewe inashika nafasi ya 20 kwenye msimamo wa ligi hiyo na inahitaji pointi moja tu kutinga hatua ya mtoano.
3. Lille vs Feyenoord
Lille na Feyenoord zitakutana kwa mara ya kwanza kwenye historia yao na hakika mechi hiyo ina mengi ya kupigania. Timu hizo zote mbili zimekusanya pointi 13 hadi sasa, zikishika nafasi ya 11 na 12 kwenye msimamo. Hata hivyo, timu itakayoshinda tu kwenye mechi hiyo ndiyo itakayokuwa na uhakika wa kumaliza kwenye nafasi nane za juu katika msimamo huo ili kufuzu moja kwa moja kwa hatua ya mtoano.
Kama kuna mechi tamu ya kuitazama, hii ni moja wapo kwa sababu kila timu itapigania tiketi ya kufuzu moja kwa moja kwenye hatua ya 16 bora kwenye mikikimikiki hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
4. Aston Villa vs Celtic
Utakwenda kuwa usiku wa kipekee kabisa huko Villa Park wakati Aston Villa ya kocha Unai Emery itakaposhuka uwanjani kukipiga na Celtic FC. Timu zote mbili zina uhakika wa kufuzu hatua ya mtoano kupitia mchujo, lakini Aston Villa ina nafasi ya kuwamo kwenye nane bora ili kufuzu moja kwa moja kwenye mtoano huyo wa hatua ya 16 bora endapo kama itaibuka na ushindi katika mchezo huo wa kesho.
Kinachovutia wengi ni kwamba mechi hiyo itakutanisha mabingwa wawili wa zamani wa Kombe la Ulaya na hakika shughuli itakuwa pevu huko Villa Park.
5. VfB Stuttgart vs PSG
Zikishika nafasi ya 24 na 22 mtawalia, VfB Stuttgart na PSG zote zimebeba matumaini ya kufuzu hatua ya mchujo wa kuwania tiketi ya kucheza mtoano wa 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Miamba ya Ujerumani, Stuttgart inapambana kuhakikisha inaendelea kubaki kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na itakuwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2009/10.
PSG itaingia kwenye mechi hiyo ya ugenini ikiwa na mzuka mkubwa baada ya ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Man City, lakini wachezaji wao itawabidi kupambana kwelikweli kukutana na joto la mashabiki wa uwanjani MHPArena.
Mechi nyingine za mwisho
Kwenye mchakamchaka huo, mechi nyingine za mwisho Barcelona itakipiga na Atalanta, Bayer Leverkusen itacheza na Sparta Prague, Bayern Munich na Slovan Bratislava, Borussia Dortmund itacheza na Shakhtar Donetsk, Dinamo Zagreb na AC Milan, Girona itamaliza ubishi na Arsenal, Inter na AS Monaco, Juventus itacheza na Benfica, PSV na Liverpool, RB Salzburg itamaliza kazi na Atletico Madric, Sporting CP na Bologna, Sturm Graz na RB Leipzig na Young Boys itamalizana na FK Crvena Zvezda.