Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) pekee ndicho chenye uhakika wa malazi ya wanafunzi, huku vyuo vingine vikiwa na wastani wa asilimia 30 hadi 50.
Hayo yamesemwa leo Jumanne, Aprili 8, 2025 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati akijibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Dk Paulina Nahato.
Akiuliza maswali hayo, Dk Nahato amehoji Serikali imejipangaje kuhakikisha wanafunzi wanaokwenda vyuo vikuu wanapata mahali pa kulala.
Aidha, amesema Chuo Kikuu cha Muhimbili katika eneo la Mlongazila jijini Dar es Salaam, kina eneo kubwa la kuweza kujengwa hosteli, lakini wanafunzi wanaendelea kubanana Muhimbili.
Amehoji kwanini wasipewe watu binafsi eneo hilo ili wajenge hosteli kwa ajili ya wanafunzi hao.

Akijibu maswali hayo, Profesa Mkenda amesema chuo ambacho wana uhakika wa wanafunzi kupata sehemu ya malazi ni Udom, wengine ni wastani wa asilimia 30 hadi 50.
“Kama nilivyojibu swali la msingi, hivi sasa Serikali inawekeza katika sehemu mbalimbali kwa ajili ya kupanua wigo nafasi za kulala na kuvutia PPP (Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi) kuwekeza,” amesema.
Kuhusu Mlongazila, Profesa Mkenda amesema ni miongoni mwa sehemu wanayowekeza ili kuongeza makazi ya wanafunzi.
Katika swali la msingi, Dk Nahato amehoji Serikali ina mpango gani wa kupunguza uhaba wa mabweni katika vyuo vikuu vya umma.
Akijibu swali hilo, Profesa Mkenda amesema Serikali inatambua changamoto ya uhaba wa malazi ya wanafunzi katika vyuo vikuu vya umma nchini.
Amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali inaendelea na ujenzi wa mabweni mapya 26 katika kampasi 12 za vyuo vikuu vya umma nchini.
Profesa Mkenda amesema mabweni hayo yakikamilika yatakuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 5,987 kwa wakati mmoja.
Amesema ujenzi wa majengo ya mabweni hayo unatarajiwa kukamilika mwaka 2026.
Waziri huyo ametoa wito kwa sekta binafsi kuwekeza kwenye ujenzi wa hosteli katika maeneo ya vyuo vikuu, ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma ya malazi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.