Udhaifu wa ushahidi wawachia huru walimu wawili kesi ya mauaji

Geita. Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Geita imewaachia huru walimu wawili waliokuwa wakikabiliwa na shitaka la kuua bila kukusudia, baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha kesi yao pasipo kuacha shaka.

Hukumu hiyo imetolewa leo Mei,19,2025 na Jaji wa Mahakama hiyo Griffin Mwakapeje na kueleza kuwa ushahidi uliowasilishwa haukuweza kuthibitisha kama walimu hao walihusika moja kwa moja katika kifo cha Atusi Butoto.

Walimu waliohusishwa katika kesi hiyo ya mwaka 2025 ni Friday Mwaisyelage na Richard Petro  waliotuhumiwa kumuua Butoto  bila kukusudia kinyume na kifungu cha 195&198 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Walimu wawili waliokuwa wakishtakiwa kuua bila kukusudia wakipongezwa na ndugu na jamaa mahakamani mara baada ya kuachiwa huru.

Washtakiwa hao kwa pamoja walidaiwa kuwa Septemba 26, 2024 huko Kabugozo Wilaya ya Geita marehemu alirudi nyumbani kwake akiwa amelewa na baada ya kula chakula cha usiku alitaka mkewe ampe tendo la ndoa lakini mkewe alikataa kutokana na kuwa kwenye siku zake.

Ilidaiwa baada ya kukataa, mume wake alianza kumpiga akimtuhumu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwalimu mwenzake ambaye ni mshtakiwa wa pili.

Kutokana na kipigo mke wa marehemu ambaye ni mwalimu wa Shule ya msingi Kabugozo alipiga kelele za kuomba msaada na walimu wenzake walienda kutoa msaada.

Inadaiwa walimu hao pamoja na majirani walimpiga marehemu na kufanikiwa kukimbia, lakini baada ya muda mkewe aliwaomba walimu wenzake wamtafute  maana alitishia kujiua na wao walimtafuta kisha kumkuta ameanguka kwenye shamba la shule.

Alipelekwa kituo cha polisi na kupatiwa PF3 na kupelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu na baada ya siku tano alipoteza maisha.

Jaji Mwakapeje amesema mambo ya kuthibitisha katika kesi hiyo ni kama kweli marehemu alipoteza maisha, na upande wa mashitaka uthibitishe kitendo kisicho halali  na kithibitishwe pasipo kuacha shaka.

Amesema hakuna ubishi kuwa  marehemu kweli alipoteza maisha kwa kuwa uchunguzi wa daktari na mke wa marehemu umethibitisha kuwa kweli hayuko tena duniani.

Amesema kiini cha pili ni kama kifo hicho kilitokana na kitendo halali kilichosababishwa na washtakiwa .

Jaji mwakapeje amesema ubishi unaoshindaniwa katika kesi hiyo ni nani alisababisha je, kilisababishwa na majeraha, kipigo, kuvilia  damu lakini hata hivyo uchunguzi wake una mchanganyiko.

Ushahidi wa shahidi wa tano, Raphael Makoye ambaye ni daktari aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu ulieleza kifo hicho  kimesababishwa na kukosa hewa kulikotokana na majeraha.

Daktari huyo alieleza aliona mwili ukiwa na majeraha kwenye paji la uso lakini halionyeshi kuvilia damu, na alipoulizwa na upande wa utetezi kama alifanya upasuaji alidai hakupasua popote.

Jaji Mwakapeje amesema ushahidi huo uko kihisia zaidi kuliko kitaalamu na kuwa ushahidi kwa njia ya mdomo alioutoa unakinzana na ule wa kimaandishi.

Mahakama hiyo imeweka mkazo kuwa ripoti ya uchunguzi ya kidaktari lazima ijazwe kwa umakini na kitaalamu  na sio kwa maneno  au  kuongea kwa ujumlajumla kunafanya chanzo kisiwe na nguvu.

Amesema taarifa ya kitabibu ina upungufu mkubwa wa kuthibitisha sababu za  kifo.

Aidha mkanganyiko wa mashahidi wa 1,2,3 na 5 na kukosekana kwa ushahidi wa kisayansi unaounga mkono uthibitisho wa kisayansi, upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha sababu za kifo kama ni  kukosa hewa, kupigwa au kuanguka kwenye mwamba.

Jaji Mwakapeje amesema upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha pasipo kuacha shaka na ushahidi unajikanganya na kushindwa kuacha shaka, hivyo Mahakama haijawakuta na hatia na kuwaachia huru.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *