Udanganyifu waikoroga NHIF, vituo vya afya -1

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya vituo vya afya vikilalamika kucheleweshewa malipo na mengine kukataliwa hivyo kushindwa kujiendesha, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema unalipa madai yaliyo halali kwa wakati.

Miongoni mwa vituo vya afya vinalalamika kucheleweshewa malipo kwa hadi miezi sita kutokana na hoja za kihasibu na madai ya kuwapo udanganyifu, huku wakati mwingine malipo hukataliwa kabisa.

Kutokana na hilo, wapo wenye vituo wanaodai wamelazimika kutokutoa huduma kwa wanachama wa NHIF na wengine wamefunga vituo kwa kushindwa kuviendesha.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk Irene Isaka, alipoulizwa na Mwananchi kuhusu madai hayo, anasema:

“Madai haya hayana ukweli wowote. Kwa sasa mfuko unalipa madai yaliyo halali kwa wakati na hakuna kituo kilichofungwa kwa sababu ya kucheleweshewa malipo. Vituo vinafungwa kutokana na changamoto za uendeshaji wa vituo vyenyewe.”

Kwa mujibu wa wenye vituo vya afya, huduma zenye changamoto kubwa zaidi katika uhakiki wa malipo ni zinazotolewa kwa kundi la wazee na watoto chini ya miaka mitano.

Inadaiwa NHIF imekuwa ikihoji ni kwa nini huduma fulani ya vipimo imetolewa au ni kwa nini dawa aina hii imetolewa, licha ya kuwa daktari aliyemuona mgonjwa ana kwa ana alipendekeza matibabu kutokana na hali na historia ya mgonjwa.

“Nyaraka tunazotuma NHIF kwa ajili ya malipo, nyingi zinazowahusu wazee zimekuwa na hoja za kihasibu na huwa hatulipwi, ingawa inajitokeza kwa wateja wengine pia, hasa zile za watoto chini ya miaka mitano,” anasema mmiliki wa kituo cha afya binafsi jijini Dar es Salaam aliyeomba kutokutajwa jina.

“Kinachoshangaza, unakuta ni hospitali ya umma na aliyependekeza dawa au kipimo kwa mgonjwa ni daktari mbobezi anayejua kwa nini alitoa dawa ile au alishauri kipimo kile, lakini wanasema dawa au kipimo hakikufaa kupewa mgonjwa,” anasema mtumishi katika moja ya hospitali za umma jijini Dar es Salaam.

“Umemtibu mgonjwa wa NHIF leo, malipo unalipwa baada ya miezi sita. Sisi kama si ruzuku ya Serikali sijui ingekuwaje. Na hapo bado hawajatukata malipo yetu,” anasema kiongozi wa hospitali moja ya kanda ambaye hakutaka kutaja jina.

Daktari mwingine katika hospitali binafsi anasema: “Unaweza kuona mgonjwa amekuja kichwa kinamuuma, mwili umechoka, ana homa na mwingine anakohoa pia. Huyu daktari utampima mkojo, malaria, full blood picture. Sasa wao wanahoji kwa nini ulimpima vipimo vyote hivyo.

“Inashangaza, mimi ndiye namuona mgonjwa, nimechukua viashiria nilivyoandika pale, yeye anauliza kwa nini ulimpima full blood picture? Sasa unajiuliza, alitaka mgonjwa atoke maabara vipimo vyote ‘nil’ kisha nimrudishe tena, haiwezekani.”

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Watoa Huduma za Afya Binafsi Tanzania (Aphtha), Dk Samwel Ogillo, anasema baadhi ya vituo vimeacha kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF, hata hivyo si vyote vinaweka wazi sababu.

“Wengine NHIF iliwatoza faini, baada ya kulipa wakawafungia kutoa huduma kwa wanachama wake, wengine walijitoa baada ya kutokulipwa fedha zao,” anasema Dk Ogillo.

Mmiliki wa Polyclinic iliyopo Handeni, mkoani Tanga, mwenye mkataba wa kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF, anasema baada ya mkataba kumalizika hatarajii kuendelea kutoa huduma kwa kushindwa kujiendesha kutokana na changamoto za malipo.

“Niliwatibu wagonjwa kwa miezi sita bila malipo, kuanzia Machi hadi Septemba 2023. Hii ilisababishwa na NHIF kuanza uchunguzi Julai mpaka Septemba, na wakati huo hawakuwa wamenilipa wakidai kulikuwa na udanganyifu.

“Nilitaka kusitisha huduma kwa wateja wa NHIF, lakini wakanisihi niendelee kutoa huduma. Wakati wa ukaguzi wao, walidai risiti nyingine zilikuwa zimefutika, hasa za EFD, sababu zilikuwa za miaka miwili. Walikuwa wanaangalia kama nimelipwa kimakosa au vinginevyo,” anasimulia mmiliki wa kituo cha afya kilichopo Bunju, mkoani Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Aphtha, Dk Egina Makwabe, anasema uamuzi wa kusitisha huduma unaangalia gharama za uendeshaji na faida na kama kuna uendelevu wa kutoa huduma.

“Kituo binafsi kinategemea kipate faida. Bei za kitita cha NHIF zinafaa zaidi kwa vituo vya umma ambavyo vyenyewe vinapata ruzuku kutoka serikalini; hawalipi kodi, mishahara, gharama za ujenzi. Uendeshaji hauwezekani vikajiendesha sawa,” anasema.

Dk Makwabe anasema ni kweli kuna vituo vya afya vimefungwa kwa kuwa vilitoa huduma na havikupata faida. Hata hivyo, anasema hana idadi kamili kwa kuwa vipo vinavyotoa taarifa na vingine havitoi.

Alichobaini CAG

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, katika ripoti iliyotolewa Machi 28, 2024, alizungumzia NHIF kukataa madai ya hospitali za umma.

Katika ripoti ya ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2022/23, alizungumzia masuala yaliyobainishwa wakati wa ukaguzi wa ufanisi wa mashirika hayo kwa sekta ya afya, yakijumuisha NHIF iliyokataa madai yenye thamani ya Sh11.83 bilioni yaliyowasilishwa na hospitali za umma.

“Wakati wa ukaguzi wangu kwa mwaka 2022/23, nilibaini Mfuko wa Bima wa Afya ulikataa jumla ya Sh11.83 bilioni, sawa na asilimia 15 ya madai yote ya Sh76.89 bilioni kutoka hospitali nne za umma,” alisema CAG katika ripoti.

Hospitali hizo alizitaja kuwa ni Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas).

CAG alisema uchambuzi wa mwenendo huo unaonyesha kumekuwa na ongezeko la kukataliwa madai, akisema mwaka wa fedha 2020/21, madai ya Sh3.87 bilioni (sawa na asilimia saba ya madai) yalikataliwa, na katika mwaka wa fedha 2021/22, madai ya Sh8.84 bilioni (sawa na asilimia 10 ya madai) yalikataliwa.

CAG Kichere alisema sababu kuu za kukataliwa ni udanganyifu katika madai na kutokuwapo kwa uhalali wa sababu za kutozingatia taratibu au kanuni zinazohusiana na malipo ya madai.

Nyingine ni kudai mara mbili, matumizi makubwa ya huduma, kutozingatia bei za Mfuko wa Bima na huduma ambazo hazijaonyeshwa katika utambuzi.

Pia husababishwa na ukosefu au ubatili wa nambari za uidhinishaji, kukosa maelezo ya huduma zinazodaiwa baada ya kuthibitishwa, kutokuwapo kwa saini ya mgonjwa au saini ya mgonjwa isiyo sahihi, huduma zisizo ndani ya kifurushi cha Mfuko wa Bima, makosa ya kukokotoa, kuandika dawa nyingi kupita kiasi na kutofuata miongozo ya kawaida ya matibabu.

“Ukwasi wa mashirika haya unaweza kuathiriwa sana kutokana na kukataliwa kwa madai kunakosababisha upotevu wa fedha,” alisema CAG Kichere.

Si hivyo tu, akiwasilisha ripoti ya ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2023/24 Machi 27, 2025, CAG anasema kuna ongezeko la madai ya hospitali yaliyokataliwa, akieleza madhara yake kwa ukwasi.

“Mfuko ulikataa madai ya Sh11.23 bilioni kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, sawa na asilimia 16 ya madai yote yaliyowasilishwa kutoka hospitali za rufaa za mikoa na wilaya.

“Madai hayo yalikataliwa kutokana na makosa ya bei, dozi, bidhaa zisizo sahihi na adha zisizotakiwa. Hali hiyo imeathiri ukwasi wa hospitali hizo kwa kupunguza mapato yaliyotarajiwa,” anasema.

Kauli ya NHIF

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk Isaka, akizungumzia madai ya wamiliki wa vituo binafsi kuhusu malipo, anasema hayana ukweli kwa kuwa mfuko unalipa madai halali kwa wakati na hakuna kituo kilichofungwa kwa sababu ya kucheleweshewa malipo.

Amesema NHIF imesajili vituo vya kutoa huduma 10,089, kati ya hivyo, binafsi ni 1,804. Hivyo, kutokana na sababu mbalimbali hutokea vikasimamisha utoaji wa huduma kwa wanachama wa NHIF, lakini kwa jitihada za pande zote mbili, vingi vimekuwa vinarejeshwa kutoa huduma pale sababu za kusitisha zinapofanyiwa kazi.

Dk Isaka anasema, kuanzia Julai 2024 mpaka Machi 4, alipotoa majibu ya maswali yaliyoulizwa na Mwananchi, ni vituo vitano pekee vilivyositisha huduma, na jitihada za pande zote kutatua changamoto hiyo zinaendelea.

Akizungumzia kuhusu udanganyifu, anasema ni moja ya sababu kubwa za vituo kufungiwa kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF.

“Mfuko umekuwa, kwa kiasi kikubwa, ukipambana na udanganyifu kwa makundi yote. Udanganyifu mkubwa ni mtu kutumia kadi isiyo yake kupata matibabu. Hizi ni miongoni mwa kesi zinazogunduliwa kwa makundi yote bila kujali umri,” anasema.

Dk Isaka, akizungumzia uhakiki wa malipo, anasema unafuata miongozo ya matibabu inayotolewa na Wizara ya Afya. Vilevile, sheria ya mfuko inaelekeza namna ya kuchakata madai.

“Mpaka sasa, mfuko una madaktari wa kawaida 167 waliosajiliwa na Msajili wa Madaktari, na madaktari bingwa 14 wanaoshiriki kazi ya uchakataji wa madai. Hivyo, mfuko una wataalamu wenye uwezo mkubwa katika eneo hilo, tofauti na madai yanayodaiwa kuwa mfuko hauna wataalamu wa kutosha,” anasema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *