Uchunguzi wa maoni wa karibuni uliofanywa na utawala wa Israel umeonyesha kuwa zaidi ya theluthi moja ya vijana Wayahudi wa Marekani wenye umri wa miaka kuanzia 14 hadi 18 wametangaza mshikamano wao na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas.
Uchunguzi huo wa maoni umefanyika baada ya mwaka mmoja tangu utawala ghasibu wa Israel ulipoanzisha vita na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Uchunguzi huo ambao umefanywa na Wizara ya Uhamiaji na Kupambana na Chuki dhidi ya Wayahudi ya Israel umebaini kuwa asilimia 36.7 ya vijana wa Wayahudi wa Marekani waliohojiwa wameafiki au kukubaliana pakubwa na neno “ninasimama katika mshikamano na Hamas”.

Uchunguzi huo wa maoni pia umeonyesha kuwa asilimia 41.3 ya vijana hao wanaamini kuwa utawala wa Israel unafanya mauaji ya kimbari huko Ukanda wa Gaza.
Katika upande mwingine, uchunguzi huo wa maoni umeonyesha kuwa asilimia 66 ya vijana Wayahudi wa Marekani wako bega kwa bega na wanaunga mkono taifa la Palestina.