Uchumi duni watajwa chanzo ongezeko magonjwa sugu kwa jamii

Mbeya. Imebainika kuwa ukosefu wa kipato kwa baadhi ya wananchi ni chanzo cha ongezeko la magonjwa sugu yasiyoambukizwa, kutokana na kukosa fedha kugharamia matibabu na kuzifikia huduma kwa wakati.

Hatua hiyo imetajwa kusababisha baadhi ya wananchi wanaobainika na matatizo ya figo, ini, saratani, afya ya akili kufanyiwa uchunguzi wa maradhi hayo tatizo likiwa limeshakuwa sugu.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Mei 5, 2025 na Mratibu wa huduma za tiba na Daktari bingwa wa uchunguzi wa kutumia mionzi, sumaku na sauti ya mawimbi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, Dk Ngwilo Mwakyusa.

Dk Mwakyusa ameyasema hayo  baada ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya,  Beno Malisa, kuzindua kambi ya madaktari bingwa bobezi 36 wa Mama Samia, kutoka taasisi mbalimbali za afya, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Dk Juma Homera.

Kambi hiyo imeanza leo Jumatatu mpaka Mei 9, 2025 katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya na kuhusisha mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Amesema hali hiyo husababisha wagonjwa kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma, huku wasio na kipato wanakata tamaa na kuishia majumbani na kusababisha usugu wa magonjwa.

“Niwasihi wananchi mikoa ya nyanda za juu kusini, kuchangamkia fursa hii ya uwepo wa kambi ya siku tano ya madaktari bingwa bobezi wa Mama Samia kupata vipimo vya matibabu kwa gharama nafuu,” amesema.

Malisa amewataka wananchi kutumia fursa hiyo ambayo Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imewafikishia maeneo ya jirani.

Amesema wana kila sababu ya kuishukuru Serikali ya awamu ya sita, kwa kusogeza huduma za kibingwa na bobezi kwa wananchi walioshindwa kuzifikia kutokana na changamoto ya kiuchumi.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya, Dk Abdallah Mmbanga amesema kambi hiyo itadumu kwa siku tano.

Amesema wamepokea madaktari bingwa 36 ambao watashirikiana kutoa huduma za kibingwa na uchunguzi kwa wananchi wa ndani na nje ya mkoa huo.

Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Vailet Sikwese amesema awali walikuwa wakilazimika kwenda Dodoma, jijini Dar es Salaam na Hospitali ya KCMC Moshi kupata huduma za kibingwa na bingwa bobezi.

“Kwa kweli nimefurahi sana Serikali kutufikishia huduma, nimepata nafuu kupunguziwa gharama ya kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu, tuna kila sababu ya kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuona wananchi wanyonge,” amesema.

Kuhusu gharama Vailet amesema, licha ya nauli kutoka Mkoa wa Njombe kuja Mbeya, amelipia Sh10,000 kama gharama za vipimo vya uchunguzi pesa ambayo   mwananchi mwenye nia anaweza kuimudu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *