
Katika kochi moja refu maeneo ya Kinondoni nilipata bahati na wasaa wa kukaa na kupiga gumzo na mmoja kati ya viongozi waandamizi wa Serikali hii. Waziri mwenye akili zake timamu na mwenye uelewa wa mambo. Aliniuliza kitu ambacho natembea na jibu lake.
Bahati nzuri tulikubaliana. Aliniuliza kama kuna ‘afya’ yoyote kwa nchi kwa hiki kinachoendelea kwa sasa katika redio nyingi nchini. Redio zetu zimetawaliwa na vipindi vya michezo. Akili ya Mtanzania wa kawaida imehamia huko.
Mheshimiwa akaniambia katika nchi nyingi ambazo zimeendelea asubuhi vipindi vya redio vimetawaliwa na programu za uchumi, jamii, sayansi na mengineyo. Tanzania ukiwasha rekodi yako asubuhi unakabiliana na wachambuzi wakipiga soga la nguvu kuhusu mechi ya jana.
Tanzania ukiwasha redio yako asubuhi unakabiliana na sauti ya mchambuzi “Ile ilikuwa kadi nyekundu halali”. Mwingine atadakia kwa juu “Sidhani, hakuwa mtu wa mwisho licha ya kucheza faulo.” Haya ndio maisha yetu.
Licha ya hawa nilimjibu mheshimiwa kwa heshima na taadhima. “Sababu ni nyinyi mheshimiwa, haya yote yanatokana na nyinyi.” akavua miwani akaipangusa na kuniangalia kwa makini.
Ndiyo, sababu ni wao. Labda yeye ana nguvu anaweza kuwa na nguvu za majadiliano ya hoja. Wengine hawana nguvu hizi. Duniani kote, mara nyingi, kitu kinachoshambuliwa kwa nguvu ni Serikali na taasisi zake. Iwe nchi iliyoendelea, iwe nchi ya uchumi wa kati, iwe nchi masikini.
Raia wa Marekani anailaumu Serikali yake. Kuna mengi anayaona hayapo sawa. Yapo ambayo raia wa Tanzania anaona raia wa Marekani analalamikia ujinga ambao ni sawa na anasa, lakini raia wa Marekani anaona haki yake ya msingi kabisa.
Raia wa Afrika Kusini alalamikia Serikali yake. Raia wa Tanzania analalamikia Serikali yake. Wakati mwingine iwe ni hoja za msingi au hoja zisizo za msingi, mwanadamu haangalii sana alikotoka, anatazama alipo au anakotaka kwenda.
Vipindi anavyotaka mheshimiwa viwepo katika redio zetu vinaweza kuwepo. Wakubwa wenzake wapo tayari kwa vuguvugu la majibizano ya hoja kali na nzito? Kuna wasomi hawana ajira na wanaweza kujiajiri katika kupiga simu redioni kukosoa mambo kila saa mbili asubuhi.
Kuna wenye vifua vya kuhimili haya na maisha yakaendelea. Wengine hawana vifua. Rahisi tu ghafla kutoonekana mtaani. Rahisi tu kuonekana mpinzani. Wakati mwingine hata wanaojaribu kujenga sana wakiwa ndani ya mfumo wanaonekana ni maadui ndani ya mfumo.
Tulipofika hapo tukaamua kuishi maisha rahisi. Na labda kwa sababu tumeishi sana katika misingi ya sera za ujamaa basi ni rahisi Mtanzania kupandishiwa bei ya umeme akamezea bila ya kuuliza chanzo. Wale majirani zetu kule upande wa pili wa Namanga wamekulia katika ubepari. Ukipandisha shilingi moja tu katika bei ya mkate asubuhi nchi nzima itapiga simu redioni.
Kutokana na haya, Watanzania tukaamua kuishi maisha rahisi. Hisia zikajengeka katika kusikiliza kinachofanywa na akina Aziz Ki uwanjani. Kila asubuhi tunafungulia huko kwa sababu hakuna kesi za akina DPP. Zile ambazo baadaye unaambiwa ‘DPP ameonyesha nia ya kutoendelea na kesi’. Huku kwenye michezo kuna raha. Kuanzia kwa waendeshaji hadi wasikilizaji.
Watu wanapumua na kujisikia kuwa huru zaidi katika eneo hilo. Wanaweza kujengeana hoja nzito lakini wakaishia kutabasamu tu bila ya hofu ya kupotea. Hii kitu ndio wasomi huwa wanasema ‘ to feel the relief’ sio. Kifua kinaweza kukubana kwa mambo mazito ya nchi, lakini ukaamua kupata nafuu katika ubishi wa nani zaidi kati ya Shomari Kapombe na Yao Yao.
Ukiachana na hilo, tatizo kubwa zaidi baada ya hapo ni kwamba kutokana na kutokuwa na mijadala mizito, kuna ‘ajira’ mpya ikazaliwa. Kuna watu wakajiajiri katika kazi ya uchawa. Viongozi wetu, matajiri wetu, mabosi wetu wanapenda wanachotaka kusikia.
Tumegoma kabisa kufanya kazi ngumu na kuruhusu tuhukumiwe kwa kazi zetu. Tumeamua tu kuna watu wapelekwe mbele wakapige zumari wawaambie wenzao ambacho mabosi wanataka kusikia. Bahati nzuri ni kazi yenye ujira mzuri.
Kuna watu wa aina mbili katika kazi hii. Kuna vijana wa mtaani wamejiajiri katika kazi hii. Lakini kuna viongozi wa ‘size’ ya kati pia wamejiajiri kupigia debe wakubwa zao zaidi. Hawa wa kwanza ni kwa ajili ya kujipatia kipato, hawa wa pili ni kwa ajili ya kulinda nafasi zao.
Matokeo yake wenye elimu zao ambao hawapo katika makundi haya mawili wanajikuta wanasota. Unaweza kukaa na Uprofesa wako ukisubiri kwenda kutoa ‘lecture’ Tokyo Japan walau upate pesa ya kumalizia kununua kiwanja Dodoma, halafu ghafla Mercedes Benz ya Chawa ikakupita kwa mbwembwe, ukiwa umejibana zako katika bajaji yako.
Kama una roho nyepesi unaweza kuuweka uprofesa wako pembeni ukaamua kujiajiri katika kazi hii mpya. Na mambo yakikunyookea ni rahisi tu kuukubali ukweli kwamba umeokotwa jalalani. Ndio maana katika hili kundi la chawa pia kuna wasomi wengi.
Wakati mwingine wakizungumza mambo unajiuliza “Huyu ndiye ana PhD ya Havard”?. Unahamisha taarifa ya habari unaamua kuangalia pambano la marudiano kati ya Simba na Al Masry lilikopigwa nchini Misri. Nchi ambayo maji yake yameanzia kwetu pale Mwanza na Kagera, lakini uchumi wao unatisha.
Nisisahau kukwambia kwamba baadaye tulikubaliana na Mheshimiwa kwamba tumechagua kuishi maisha mepesi. Maisha yaliyojenga sana vipindi vyetu vya michezo vya asubuhi mpaka jioni kuwa na topiki za moto kuliko topiki za uchumi. Kupanga ni kuchagua.
Maisha mepesi mengine ndio ambayo yamekwenda kutengeneza chawa. Wanaongea kwa niaba yetu lakini wanaongea kwa kupamba zaidi. Hauwezi kubishana na chawa kwa sababu hahitaji hoja zako na hayupo mbele yako kwa ajili ya hoja. Yupo kwa ajili ya kupamba tu. Hakuna kingine.
Sijui tutaupiga huu mwendo mpaka lini, lakini kwa sasa ndio hali halisi. Tusidanganyane. Mabosi wetu wameuchagua huu mwendo. Sijui kama wanajifanyia tathimini katika viwango vya kukubalika huku ‘site’ au tumeamua tu tupige mwendo wa chawa.
Hofu tu ni kwamba watoto wetu wa sasa wasije kuwaona chawa kuwa mashujaa wa maisha. Vizazi vya mwaka 2000 vitaipoteza nchi vibaya. Kwani na wao hawatataka njia fupi ya maisha? Nani anaitaka njia ndefu?