
Kwa mujibu wa Ibara ya 3. (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977; “Jamhuri ya Muungano (wa Tanzania) ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa uliorejeshwa tangu mwaka 1992”
Ili kutekeleza Ibara hiyo, sheria namba 5 ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 ilitungwa kulinda haki za kisiasa na kutoa haki sawa ya kufanya shughuli za kisiasa kwa vyama vyote.
Katika Ibara ya 12. (1) na 13. (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, usawa mbele ya macho ya sheria unasisitizwa, huku Ibara ya 13. (4) ikizipiga marufuku mamlaka yoyote nchini kutenda kwa ubaguzi, iwe kwa kuangalia utaifa, kabila, dini, jinsia, rangi, itikadi za kisiasa au hali ya kiuchumi.
Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 nayo inatoa uhuru wa maoni kwa wote.
Nimenukuu Ibara hizo za Katiba ya Jamhuri ya Muungao wa Tanzania ya mwaka 1977 na kutaja sheria namba 5 ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 kupata mtiririko mzuri wa kujenga hoja yangu ya leo kuhusu vitendo vya baadhi ya viongozi na watendaji wa Jeshi la Polisi katika masuala na matukio ya kisiasa.
Matukio ya kuzuia shughuli za kisiasa na hata kuwatia mbaroni viongozi wa vyama shindani (wengi wanaita vyama vya upinzani) dhidi ya chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM) vinadhihirisha kuwa baadhi ya viongozi na watendaji ndani ya Jeshi la Polisi hawaishi takwa la Katiba na sheria ya mfumo wa vyama vingi unaotoa fursa na haki sawa kwa vyama vyote vyenye usajili wa kudumu kufanya shughuli za kisiasa.
Kuna mifano ya matukio kadhaa tangu mwaka 1992, mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa hadi sasa yanayodhihirisha kuwa baadhi ya viongozi na watendaji ndani ya Jeshi la Polisi wanaendelea kuishi kwenye fikra za mfumo wa chama kimoja cha siasa kwa kudhani CCM ina haki kuliko vyama vingine.
Marehemu Agustino Mrema na makada wenzake wa NCCR-Mageuzi enzi hizo walikuwa ni waathirika wa mwanzoni wa utendaji wa baadhi ya viongozi wa Jeshi la Polisi usiojali haki ya kisiasa ya vyama shindani dhidi ya CCM.
Wenye kumbukumbu wanaelewa jinsi misafara na mikutano ya kisiasa ya Mrema ilivyopigwa mabomu ya machozi kuwazuia wafuasi wake kumbeba kiongozi huyo kabla au baada ya mikutano ya kampeni.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndiye aliyemaliza kadhia hiyo baada ya kuhoji ni kosa gani la kisheria wanalotenda Mrema na wafuasi wake wanaombeba.
Miaka 33 tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe, bado tunashuhudia mamlaka za Serikali zikitumia nguvu ya dola kudhibiti shughuli halali za kisiasa za vyama shindani kinyume cha katiba na sheria.
Zuio haramu la shughuli na mikutano ya kisiasa iliyodumu kwa takriban miaka saba kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2023 ni mfano hai jinsi dola inavyotumika siyo tu kudhibiti shughuli halali za vyama shindani dhidi ya CCM, bali hoja na mawazo mbadala kinyume cha sheria na katiba.
Matukio ya viongozi wa Chadema, likiwemo lile la aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe na wenzake kadhaa kukamatwa jijini Mbeya walipokwenda kuhudhuria kongamano la maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani lililoandaliwa na Baraza la Vijana wa chama hicho (Bavicha) ni mfano mwingine wa karibuni wa matumizi ya dola kudhibiti hoja na mawazo mbadala.
Nguvu kubwa iliyotumiwa na Jeshi la Polisi dhidi ya wananchi na wafuasi wa Chadema kuwazuia kuhudhuria Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza kesi dhidi ya Mwenyekiti wao Tundu Lissu, pia yanaonyesha jinsi nguvu ya dola inavyotumika kuzuia sauti zenye hoja kinzani.
Ni vema viongozi na watendaji katika mamlaka za dola waheshimu na kulinda Katiba kwa kuachia shughuli za kisiasa zifanyike kwa uhuru, haki na usawa kwa vyama vyote vya siasa, huku hoja za kisiasa zikijibiwa kisiasa kwa hoja imara zaidi bila matumizi ya nguvu ya dola.
Tuzingatie wosia wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuwa “Hoja haipigwi rungu; bali hujibiwa kwa hoja bora na imara zaidi.”
Peter Saramba ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa, anapatikana kwa 0766434354.