UCHAMBUZI WA SARAMBA: Kabla ya amani, tuombee haki, utu, usawa na upendo

“Ombeni, nanyi mtapewa, tafuteni, nanyi mtaona, bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea, naye atafutaye huona, naye abishaye atafunguliwa,”

Kwa waumini wa dini ya Kikristo, hiyo ni ahadi inayopatikana katika Biblia Takatifu kupitia Injili ya Mathayo 7:7-8.

Katika imani ya dini ya Kiislam, ahadi ya kuomba na kupata iko katika Sura Al-Baqarah (2:186) ya Qurani Takatifu kinachosisitiza kuwa Mungu (Allah) ni karibu na watu na anajibu dua za wanaomwomba kwa dhati na imani. Sura hiyo inahimiza kumwomba Mungu kwa uaminifu na kwa hakika atawajibu.

Nimeanza kwa kutumia vitabu Vitakatifu vya Biblia na Qurani kujenga hoja ninayolenga kuzungumzia; nalo ni wimbi la mikutano na mikusanyiko ya kidini ya kuombea viongozi na amani kwa Taifa.

Mara kadhaa tumeshuhudia viongozi wa dini tofauti nchini wakiandaa ama mikesha au mikutano maalum ya kuombea amani na inatarajiwa mikutano na mikusanyiko hii ya kuombea viongozi na amani kwa Taifa itaongezeka kadri tunavyokaribia uchaguzi baadaye mkuu mwaka huu.

Hata katika awamu za uongozi zilizopita, mikutano na mikusanyiko ya aina hii imekuwepo; na binafsi, sina nongwa nayo. Ni jambo jema kuwaombea viongozi wetu na amani kwa Taifa letu.

Hata hivyo, ni rai yangu kwamba kabla ya kuombea amani, ni vema kwanza tuombee haki, usawa, utu na upendo kwa wote ndani ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Natamani kuwaona viongozi wetu wa kiroho wanapofikiria kuombea Taifa basi, wafikirie kuombea haki, usawa, utu na upendo kwa wote bila kujali tofauti wayo yote miongoni mwa wanajamii.

Nasema tuombee haki, usawa, utu na upendo kwa sababu mambo hayo manne ndiyo msingi wa amani.

Kwa nini? Ni kwa sababu amani ni tunda la haki, usawa, utu na upendo katika jamii na Taifa.

Jamii ya watu wanaoishi kwa kutendeana haki, kutendeana kwa usawa, kujali utu wa kila mmoja na upendo kwa wote hukaa kwa amani na utulivu ka sababu hakuna anayeonea wala kuonewa.

Haki, usawa, utu na upendo utazalisha viongozi wanaotambua kwamba nafasi zao ni za utumishi wa umma na siyo fursa ya kujilimbikizia mali.

Jamii na Taifa lenye watu wanaoshi kwa kuzingatia haki, usawa, utu na upendo hupata viongozi wasiotumia nafasi na ofisi za umma kufuja mali, fedha na rasilimali za umma.

Vituo vyetu vya Polisi, Mahakama na ofisi za umma hazitageuka kuwa magulio ya kuuza na kununua haki za raia ambapo mwenye nacho ndio hupata na wasio nacho kupoteza hata kile kidogo walichonacho.

Tukiombea na kupata Taifa lenye haki, usawa, utu na upendo, kamwe Mahakimu na Majaji wetu hawatachelewesha mashauri na haki za watu mahakamani kwa kuahirisha kesi bila sababu za msingi.

Viongozi wetu wa dini na waumini wao wakijikita kuombea haki, usawa, utu na upendo ni hakika Taifa letu halitapata viongozi wanaoweka asilimia 10 katika mikataba ya miradi ya maendeleo wanayosaini.

Tutakapoanza kuombea na kupata jamii yenye haki, usawa, utu a upendo, ndipo Taifa litapiga hatua siyo tu kwenye maendeleo ya vitu, bali pia maendeleo na ustawi wa watu pia.

Haki, usawa, utu na umoja utatupatia viongozi, wanachama, wafuasi na makada wa vyama vya siasa wasiohasimiana kwa tofauti ya itikadi zao, bali watavitumia vyama vyao kama majukwaa ya kunadi, kuuza sera ili hatimaye kuushawishi umma kuwapa dhamana ya kuongoza dola.

Tunapokaribia uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ni vema viongozi wetu wa dini waombee haki, usawa, utu na upendo kuepusha kampeni za kisiasa za kuhasimiana, kuhujumiana na hata kutendeana uovu.

Kwa maoni yangu, hata ile kampeni ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya “No reforms, no election” itapata jibu kwa sababu uwanja Taifa letu litashuhudia uchaguzi unaendeshwa katika misingi ya haki, usawa, utu na upendo kwa wote.

Nawasihi viongozi wetu wa kiroho kujikita kuombea haki, usawa, utu na upendo ndipo tutapata Taifa leenye amani.

Bila haki, bila usawa, utu na upendo kwa wote, ni ndoto ya kupata jamii na Taifa lenye amani.

Tukifanya ioyo yetu kuwa migumu kwa kuendelea kuwaombea viongozi na amani pekee, ni hakika jamii na Taifa letu litakuwa na utulivu lakini isiyo na amani kwa sababu amani ni tunda la haki.

Peter Saramba ni Mwandishi wa habari mwandamizi, anapatikana kupitia [email protected] au 0766434354.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *