
Naelekea zangu Kisarawe, naiacha Barabara ya Nyerere eneo la Pugu, njiapanda ya kuelekea Chanika.
Mbele kidogo kabla hujafika msitu wa hifadhi wa Kazimzumbwi, nasoma bango kubwa lililopo kando ya barabara, likiwa na maandishi makubwa yasomekayo: Welcome to Coast region, yakimaanisha Karibu Mkoa wa Pwani.
Kama haitoshi, hata mitandaoni unapofungua tovuti rasmi ya mkoa huo unakutana na maneno Coast Region.
Najisaili moyoni, Tanzania ya leo (acha ile ya zamani) ina mkoa unaoitwa Coast?
Najaribu kupekua nyaraka za Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) sioni jina hili, bali kilichopo ni Mkoa wa Pwani chini ya Abubakar Kunenge, huku ukiwa unajumuisha wilaya za Kibaha, Bagamoyo, Chalinze, Kisarawe, Mafia, Mkuranga, Kibiti na Rufiji.
Hata ramani hazionyeshi jina Coast ambalo hata hivyo nikiri kuwa liliwahi kutumika zamani na sijui kama bado linaendelea kutumika hadi sasa.
Nilichobaini ni wahusika kulazimisha tafsiri hata mahala siko. Ni kweli neno pwani linatafsirika na kuwa coast katika Kiingereza.
Lakini tunapomaanisha mkoa, tafsiri hiyo ina walakini; najiuliza hivi tuna mkoa uitwao Coast katika Tanzania ya sasa?
Tukitaka iwe hivyo kwa kutafsiri majina ya mikoa, tutakuwa wachekeshaji. Nitoe mifano kadhaa.
Dar es Salaam ni jina linalotokana na lugha ya Kiarabu likimaanisha Nyumba ya Amani au bandari salama.
Hivi tukitaka kuuita mkoa huo kwa kutafsiri Kiingereza, itakuwa busara kuuandika kama House of Peace Region?
Au Mkoa wa Kilimanjaro ambao simulizi za kimapokeo zinadai kuwa asili yake ni maneno ya wenyeji kilima kyaro, yaani kilima kirefu, je, nao tuuandike High Mountain Region? Hivi ni vichekesho!Nitoe wito kwa walioweka bango hilo kurekebisha ili lisomeke: Welcome to Pwani region na siyo Coast region.
Tanzania hakuna mkoa wa Coast, na wala hakukuwa na sababu wala busara ya kutafsiri jina Pwani kwenda Coast.
Hata hivyo, kama neno Coast ndilo jina halisi la eneo hili (na hapa nitaomba ufafanuzi wa Serikali) linalojumuisha wilaya hizo nilizozitaja, kwa upande mwingine hakuna haja ya kutafsiri na kuitwa Pwani.
Libaki neno Coast kama lilivyo, vinginevyo tukilazimisha kulipeleka na kuwa Pwani, basi busara sasa itatutuma tufanye tafsiri ya majina mbalimbali.
Timu za mpira wa miguu kama vile Young Africans, Coastal Union, Singida Black Stars, nazo zitalazimika kuwa na tafsiri ya majina ya Kiswahili.
Unaonaje tukiita Young Africans kwa jina la Waafrika Vijana kwa kuwa tu tumetafsiri maneno ya Kiingereza au Singida Black Stars ikawa Nyota Weusi wa Singida?
Lakini kwa nini tumefikia hapa na kuna haja gani ya kuandika kwa kimombo hata kwa vitu visivyo na ulazima?
Hivi isingetosha tu kuandika Karibu Mkoa wa Pwani? Lini Watanzania tutaachana na kasumba ya kuhusudu Kiingereza?
Uzoefu wangu unaonyesha hata katika mazingira ya watumiaji watupu wa Kiswahili, tunang’ang’ana na Kiingereza.
Usishangae hospitalini huko vijijini kukuta majengo na ofisi yameandikwa kwa kimombo, kama vile watumiaji ni wageni kutoka nje.
Nadhani sisi tunaweza kuwa watu wa pekee duniani ambapo mkusanyiko wa wazungumzaji wa Kiswahili watupu na unaohusu masuala ya Waswahili, wahusika watalazimisha matumizi ya kimombo. Huu ni utumwa ambao sifichi hisia zangu kwa kusema kuwa umefurutu ada.
Mapenzi kwa Kiingereza yametutawala wengi. Nenda maeneo yote ya Waswahili ambayo huwezi kumkuta mgeni asiyejua Kiswahili, halafu chunguza majina ya mitaa yetu.
Utakachokutana nacho ni Mbonde Street, Bonge Street na mifano kama hiyo. Maduka na magenge hayanogi bila ya kuyaandika Muha shop au Kitopeni shop.
Hata Mama Sikudhani wa Buza kwa Mpalange kule kwetu wilayani Temeke, akifungua fremu ya ususi, ataandika: Shostito Salon!
Nieleweke, mimi si muumini wa kubeza lugha za kimataifa, hasa Kiingereza. Natambua nafasi na umuhimu wake, lakini tuzitumie katika mazingira yanayosadifu utumizi wake na siyo kuzilazimisha hata kwenye mazingira yasiyoswihi.
Msingi Mkuu wa lugha ni kurahisisha mawasiliano. Kwa nini tujikwaze kwa kutumia lugha ambayo walio wengi hawaimudu? Kiingereza sawa ila tukitumie kunakostahiki.
Abeid Poyo ni mhariri wa makala Mwananchi. 0754990083.