UCHAMBUZI WA MJEMA: Unampa asilimia ngapi mbunge, diwani wako?

Imebaki miezi michache kabla ya Bunge na mabaraza ya madiwani kuvunjwa ili sasa tuingie kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu 2025, na hiki ndicho kipindi muafaka cha kuwapima ili ikifika Oktoba kila mmoja avune alichokipanda.

Kwa taarifa tu, kwa wabunge na madiwani waliopo madarakani sasa hivi, wao tutawachagua na kuwarudisha kwa kupima utendaji wao na sio tena kwa kura za ahadi, tutatumia kuchagua sura mpya.

Bahati nzuri zaidi ya asilimia 95 ya wabunge na madiwani wanaomaliza muda wao wanatokana na CCM, kwa hiyo hawatakuwa na wa kumbebesha lawama endapo kuna ahadi na ilani ya CCM 2020-2025 hazikutekelezwa kwa ukamilifu.

Katika Bunge la 2015, Rais wa awamu ya tano, John Magufuli na makada wengine wa CCM, walikuwa wanaulaumu upinzani kwamba unawachelewesha kutokana na namna walivyokuwa wanahoji na kujenga hoja juu ya masuala mbalimbali.

Kuna usemi wa waswahili unasema; “mchawi mpe mwanao amlee,” kwa sababu kwa kufanya hivyo, kutamzuia kumuua mtoto, ataogopa akifanya hivyo atajulikana yeye ndiye aliyehusika na mauaji hayo na pengine hata kushitakiwa.

Ndivyo watanzania kupitia uchaguzi mkuu 2020 (uwe ulikuwa uchaguzi au uchafuzi kama wapinzani wanavyodai), wakaona isiwe tabu si mnasema upinzani ndio kiini cha matatizo yetu?, tunawapa wabunge na madiwani kama wote.

Nitangulie kuwaasa mapema watanzania, tukatae kugeuzwa karai la zege ambalo lina sifa moja tu, kwamba wakati wa ujenzi linaonekana lina thamani kubwa lakini ujenzi unapomalizika huhifadhiwa nyuma ya nyumba hadi ujenzi utokee tena.

Ninafahamu hiki ndio kipindi ambacho wabunge na madiwani, hata wale ambao kwa miaka mitano ama walikuwa hawapokei simu zetu au kubadili namba za simu, sasa watarudi na kuwa karibu sana na wananchi hata misibani tutawaona.

Majukumu ya Kikatiba ya Mbunge Ibara ya 63(1) ambayo inasema Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu ambacho kitakuwa na madaraka kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake.

Kwa hiyo, katika kutekeleza wajibu huo, mbunge anaweza kumuuliza waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya umma, kujadili na kupitisha bajeti, kujadili na kuidhinisha mpango wowote unaokusudiwa kitekelezwa hapa nchini.

Wajibu mwingine ni kushiriki kutunga sheria, kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inahitaji kuridhiwa, kama ulivyokuwa mkataba wa DP World na Tanzania.

Kwa hiyo wajibu wa mbunge sio kujenga barabara, shule, huduma za maji au afya au kutoa fedha mfukoni mwake kutekeleza miradi ya maendeleo, hapana nchini.

Huo ni wajibu wa Serikali na kazi ya mbunge ni hizo zinazotajwa na ibara ya 63 ya Katiba.

Kwa kutotambua majukumu yao, ndio maana wananchi wanaona kila kitu katika maisha yao kinapaswa kufanywa na mbunge au unaona mbunge anampigia waziri magoti kuomba barabara au maji badala ya kuisimamia Serikali.

Ni kutokana na uelewa huo mdogo, sishangai kukuta mbunge anatumia muda wake wa dakika 5 au 10 kuchangia bajeti, kumsifia Rais kuwa ameleta hiki au kile wakati huo ni wajibu wa kikatiba wa Serikali na wala si fadhila ya Rais au waziri.

Wala si sahihi wakati wa kampeni mbunge kuahidi ataleta barabara, au atajenga shule au ataleta visima vya maji, hizo ni hadaa za kisiasa na ndio inazaa dhana kuwa mbunge anapaswa kuwa mtu mwenye fedha na mali za kugawa.

Kwa hiyo, kinacholeta maendeleo iwe ni kwenye Jimbo au kata au mtaa ama kijiji, si fedha binafsi za mwanasiasa, la hasha, bali ni fedha zinazotokana na kodi zetu na hata kama ni mikopo ya nje, bado ni kodi zetu kwa kuwa litalipwa na sisi.

Majukumu ya diwani hayatofautiani sana na ya mbunge, kinacholeta utofauti ni vyombo vya uwakilishi kwamba mbunge anakuwa mwakilishi wa wananchi bungeni na Diwani anakuwa mwakilishi wa wananchi kwenye halmashauri.

Kazi kubwa ni kusimamia matumizi ya fedha za Halmashauri, kuwa kiungo kati ya Halmashauri na ngazi za msingi za serikali za mitaa, kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya kata yake na kusimamia misingi yote ya utawala bora.

Kama nilivyotangulia kusema, tunapaswa kuanza kuwapima wawakilishi wetu hawa kama wametutendea haki na tunastahili kuwarudisha kupitia sanduku la kura, au walisimamia maslahi yao binafsi na ya chama kilichowadhamini.

Niseme kuna aina mbili za kuwachagua viongozi wa kisiasa kama hawa wabunge na madiwani, kwamba kwa waliopo kwenye uongozi tunawapigia kura kulingana na utekelezaji wa Ilani (perfomace voting) sio ahadi tena (promise voting).

Katika Uchaguzi Mkuu 2020, waliinadi ilani ya chama kilichowaingiza katika madaraka, sasa hatupaswi kuwapa kura kama kile walichotuahidi kupitia ilani hawajakitekeleza kwa kuwa huo ni mkataba baina ya mbunge au diwani na wananchi.

Wenye lugha yao ya kimombo, wanasema ilani ya uchaguzi nikinukuu; “A manifesto is a published declaration of the intentions, motives, or views of the issuer, be it an individual, group, political party or Government.”

Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi, Ilani ya Uchaguzi ni tamko lilochapwa linaloonyesha makusudio, malengo au mtazamo wa mtoaji (ilani), awe ni mtu binafsi, kundi, chama cha siasa au Serikali kwa muktaba wa makala hii ni ilani ya CCM.

Sasa kama mlinadi sera, wananchi wakawakubali na kuwapa dola, tunapaswa kuwapima kama kweli mlisimama katika kuwawakilisha wananchi bungeni au kwenye mabaraza ya madiwani, au mlitanguliza maslahi yenu mbele.

Wabunge ni kada ya watumishi wa umma wanaolipwa fedha nyingi kwa mwezi, kwa hiyo sisi mnaotuwakilisha, tulitarajia kuona michango yenye tija ya kuisimamia Serikali na sio kuligeuza bunge kuwa sehemu ya uchawa kwa viongozi.

Tungekuwa na Katiba ile ya Tume ya Jaji Warioba, ibara ya 129(1)(a) tungeweza kuwaondoa mapema wabunge tunaowaona wanaunga mkono sera ambazo zinaenda kinyume na maslahi ya wapiga kura au kinyume na maslahi ya Taifa.

Ukisoma ile (b), ilisema wananchi wangeweza kumwajibisha mbunge kwa kushindwa kuwasilisha au kutetea kwa dhati hoja zinazotokana na kero za wapiga kura wake na (c) kama ataacha kuishi au kuhamisha makazi yake kwa miezi sita.

Bahati mbaya sana, rasimu hii iliyokuwa imebeba maoni ya watanzania wengi ilipigwa chini, sasa mahali pekee tunapoweza kumwajibisha mbunge aliyekwenda kinyume na mambo hayo matatu, ni kupitia sanduku la kura.

Huu ni wakati mwafaka wa kuwapima wabunge wetu kama walitumia vizuri ibara ile ya 63 katika kuisimamia na kuishauri Serikali juu ya matendo mabaya yanayoendelea nchini ya kupotea kwa watu, kutekwa, kuteswa na kuuawa.

Lakini tuwapime wabunge wetu na madiwani, wameshughulikia vipi hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinazoibua madudu kila mwaka zikisomwa, lakini vipi kuhusu kubana matumizi makubwa ya Serikali.

Mwaka 2022, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alitoa wimbo mzuri sana wa kubana matumizi ya serikali ikiwamo ununuzi wa magari na mafuta, wabunge wetu wamesimamiaje kuhakikisha kauli hii inakuwa na uhalisia?

Wabunge wetu ambao nimetangulia kusema wanalipwa mapesa mengi kweli kweli, wameisimamia vipi serikali kuhakikisha miswada ya sheria inayopelekwa na Serikali bungeni inakuwa na maslahi kwa wananchi na haiwi ni kandamizi.

Tunapaswa kuwahoji wabunge wetu wametumia vipi ibara hiyo ya 63 kuisimamia na kuishauri Serikali kuhusu mikopo ya kibiashara na ile yenye riba nafuu inayopandisha deni la taifa, inatumika vizuri na thamani ya fedha inaonekana?

Lakini pia tuwapime wabunge wetu, wameisimamia vipi serikali kuhakikisha Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya Haki Jinai, vinatekeleza majukumu yake kwa kuheshimu utawala wa sheria, haki za binadamu na utu wa mwanadamu.

Ninasema hivyo kwa sababu licha ya Rais Samia ambaye ni Amiri Jeshi mkuu kulisema sana Jeshi la Polisi, bado tunaona watu wanakamatwa mithili ya utekaji, kufichwa kwenye vituo vya Polisi na wengine kukaa muda mrefu mahabusu.

Mimi nimechokoza tu mada, unaweza kuongeza orodha ya mambo ambayo tunapaswa kuwahoji na kuwapima wabunge na madiwani wetu kabla ya kufika kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na Madiwani Oktoba 2025.

0656600900