UCHAMBUZI WA MJEMA: Tanzania inahitaji upinzani imara leo kuliko jana, juzi

Novemba 2017, Rais mtaafu wa Tanzania (2005-2015), Jakaya Kikwete, alisema vyama vya siasa vilivyo madarakani barani Afrika, havipaswi kuvichukulia vyama vya upinzani kama maadui, bali wabia katika kuendeleza misingi ya kidemokrasia.

Ukiacha tafsiri hiyo ya Kikwete, binafsi naviona vyama vya upinzani kama taa inayosaidia kuimulikia Serikali iliyopo madarakani kuna njia inayopita au kioo cha Serikali iliyo madarakani, ambacho inaweza kukitumia kujitazama kama ipo sawa.

Mathalani, kuibuliwa kwa kashfa za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), ufisadi katika mfuko wa kuwezesha uagizaji bidhaa nje (CIS), kashfa ya ununuzi wa Rada, kashfa ya Escrow na Richmond, yote ni kutokana na kuwa na upinzani imara bungeni.

Ukiacha kashfa hizo, lakini hata kusambaa na kujulikana kwa mkataba wa uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kati ya Tanzania na kampuni ya DP World ya Dubai kulitokana na uzalendo wa Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Kenani.

Lakini leo hii ni kwa sababu ya upinzani, wananchi wanaliona Bunge la 10 na 11 kama mabunge moto kwelikweli katika kuisimamia na kuishauri Serikali hadi tukashuhudia mawaziri na watendaji kadhaa wakijiuzulu au kuwajibishwa.

Ni kwa msingi huo, ndio maana nimetangulia kusema Tanzania tunahitaji upinzani imara leo kuliko jana na juzi, na si jambo la busara na halitapendeza endapo atatokea Mtanzania atafurahia kifo cha mojawapo ya chama makini cha upinzani.

Akiwa Johannesburg, Afrika Kusini akijadili mada iliyowasilishwa na Barney Pityana ambaye ni makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Afrika Kusini kuhusu utawala bora, Kikwete alitaka wanasiasa wa upinzani wasichukuliwe kama maadui na serikali.

Sasa ukiangalia yanayotokea nchini Uganda kwa kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, Kizza Besigye aliyegombea urais mara kadhaa kupitia chama cha Forus for Democratic Change (FDC), unaweza kutafsiri kuwa upinzani ni dhambi.

Kwake kulala mahabusu, kuzuiwa akiwa nyumbani (house arrest), kushambuliwa na maofisa wa vyombo vya dola kama polisi, ni jambo la kawaida kwa Besigye kama inavyomtokea Bob Wine wa chama cha National Unit Platform (NUP).

Sasa hivi, Besigye yuko mahabusu kwa mashitaka ya uhaini tena akitekwa nyara katika Jiji la Nairobi nchini Kenya na kusafirishwa hadi Kampala, Uganda.

Ipo mifano mingi ya viongozi wa upinzani wanaopitia shuruba za aina hii, Birtukan Midekssa wa Ethiopia ambaye ni kiongozi wa upinzani mwanamke na hata hapa Tanzania wapo viongozi na wafuasi wa upinzani wanapitia kipindi kigumu.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe alishakamatwa mara kadhaa, mrithi wake wa sasa Tundu Lissu na viongozi wengine na wafuasi wa chama hicho wamepitia misukosuko.

Wapo viongozi na wanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini waliofunguliwa kesi za kisiasa na kukaa mahabusu zaidi ya mwaka mmoja, na wapo waliotekwa, kuuawa na wengine kupotezwa na hawajulikani walipo.

Hivi ni kweli upinzani hauna faida kiasi cha kuonekana ni uadui au ni dhambi kuwa mpinzani? Hapana, Jawarlal Nehru (1889-1964) wa India, alisema demokrasia ndio mfumo bora wa Serikali unawapa nafasi raia kuwawajibisha viongozi.

Kama ndivyo, wananchi huvitumia vyama vya upinzani kama taasisi za umma, kuwawajibisha viongozi wa serikali na hili tumeliona katika kashfa nilizozitolea mfano, na ndio maana nasema tunahitaji upinzani imara leo kuliko jana na juzi.

Kwa hiyo, akitokea yeyote yule akafurahia kifo cha Chadema au ACT Wazalendo ama vyama vingine makini vya siasa, huyo atakuwa ni mtu asiyefahamu faida za kuwa na upinzani ambao siku zote huwa ni kioo kwa Serikali iliyopo madarakani.

Nimesikitika sana na hali ambayo ninaiona ndani ya Chadema baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa viongozi wao wa kitaifa, baadhi ya viongozi na wanachama ambao hawakumuunga mkono Lissu, ni kama wanatamani chama hicho kimfie.

Ukisoma maandishi yao katika mitandao ya kijamii unashangaa kiongozi kabisa wa Chadema anakiombea mabaya chama chake kwa sababu tu Freeman Mbowe waliyemtaka hakushinda, huu ni usaliti wa hali ya juu na usiokubalika duniani.

Bahati mbaya sana, wapo ambao walijiaminisha Mbowe hawezi kushindwa na hata baada ya kushindwa hawataki kukubali kuwa ushindi wa Lissu na John Heche kama makamu wake ni wa chama na maisha yanapaswa kuendelea.

Ukiwauliza ni kwa nini wanatamani Lissu ashindwe kukitoa chama hapo alipokiacha Mbowe, watakuambia Lissu alimtukana sana Mbowe na kumdhalilisha, lakini matusi ambayo ni kosa la jinai hayasemwi waziwazi.

Lakini wanachoshindwa kufahamu ni kuwa matendo na kauli zao zinapunguza uhai wa chama chao na kama nilivyosema Tanzania inahitaji upinzani imara ili kuifanya Serikali inayoongozwa na CCM isibweteke au kujisahau ama kujimwambafai.

Vilevile, ambavyo sitamani Chadema kipoteze mwelekeo, pia sitamani chama makini kama ACT-Wazalendo, Chama cha Wananchi (CUF) na vingine vichache, vipoteze mwelekeo kwani CCM kilichopo madarakani kinaweza kujisahau.

Sote tunafahamu namna Watanzania wanavyolitizama Bunge la sasa ambalo lina wingi wa wabunge kutoka CCM (asilimia zaidi ya 95), lakini ukilifanyia tathimini ni kuwa limepoteza ladha kwa sababu hakuna wabunge machachari wa upinzani.

Ninatamani kuona Bunge linalofanana na wakati akina Dk Wilbroad Slaa, Freeman Mbowe, Tundu Lissu, Zitto Kabwe, Godbless Lema, John Heche, Halima Mdee, Esther Bulaya, David Kafulila, Joseph Mbilinyi na James Mbatia wako bungeni.

Vyama vya upinzani na si hapa Tanzania tu, duniani kote vinafanya kazi kubwa ya kuwa jicho la umma (checks and balance), vinawasilisha maoni mbadala, hupendekeza sera mbadala na kuhamasisha umma kushiriki masuala ya siasa.

Lakini vyama vya upinzani, pia, huwa wajibu wa kutetea makundi yasiyo na sauti (minority), hukosoa utendaji wa Serikali, husaidia kuibua mijadala ya wananchi lakini wajibu mwingine ni kujiandaa kushika dola au kuingia madarakani.

Pamoja na faida zote hizo, baadhi ya watawala huwaona wapinzani kama maadui badala ya wabia wa kustawisha demokrasia na wangetamani vyama vya upinzani visiwepo kabisa, licha ya Katiba zao kutambua uwepo wa vyama vingi vya siasa.

Ndio maana nimeamua kurejea kauli ya Kikwete aliyoitoa katika Jukwaa la Uongozi barani Afrika mwaka 2017 akitaka wanasiasa wa upinzani wasichukuliwe na Serikali iliyopo madarakani kama ni maadui, bali wabia wa kustawisha demokrasia.

Kikwete alijitahidi sana kutekeleza dhana hiyo, lakini kuanzia mwaka 2016, mwelekeo wa kisiasa wa Tanzania umebadilika sana ambapo vyama vya upinzani na viongozi wake wanaonekana ni maadui badala ya kuwa Jicho la Serikali.

Yaani nchini ni kama CCM imejimilikisha nchi, haitaki tena uchaguzi huru na wa haki kwani kwa tuliyoyashuhudia uchaguzi wa serikali za mitaa 2019, uchaguzi mkuu 2020 na uchaguzi serikali za mitaa 2024, ushindi wa upinzani ni ndoto.

Lakini kama tungeibeba dhana hii ya Kikwete na wahafidhina ndani ya CCM wakawekwa pembeni, nchi hii ingekuwa na upinzani wenye nafasi ya kuishauri Serikali na kuikosoa inapokengeuka, kupitia Bunge au mabaraza ya madiwani.

Tukiruhusu upinzani ufe, tutalia kilio cha kusaga meno. Tusiruhusu hili kwani polepole tutakaribisha udikteta.

0656600900

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *