
Inawezekana Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT-Wazalendo na vyama vichache makini, vina hoja ya msingi ya kutaka mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi, lakini inawezekana pia baadhi ya njia wanazotumia kushinikiza si sahihi.
Februari 23, 2025 ACT-Wazalendo ilifanya Mkutano wa Halmashauri Kuu na kuazimia kipaumbele chao kwa sasa ni kupigania maboresho ya mfumo wa uchaguzi utakaohakikisha haki na kuheshimiwa kwa maamuzi ya wananchi.
Moja kati ya kupigania kipaumbele hicho ni kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na kwamba suala kushiriki ama kutoshiriki uchaguzi mkuu 2025 kabla ya marekebisho litaamuliwa na kamati ya uongozi ya kitaifa katika wakati muafaka utakapofika.
Lakini Chadema ndiyo iliyotangulia kuweka msimamo kwani Desemba 10, 2024, kupitia mwenyekiti wao Freeman Mbowe ilikuja na msimamo wa “No Reforms No Election,” ikimaanisha bila mabadiliko basi uchaguzi hautakuwepo.
Msimamo huo ulipata baraka za Baraza Kuu la Chadema na mkutano mkuu uliofanyika Februari 21, 2025 na msimamo huo unasimamiwa kikamilifu na mwenyekiti wa sasa wa Chadema, Tundu Lissu na kamati kuu yake nzima.
Takribani siku mbili zilizopita, NCCR-Mageuzi wao, kupitia kwa makamu mwenyekiti wao, Joseph Selasini, wao hawana mpango wa kususia uchaguzi mkuu kwa kigezo cha marekebisho ya Katiba na kwamba watashiriki uchaguzi mkuu.
Huo ni mtizamo wa vyama hivyo vitatu, lakini Chama cha Mapinduzi (CCM), wao wanasema kauli ya “No Reforms no Election” haina nafasi kwa sasa na kutaka CCM kutumia nafasi ya mazungumzo badala ya kushikilia misimamo isiyotekelezeka.
Msimamo wa CCM nina hakika unaungwa mkono na vyama marafiki ambavyo sote tunavifahamu kutokana na misimamo ya viongozi wake ingawa sina hakika sana kuhusu idadi ya wanachama na wafuasi walionao au wanaowaunga mkono.
Kwa Mtanzania yeyote mpenda haki aliyeshuhudia yaliyotokea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa 2019 na 2024 na uchaguzi mkuu 2020, anavielewa vyama hivyo, vinaposema enough is enough (imetosha) na vinahitaji mabadiliko ya kimfumo.
Lakini Mtanzania huyo huyo mpenda haki, hatukubaliana na njia ya Chadema na ACT-Wazalendo inayotumia ya kuhamisha watu wasijiandikishe kupiga kura kwa sababu mathalani, mifumo ikabadilika kabla ya uchaguzi wa Oktoba vinafanyaje?
Maana yake vitabaki na wapigakura wale tu wanaowaunga mkono na ambao wamejiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura, ila wale watawapoteza wale ambao ndio wametimiza miaka 18 au walihitaji kuboresha taarifa zao.
Tuna kama siku 224 kufikia Oktoba 26, 2025 kama Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) itapanga tufanye uchaguzi Jumapili ya mwisho wa Oktoba.
Ukisoma Ibara ya 5(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inasema kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka 18 anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi unaofanyika Tanzania ukiwamo huo wa Oktoba.
Ibara hiyo ndio ambayo imekopwa na sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2024 katika kifungu cha 9(1) kiachosema raia wa Tanzania mwenye umri huo atastahili kuandikishwa kuwa mpiga kura hapa nchini.
Lakini ukisoma ibara ndogo ya (2)(a) hadi (d) imeweka masharti yanayoweza kuzuia raia asitumie haki ya kupiga kura kuwa ni pamoja na kuwa na uraia wa nchi nyingine, kuwa mgonjwa wa akili na kutiwa hatiani kwa makosa fulani ya jinai.
Halikadhalika ibara hiyo imeweka sharti kama atakosa au kushindwa kuthibitisha au kutoa kitambulisho cha umri, uraia au uandikishwaji kama mpiga kura. Kwa maneno mengine mtu atazuiwa kupiga kura kwa sababu hizo tu.
Pengine ni kutokana na msimamo huo wa katiba ndio maana chama tawala (CCM), kupitia kwa makamu mwenyekiti (Tanzania Bara), Steven Wassira na Katibu wa Itikadi, Mafunzo na Uenezi, Amos Makala wanasema uchaguzi uko pale pale.
Kama nilimsikia Wassira vizuri, alienda mbali na kusema hakuna mabadiliko (reforms) itakayofanyika kwa sababu hayo ni mambo ya kisheria na Bunge la Februari 14, 2025 limemalizika na kubaki na kikao kimoja tu mahsusi kwa bajeti.
Katika siasa, kauli kama ya Wassira na Makala haiwezi kuwa Alpha na Omega (mwanzo na mwisho), kwa sababu lolote linaweza kutokea kabla ya uchaguzi mkuu, kama nguvu ya umma itaamua vinginevyo kwa sababu ndio wenye nchi.
Nilibahatika kumsikiliza Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Tundu Lissu alipokuwa akisisitiza msimamo wao wa “No reforms no Election,” kwamba bila mabadiliko basi hakuna uchaguzi akihoji wananchi wajiandikishe kupiga kura ili iweje.
Nikimnukuu, “wakikuambia kajiandikishe kupiga kura waulize ili iweje? Kama kujiandikisha ni kuruhusu kura za wizi, kura feki kwa mamilioni, tukajiandikishe kupiga kura ili iweje. Wakituambia tukapige kura tuwaulize ili iweje.”
Huo ni msimamo wa Chadema, lakini tumesikia taarifa kutoka Zanzibar kuwa Machi 11, 2025 wanachama watatu wa ACT-Wazalendo walikamatwa wakizuia wananchi wasijiandikishe katika daftari la wapigakura mkowa wa Kusini Unguja.
Nafikiri hili ni kosa kubwa la kiufundi kama nilivyotangulia kusema kwa sababu licha ya msimamo mkali wa CCM na Serikali yake kuwa uchaguzi mkuu uko pale pale, hii haizuii uwepo wa maridhiano kama Taifa kabla ya Oktoba 2025.
Hebu tuchukulie mfano japo ni ngumu kama Ngamia kupita tundu la sindano, kwamba nguvu ya umma (sio Chadema wala ACT-Wazalendo), itaamua inataka mabadiliko kabla ya 2025, na yakafanyika, hivyo vyama vitapata wapi wapiga kura?
Kwa sababu watakuwa wamezuia kundi kubwa tena la vijana (Gen Z) ambao wametimiza umri wa kujiandikisha kupiga kura au kwa sababu ya kuwa vyuoni hawakupata nafasi ya kujiandikisha na sasa wanataka kufanya hivyo.
Lakini kitambulisho cha mpiga kura kina faida nyingine za ziada ukiacha kupiga kura, kwa sababu baadhi yetu ndio tunakitumia kudhamini ndugu zetu mahakamani na polisi, kufungua akaunti benki au kujitambulisha tu wewe ni nani.
Chadema na vyama vingine ambavyo vinaona hakuna haja ya kushiriki uchaguzi mkuu kwa mifumo ya kisheria iliyopo, wasilazimishe watu wasijiandikishe, badala yake wawahamasishe wajiandikishe kwani huko mbeleni watawahitaji.
Kujiandikisha ni jambo moja na kupiga kura ni jambo lingine, kwa sababu mtu anaweza ajiandikishe na kwa utashi wake akaamua asipige kura na hiyo ni haki yake ya kidemokrasia kwa mujibu wa Katiba ibara ya 5(1) ya Katiba yetu.
Ukifuatilia takwimu zilizotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Oktoba 30, 2020, utabaini Watanzania milioni 14.8 sawa na asilimia 49.8 hawakujitokeza kupiga kura kati ya Watanzania milioni 29.8 waliojiandikisha uchaguzi mkuu 2020.
Kwa hiyo, si sahihi kwa vyama hivyo kuhamasisha wanachama wao na Watanzania wasijiandikishe au kuboresha taarifa zao, badala yake ni vyema wakawahamasisha kujiandikisha ili kuwa na ‘Jeshi’ kubwa na kulitumia kupata uhalali wa kisiasa.
Hii maana yake nini, kama kiongozi anachaguliwa na idadi ndogo ya Watanzania kwa maana chini ya asilimia 50 maana yake kwa sheria za Tanzania atakuwa na uhalali wa kisheria, lakini kwa macho ya kidemokrasia, hawana uhalali kisiasa.
Katika sayansi ya siasa, uhalali (legitimacy) ni haki ya kukubalika kwa mamlaka, hii inaweza kukubalika kwa utawala na utawala ambao unakuwa na uhalali wa kisiasa, unakuwa na wakati mzuri wa kuongoza na mipango yake kukubalika na wananchi.
Rais wa 9 wa Marekani, William Henry Harrison aliwahi kusema:“The only legitimate right to govern is an express grant of power from the governed,” akimaanisha haki pekee halali ya kutawala lazima ipate mamlaka kwa wananchi.
Kwa hiyo si sahihi kwa chama chochote cha siasa kuhamasisha wapigakura kususia kujiandikisha, hilo ni kundi kubwa ambalo chama kitahitaji pale kitakapoamua kupinga maamuzi ya uchaguzi kuwa hayakuwa ya haki wala huru.
Hii maana yake ni kuwa idadi ya wapigakura mathalan ambao hawatajitokeza kupiga kura, inakuwa ni kielelezo cha utawala kutowekwa na wananchi kwa hiyo njia zozote halali za kuukataa utawala zitapata uungwaji mkono mkubwa.
Rai yangu kwa CCM irudi katika falsafa yake ya kuwa chama sikivu, kiviite Chadema na ACT-Wazalendo mezani kuzungumza, na si vibaya ikaiga utaratibu wa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete.
Vyama hivyo vya upinzani na vingine vyenye msimamo kama wa Chadema na ACT -Wazalendo, navyo visishupaze shingo la kukataa mazungumzo pale CCM watakapoona ipo haja ya kufanya hivyo kwa mustakabali wa amani ya nchi yetu.
Mwaka 2017, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres akiwa nchini Kenya, alinukuliwa akisema machafuko mengi hutokea pale haki za binadamu na za kiraia zinapokiukwa hasa chaguzi zinapokuwa sio za huru na haki.
Bado tunayo nafasi ya kufanya uchaguzi mkuu 2025 kuwa wa huru na haki ila tusihamasishe raia wasijiandikishe kwenye daftari la kudumu la kupiga kura, halafu tuwaache wenyewe waamue kupiga kura kwa mazingira ya sasa ama la.