UCHAMBUZI WA MJEMA: Makosa ya Waziri Mchengerwa, RC Chalamila haya hapa

Wiki iliyopita, umma wa watanzania umemshuhudia waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ‘akifoka’ kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amepoka mamlaka yake ya uwaziri.

Hii ni baada ya RC Chalamila kuruhusu mabasi na magari madogo kupita katika barabara za mradi wa mabasi yaendayo kasi (BRT) Jijini Dar es Salaam, akidai ni kutekeleza maagizo ya waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa.

Ukali wa waziri Mchengerwa ni kwamba BRT iko chini ya Tamisemi hivyo ni wizara hiyo pekee ndio iliyopaswa kutoa kibali cha mabasi na magari madogo kupita katika barabara hizo, hata kama kulikuwa na maagizo ya waziri Bashungwa.

Nimetangulia kuuliza nani yuko sahihi kati ya waziri Mchengerwa na RC Chalamila na katika kulielewa hili ni vizuri sana tukatafuta maagizo yalipoanzia, yalikuwaje au yalielekeza nini na je namna RC Chalamila alivyotekeleza ilikuwa ni sahihi>

Kwa hiyo tunapoamua kumtafuta mchawi kwa maana ya nani hasa amesababisha mtafaruku huu, ni lazima tujue hili jambo lilianzia wapi na kama ilikuwa sahihi kwa Waziri Mchengerwa kulizungumza kwa ukali kama alivyolizungumza hadharani.

Desemba 2024, waziri Bashungwa alisema kila akipita huko bararani anaona barabara za BRT ambazo zinasubiri kutumiwa na mabasi, zimekamilika lakini hazitumiki na wakati huo huo wananchi wanatesema kwenye foleni.

Kwa hiyo waziri Bashungwa akasema kwanini ule muda wenye foleni ndefu (peak hours), mabasi ya kawaida na magari madogo yasitumie barabara hizo kwa kusimamiwa na Trafiki, lakini mabasi ya BRT yakija, basi utaratibu huo utakoma.

Nikimnukuu alisema “Kwanini tusikae na Jeshi la Polisi na Tamisemi tukakubaliana ni lini mabasi ya BRT yatakuja”, na kwamba katika muda huu ambapo barabara zimekamilika, hakuna mabasi ya BRT basi barabara hizo zihudumie wananchi.

Lakini akamtaka RC Chalamila ku coordinate (kuratibu) jambo hilo tena akimsifia kuwa yapo mambo makubwa tu ameyaratibu na yakaenda vizuri hivyo alitarajia angeratibu Polisi na Tamisemi kukaa na kukubaliana.

Sasa kwa kauli ya waziri Bashungwa, alitambua kuwa ili kufanya uamuzi huo, ni lazima Tamisemi ishirikishwe (na kutoa kibali), na akaliacha suala hilo kwa RC Chalamila aliratibu, swali ni je, RC Chalamila aliwasiliana na Tamisemi?

Swali la pili, katika maelekezo ya waziri Bashungwa, hakuna mahali popote alizungumzia kuruhusu malori kupita kwenye barabara za BRT, nani aliruhusu malori kupita katika barabara hizo? Polisi wetu kwa maana ya Trafiki wamelala?

Nauliza hivyo kwa sababu wakati Waziri Bashungwa akitoa maelekezo hayo kwa RC Chalamila, viongozi wa Jeshi la Polisi walikuwepo siku hiyo na waziri akasisitiza Polisi na Tamisemi wakae pamoja wakubaliane chini ya uratibu wa RC Chalamila.

Hebu tuje alichokisema Chalamila, yeye alisema kutokana na maagizo ya waziri Bashungwa (sijui kama alikuwa ameshawasiliana na Tamisemi), akaagiza mabasi na magari madogo yapite barabara za BRT zilizokamilika lakini hazina mabasi hayo.

Akataja barabara ya kutoka Mbagala hadi katikati ya mji na kutoka Ofisi ya mkuu wa wilaya ya Ilala hadi Magomeni na kusisitiza kuwa sio barabara zote bali zile ambazo mabasi hayo ya mwendokasi hayajaanza safari katika njia hizo.

Kwa kauli ya Chalamila, hakuruhusu malori bali mabasi na magari madogo pekee lakini alifanya kosa la kiufundi kwa kutoainisha muda ule tu wa foleni inapokuwa kubwa kama Waziri Bashungwa mwenyewe alivyosema “Peak hours”.

Katika maelekezo ya Waziri Bashungwa na RC Chalamila, hakuna mahali hata mmoja aliruhusu malori nayo yapite katika barabara za BRT maana yake kuna chombo (Jeshi la Polisi) ambacho hakikutekeleza wajibu wake ipasavyo.

Mchengerwa anasema barabara ya Mbagala yanapita malori yenye uzito wa tani 30 hadi 40 na tayari barabara imeanza kuharibika na ndipo akahoji Chalamila alipata wapi mamlaka ya kuruhusu barabara za BRT bila kibali cha Tamisemi?

Nikimnukuu, Waziri Mchengerwa anasema “Sijui nani (akimlenga RC Chalamila) amewapa Mamlaka hayo ya kutoa kibali kwa sababu barabara hizo zinasimamiwa na DART (Wakala ya Mabasi Yaendayo Haraka) iliyopo chini ya Tamisemi”.

“Mwambie RC, hatuwezi kuruhusu malori kupita katikati ya barabara za mwendokasi. Haiwezekani. Kwa magari ya abiria itaeleweka. Wekeni utaratibu vizuri, leteni wizarani (Tamisemi) mpate kibali,”mwisho wa kunukuu.

Kwa kauli hiyo, Mchengerwa hana tatizo mabasi na magari madogo yakipita, isipokuwa lazima lipate kibali cha wizara yake, jambo ambalo ni wazi RC Chalamila anaweza kuwa hakuishirikisha Tamisemi kama Bashungwa alivyoelekeza.

Nimejaribu kueleza japo hili kwa kirefu na kuleta nini hasa yalikuwa maagizo ya Waziri Bashungwa na RC Chalamila, ambayo ukisoma utabaini maelekezo ya wazri Bashungwa yalikuwa wazi kabisa kuwa lazima Polisi na Tamisemi washirikishwe.

Ninaamini kama wangeshirikishwa chini ya uratibu wa RC Chalamila, maana yake Tamisemi ingekuwa imetoa kibali, Jeshi la Polisi nao kama wangekuwa wameshirikishwa wangefahamu kabisa malori hayakuruhusiwa kupita njia hizo.

Kama polisi walishirikishwa na kushiriki kama ambavyo Waziri wao alitaka iwe hivyo, na wakazembea na kuacha malori nayo yakapita katika barabara hizo basi hapo kuna kiongozi au viongozi wa Jeshi la Polisi wanapaswa kuwajibika.

Pamoja na yote hayo, ingawa Waziri Mchengerwa yuko sahihi kwamba yeye ndio ana mamlaka na barabara hizo, lakini sikufurahishwa na namna alivyofikishwa ujumbe wake wakati wangeweza kukaa ndani ya Serikali na kukaripiana huko.

Bahati mbaya, kipaumbele chake kilikuwa ni kutaka kuonyesha “mamlaka”, badala ya kutafuta njia bora ya kushughulikia mtafaruku huo pasipo kuivua nguo au kumnanga RC Chalamila na kufanya Serikali ionekane kama iko shaghalabaghala.

Haileti picha nzuri kwa wateule wa Rais kushutumiana hadharani kutokana na maamuzi ya mmoja wao, sielewi kwanini waziri Mchengerwa hakuona umuhimu wa kumwita Chalamila na Jeshi la Polisi na kuwaeleza kile ambacho hakiko sawa.

Wanazuoni wanasema Mawasiliano bora mahali pa kazi ni muhimu kwa ajili ya kuongeza ari ya wafanyakazi, ushiriki, tija, na kuridhika, na kusababisha ushirikiano bora wa timu, utatuzi wa migogoro na hatimaye, kuboresha matokeo chanya.

Kuonyeshana ubabe hadharani kwa wateule wa Rais hakuleti picha nzuri ndani ya Serikali na zaidi inaonyesha hakuna mawasiliano mazuri baina ya watendaji na ni kama wanagombea fito (mamlaka) badala ya kumtumikia mwananchi kwa tija.

RC Chalamila kuna mahali ameteleza, lakini Waziri Mchengerwa naye kuna mahali ameteleza kwa sababu umma unajua RC Chalamila alikuwa akitekeleza agizo la Waziri Bashungwa hivyo wanapata picha kuwa labda wawili hao hawako vizuri.

0656600900

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *