
Nimemsikia Rais Samia Suluhu Hassan akiwaambia wakurugenzi wa halmashauri au ‘Ma-Ded’ wenye nia ya kugombea ubunge, waseme mapema ili waachie nafasi hizo na mamlaka ya uteuzi impandishe aliye chini yake kushika wadhifa huo.
Rais Samia alitoa maelekezo hayo Machi 11, 2025 jijini Dodoma akifungua mkutano wa 39 wa viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), akisisitiza wasipofanya hivyo basi watakuwa wanacheza pata potea.
Katika maelekezo hayo, alisema ujumbe huo pia uende kwa watumishi wote wa umma wenye nyadhifa, hivyo kwa tafsiri yangu maelekezo haya pia yanakwenda kwa wakuu wa mikoa (Ma-RC), makatibu tawala na pia wakuu wa wilaya ‘Ma-DC.’
Nimetangulia kumpongeza Rais Samia nikisema maelekezo yake haya yatatusaidia kuondoa vurugu majimboni, kwa sababu tumeona katika baadhi ya majimbo kuna migogoro ya kimahusiano baina ya wateule hao na ukitafiti kiini ni ubunge 2025.
Mtifuano zaidi unatokea pale mkuu wa mkoa anapotamani jimbo mojawapo katika mkoa anaouongoza ama DED au DC wote wanatamani jimbo katika halmashauri au wilaya anayoiongoza, kila siku inakuwa mikwaruzano.
Wala mikwaruzano si baina ya wateule hao wao kwa wao, lakini mtifuano unaweza kuwa baina yao na wabunge walioko madarakani sasa. Wakati mwingine hata wanaweza kutoleana maneno ya kejeli hadharani.
Lakini ukiacha hili la kudharauliana na kuonyeshana ubabe majimboni, wateule hao hawatulii kwenye maeneo yao ya kazi, kila mara ama kwa kutoroka au kwa ruhusa, hukimbilia majimboni kuweka mambo sawa.
Hali hii huwafanya wabunge walio madarakani kuwa mguu mmoja ndani (bungeni) na mwingine nje (jimboni) kujaribu kuweka mambo sawa pale mtia nia anaposambaza sumu katika jimbo lake.
Kwa kauli ya Rais ambayo nitairejea katika aya zinazofuata, ni wazi itapunguza hekaheka majimboni, kutunishiana misuli, kufanyiana ubabe na hata kudharauliana waziwazi mbele ya wananchi.
Rais Samia alitumia kikao hicho kutuma ujumbe kwa watendaji wote wa Serikali na taasisi za umma, alimtaka Katibu Mkuu Kiongozi kusambaza waraka katika serikali za mitaa, kuwataka wateule hao wanaotaka majimbo waseme mapema.
Aliwaambia Ma-Ded kuwa yeyote mwenye nia ya kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu 2025 aseme mapema ili aliyepo chini yake apandishwe kushika wadhifa huo, badala ya kushtukiza na kuchukua fomu muda unapowadia.
Utaratibu huo kwa mujibu wa Rais, unafanya serikali za mitaa zikose viongozi au kukosa wasimamizi hivyo zitajazwa na watu wasio na uzoefu, lakini kama taarifa inatolewa mapema, wanaopandishwa wanapata muda wa mafunzo.
Endapo DED na watendaji wengine wa Serikali watachukua fomu wakati zikianza kutolewa, bila kutoa taarifa, basi Rais Samia kasema watakuwa wamekosa yote kwa maana atakuwa amekosa fomu na atakuwa amepoteza cheo chake.
Rais akawataka wakajipime na kufanya uamuzi mapema kwa kuwa asingependa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani 2025 ufanyike kwa kubahatisha, badala yake anataka usimamiwe na watu makini.
Kwa mujibu wa Rais Samia, watakaozingatia maelekezo hayo wana uwezekano mkubwa wa kupewa uteuzi endapo watashindwa lakini ni wale tu ambao ni watendaji, wachapakazi wazuri na wenye rekodi ya uadilifu.
Ingawa kauli ya Rais itapunguza misuguano tunayoishuhudia majimboni, lakini imeibua changamoto nyingine ya kutoeleweka, kwamba wapo Ma-DED tena ambao ni makada wa CCM wamepangwa kusimamia uchaguzi mkuu 2025.
Kilio cha kuundwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kinachangiwa na sura kama hizi kuonekana kusimamia uchaguzi. Ni vyema hata kama Ma-DED ndio watahesabika kama watumishi wa umma waandamizi, hawa makada wawekwe pembeni.
Turudi kwenye mada yetu ya msingi, hilo la Ma-DED ambao ni makada wa CCM kusimamia uchaguzi tutalijadili siku nyingine, lakini kauli ya kuwataka wajitokeze mapema ni jambo muhimu ili kutofifisha utendaji wa Serikali.
Hakuna asiyejua kuwa mwisho wa uchaguzi ndiyo mwanzo wa uchaguzi mwingine, kwa hiyo ni wazi hao wanaotamani ubunge leo hii ambao Rais Samia anawanyooshea kidole hawajaanza leo harakati, tayari walishaanzisha mitandao.
Wala haidhoofishi tu utendaji wa Serikali, lakini harakati zao majimboni zinadhoofisha pia utendaji kazi wa Bunge kwa kuwa kama nilivyotangulia kusema, akili za wabunge wanaotaka kutetea nafasi zipo kwenye majimbo yao zipo huko badala ya bungeni.
Licha ya uwepo wa kanuni za uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya dola, toleo la 2021 ambazo ndizo zinakwenda kuwa kichinjio kwa walioanza kampeni mapema, lakini ni kama kundi hili haliogopi kabisa kanuni hii.
Kifungu cha 25(5) kinasema: “Ni marufuku kwa mwanachama yeyote anayetarajia kugombea au wakala wake, kufanya vitendo ambavyo ni dhahiri kuwa sehemu ya kampeni za kuwania nafasi anayoitafuta kabla ya uongozi uliopo haujamalizika.”
Ibara ndogo ya (6) inasema ni marufuku kwa mwanachama anayetarajia kugombea au wakala wake, kutoa misaada mbalimbali wakati uchaguzi unapokaribia (kama huu wa 2025) ambayo ni dhahiri ina lengo la kuvutia kura.
Lakini kanuni hiyo hamgusi Rais, mbunge, mwakilishi au diwani ambaye yupo madarakani wakati huo kwa kuwa yeye atakuwa bado ana wajibu wa kuhudumia eneo lake la uongozi, iwe ni nchi nzima, jimbo au kata anayohudumu.
Ukisoma ibara ndogo ya 7(a) na (b) inasema kiongozi atakayechaguliwa katika kura za maoni lakini ikathibitika alivunja miiko hiyo, atavuliwa uongozi na pia kama ni mwanachama, hatateuliwa kugombea nafasi yoyote aliyoiomba.
Pamoja na Rais Samia kuwataka hao wanaotamani majimbo waseme mapema, naamini hata wakifanya hivyo haitakuwa ndiyo tiketi ya kwenda majimboni kufanya vurugu na kuwavuruga wabunge waliko madarakani.
Ni kweli Rais amewapa green light (amewawashia taa kuwaruhusu kutia nia), lakini hiyo haiwaruhusu kuvunja Kanuni za maadili ya chama kwa kwenda majimboni kuanza kampeni mapema, wakifanya hivyo waliwe kichwa tu.
Harakati zote zianze baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuvunjwa na CCM kutangaza utaratibu kwa wanaotaka kuteuliwa kuwania ubunge, tofauti na hivyo itakuwa ni vurugu majimboni.
Angalau kauli ya Rais inaweza kwenda kutibu tatizo lililopo katika baadhi ya majimbo kwa wateule hao kutunishiana misuli hadharani kwenye maeneo wanayoyatamani, ili kuwaonyesha wananchi nani ni zaidi ya mwenzake.
Ninaamini kauli za kibabe dhidi ya mbunge aliye madarakani ama DED, DC au miongoni mwao, kwa sababu tu ya ubunge 2025 zitakoma.
0656 600 900