UCHAMBUZI WA MJEMA: Hawa ndio maadui watatu wa Chadema uchaguzi mkuu 2025

Uchaguzi wa viongozi wa juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umemalizika lakini ukweli ni kuwa kuna usaliti wa chini kwa chini na wazi wazi unaendelea kukitafuna chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

Siku zote ukweli huwa una sifa moja kuu kwamba hata ukiuchukia au kuukataa, hauwezi kugeuka kuwa uongo na ni kwa msingi huo, ni wajibu wa viongozi na wanachama kuamua kusuka ama kunyoa kama wanakitakia mema chama chao.

Ni ukweli ulio dhahiri kuwa majeraha na makovu ya uchaguzi huo ni makubwa kutokana na aina ya kampeni zilizofanyika, bila kutibu majeraha chama hicho hakiwezi kutoboa uchaguzi mkuu 2025 kama kitaamua kushiriki uchaguzi huo.

Kwanini, kwa sababu kinakwenda kushindana na maadui watatu wakubwa, moja ni maadui ndani ya chama unaotokana na usaliti, mbili ni adui yao mkubwa ambaye ni Chama cha Mapinduzi (CCM) na tatu vyama vingine vya siasa.

Katika mazingira ya kisiasa tuliyonayo Tanzania kwa sasa, chama chochote kinachohitaji ushindi, kinahitaji umoja na mshikamano wao kwa wao kama vile mgonjwa na uji, kabla ya kutoka nje na kuomba kuungwa mkono na watanzania.

Ninafahamu kuna changamoto ya mifumo ya kisheria ya uchaguzi (legal frameworks), inayotoa hakikisho la uchaguzi huru na wa haki, lakini Chadema kinapaswa kutengeneza mshikamano na kutibu majeraha leo na wala si kesho.

Mwandishi wa vitabu vya mashairi raia wa Marekani Matthew Joseph Thaddeus Stepanek, maarufu kwa jina la Mattie Stepanek alipata kusema “Unity is strength… when there is a team work and collaboration, wonderful things can be achieved”

Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi, Stepanek anasema umoja ni nguvu, kwamba katika kufanya kazi kwa ushirikiano kama timu moja, mambo ya ajabu yanaweza kupatikana, na kwa muktadha wa makala haya ni ushindi kwa Chadema.

Hakuna ubishi uchaguzi katika nafasi ya mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho uliofanyika Januari 21,2025 Mlimani City jijini Dar es Salaam, umegawa viongozi na wanachama katika makundi mawili makubwa ndani ya chama.

Makundi hayo ni lililokuwa likimuunga mkono aliyekuwa mwenyekiti, Freeman Mbowe, ambalo baadhi wamekataa kukubali kushindwa na la mwenyekiti mpya, Tundu Lissu, ambalo linadaiwa kuwaweka pembeni waliokuwa kundi la Mbowe.

Siku zote katika uchaguzi kuna kushindwa ama kushindwa na kila upande unapaswa kuandaa wafuasi wao kisaikolojia kupokea matokeo yoyote yale, yawe mabaya au mazuri kwa upande wao na wajue kuna maisha baada ya uchaguzi.

Nilimsikiliza na kumwelewa Mbowe alipotoa hotuba yake mara baada ya matokeo kutangazwa na Lissu kuibuka kidedea, akisisitiza umuhimu wa kutibu majeraha ya uchaguzi huo, lakini sioni kasi ya kushughulikia ushauri huo kabla ya Oktoba 2025.

Nasema hivyo kwa sababu naona chuki za dhahiri na za wazi kwa baadhi ya waliokuwa kundi la Mbowe ambao ni kama wanaona wanastahili kupigiwa magoti na kuombwa radhi kwa kampeni wanazodai zilimdhalilisha Mbowe.

Ni kweli imani ya Mbowe, kampeni timu yake na wanachama waliokuwa wakimuunga mkono waliaminishwa na wakaamini Mbowe atashinda kwa asilimia 100, lakini haikuwa hivyo, ndio unanuna na wewe ni kiongozi au mwanachama?

Dalili za Lissu kushinda mbona zilionekana mapema tu kwamba kizazi cha sasa kilihitaji kiongozi wa aina ya Lissu na John Heche kama makamu wake kutokana na mazingira ya kisiasa ambayo Tanzania imeyapitia tangu uchaguzi wa 2019.

Sura za walionuna tunaziona kupitia matamshi na maandiko yao katika mitandao ya kijamii, ni kama vile watu waliokaa mbali wanaombea limharibikie Lissu, kila anachokiandika ni kile tu ambacho ni hasi (negative) kwa Lissu na uongozi mpya.

Tumo huko kwenye baadhi ya makundi ya WhatsApp, tunaona baadhi ya viongozi wa Chadema na wanachama waliokuwa watiifu kweli kweli wakati wa uongozi wa Mbowe, lakini sasa wamekengeuka, wanakibagaza chama chao mitandaoni.

Ni lazima watambue, unapotoboa mtumbwi, hazimi tu nahodha bali mnazama wote mliomo ndani ya chombo hicho na ndio maana nimetangulia kusema Chadema kwa hali mnayoenda nayo, mnapaswa kuchagua kunyoa au kusuka.

Yapo matukio na kauli nyingi tu zinatokea ndani ya Chadema ambazo ukichunguza kiini chake utabaini ni uchaguzi wa mwenyekiti wa chama taifa na ukiuliza si kwamba hawakubaliani na matokeo, la hasha bali aina ya kampeni zilizofanyika.

Huo ni pande wa kundi la Mbowe, lakini kundi lililokuwa linamuunga mkono Lissu, baadhi wanaowaona kundi lile la Mbowe kuwa ni maadui na ni kutokana na aina ya kampeni zilizofanyika hasa zilizofanywa na wapambe na ‘Chawa’ wa Mbowe.

Tunachokiona sasa, wapo baadhi ya viongozi katika kambi ya Lissu wanaona kama kumtaja Mbowe na mafanikio yake katika mikutano ambayo mgeni rasmi ni Lissu ni taboo (mwiko), na kuna kila dalili za kuanza kuwatenga kisirisiri.

Huu ni mwelekeo mbaya sana kwa chama cha siasa ambacho umma unakichukulia kama chama kikuu cha upinzani ambacho siku moja kinatarajiwa kinaweza kushika Dola njia pekee ya kutoka hapo kilipo ni kutafuta maridhiano haraka ya kweli.

Lakini katika kutafuta maridhiano hayo, ni lazima kila upande uweke mapanga chini na kujishusha kwa sababu uchaguzi umemalizika, chama chenu kimepata uongozi, kwa hiyo mnatakiwa kuungana kukabiliana na adui yenu mkubwa CCM.

Ninaamini huko ambako viongozi wa kitaifa wa Chadema wanapita wakifanya amsha amsha ya kampeni yao ya “No Reforms No Election” kwamba kama hakuna mabadiliko basi hakuna uchaguzi, wanaona watanzania wanavyojitokeza.

Lakini Chadema waelewe kuwa matendo na kauli za baadhi yao zinapunguza uhai wa chama chao na kama nilivyosema Tanzania inahitaji upinzani imara ili kuifanya Serikali inayoongozwa na CCM isibweteke au kujisahau ama kujimwambafai.

Vile vile ambavyo sitamani Chadema kipoteze mwelekeo, pia sitamani chama makini kama ACT-Wazalendo, Chama cha Wananchi (CUF) na vingine vichache, vipoteze mwelekeo kwani CCM kilichopo madarakani kinaweza kujisahau.

Sote tunafahamu namna Watanzania wanavyolitizama Bunge la sasa ambalo lina wingi wa wabunge kutoka CCM (asilimia zaidi ya 95), lakini ukilifanyia tathmini ni kuwa limepoteza ladha kwa sababu hakuna wabunge machachari wa upinzani.

Ninatamani kuona Bunge linalofanana na wakati akina Dk Wilbroad Slaa, Freeman Mbowe, Tundu Lissu, Zitto Kabwe, Godbless Lema, John Heche, Halima Mdee, Esther Bulaya, David Kafulila, Joseph Mbilinyi na James Mbatia wako bungeni.

Vyama vya upinzani na si hapa Tanzania tu, duniani kote vinafanya kazi kubwa ya kuwa jicho la umma (checks and balance), vinawasilisha maoni mbadala, hupendekeza sera mbadala na kuhamasisha umma kushiriki masuala ya siasa.

Lakini vyama vya upinzani pia huwa wajibu wa kutetea makundi yasiyo na sauti (minority), hukosoa utendaji wa serikali, husaidia kuibua mijadala ya wananchi lakini wajibu mwingine ni kujiandaa kushika Dola au kuingia madarakani.

Kwa hiyo hiki kinachoendelea ndani ya Chadema kwa baadhi ya viongozi wao na wanachama kukibagaza na kukinanga chama chao hakina afya na badala yake wataenda katika uchaguzi mkuu wakiwa wamechoka kweli kweli.

Ninatamani Lissu na Mbowe watoe hotuba katika jukwaa moja, kuwasihi viongozi wao na wanachama kuvunja makundi yao na kuwa wamoja na kusameheana kwa yaliyotokea katika uchaguzi wao na kufungua ukurasa mpya ili kuwa nguvu moja.

Wala wasijidanganye, wakienda hivi wanavyokwenda naamini safari yao itakuwa ngumu sana kwa sababu hata hiyo “No Reforms No Election” inahitaji nguvu ya pamoja ya kupata mafanikio chanya, tofauti na hivyo mna wale maadui watatu.

0656600900

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *