UCHAMBUZI WA MJEMA: Haki na amani ni watoto pacha uchaguzi mkuu 2025

Nimefurahishwa na ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha uchaguzi mkuu 2025 unafanyika kwa haki na furaha yangu kubwa ni neno ‘Haki’ kwa kuwa haki na amani ni kama watoto mapacha.

Akizungumza Machi 31, 2025 wakati wa Baraza la Idd El Fitri lililofanyika Jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisisitiza kuwa katika kuhakikisha haki inatamalaki, Serikali itasimamia misingi yote ya kanuni, sheria na desturi zote za uchaguzi.

Rais alitoa kauli hii wakati akijibu ombi la Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) kupitia kwa Katibu mkuu wake, Alhaji Nuhu Mruma, aliyeiomba Serikali kufanyia kazi dosari zilizojitokeza katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa 2024.

Katika ombi hilo, Katibu huyo aliziomba mamlaka za Serikali kuzifanyia kazi dosari zilizoripotiwa katika uchaguzi huo na kusisitiza suala la kutenda haki katika kila hatua ya mchakato wa uchaguzi kwani haki ndio msingi mkuu wa amani.

Akijibu ombi hilo, Rais alienda mbali na kusema kuna maboresho na mageuzi makubwa Serikali imeyafanya kama vile kuruhusu mikutano ya hadhara, kufuta sharti la kupita bila kupingwa na kuanzisha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Nimesikiliza mawaidha ya baadhi ya viongozi wa dini ya kiislamu maaeneo mbalimbali nchini, wamerudia neno ‘amani’ mara nyingi katika mawaidha yao bila kugusa neno ‘haki’ wakisahau kuwa bila haki, amani haiwezi kuwepo.

Dk Muhammad Mahathiri ambaye alipata kuwa waziri mkuu wa Malaysia, aliwahi kusema “We cannot accept the idea that there are groups that are superior to others. Justice should apply to everyone, regardless of race or religion”

Kwa tafsiri ya Kiswahili isiyo rasmi, kiongozi huyo anasema “Hatuwezi kukubali wazo kwamba kuna vikundi ambavyo ni bora kuliko vingine. Haki inapaswa kutumika kwa kila mtu, bila kujali rangi au dini”, na hapa naongeza Itikadi.

Mufti Ahmed Deedat ambaye ni mwanazuoni wa Kiisalmu nchini Afrika Kusini anayeheshimika sana kwa kutetea haki, anasema “Justice is the cornnerstone of any society. Without Justoce, no peace or stability can prevail in the world”

Ujumbe huu muhimu ambao aliutoa katika kusanyiko la kidini, unamaanisha kuwa “Haki ndio msingi wa jamii yoyote. Bila Haki, hakuna amani au utulivu unaoweza kutawala duniani”, ni kupitia mawaidha yao haya wanaheshimika sana duniani.

Askofu mkuu Desmond Tutu wa Afrika Kusini ambaye alipigania haki na amani katika jamii iliyokuwa ikikandamizwa na makaburu kutokana na ubaguzi wa rangi na alihubiri sana suala la maridhiano kama njia muhimu ya kudumisha amani.

Ni kupitia harakati zake hizo alisema “if you are neutral in situations of injustice, you have chosen the side of the oppressors”, akimaanisha Ikiwa hauegemei upande wowote katika hali za dhuluma, umechagua upande wa wadhalimu.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Oscra Romero wa El Salvador ambaye alipogania sana haki naye alipata kusema “The church cannot be silent when it sees the sufferings of the poor and oppressed. The church must speak out of injustice.

Papa John Paul wa II naye aliwahi kusema “Peace is not just the absence of war. It is the work of justice” akiamini kuwa amani ya kweli inaweza tu kupatikana kama haki itatolewa kwa wanaokandamizwa na haki hiyo ikalindwa na watawala.

Viongozi hawa wa Dini walibeba misingi ya haki, amani na utu wa binadamu, mara nyingi wakiwa katika hatari kubwa ya kibinafsi, wakitetea watu wanaoonewa na kutengwa katika jamii zao, tujiulize viongozi wetu wamesimama upande gani?

Sauti zao zinaendelea kuhamasisha harakati za haki na upatanisho duniani kote na nimeamua kuandika kile walichohubiri kwa makusudi kabisa, kuwaonyesha baadhi ya viongozi wetu hapa Tanzania wamekariri “amani” bila kuhubiri kwanza “Haki”.

Kwa hiyo kumbe hata hapa Tanzania, viongozi wetu wa dini wakihubiri haki katika chaguzi zetu, ni wazi moja kwa moja (automatically) amani itatamalaki, lakini ninaona baadhi ya viongozi wamegeuka chawa na kukumbatia udhalimu.

Siamini kama viongozi wetu wa dini (sio wote) hawakuona kilichotokea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na 2024 na uchaguzi mkuu 2020, ambacho kimsingi kama tusipotubu na kurudi kwenye mstari, amani yetu iko mashakani.

Sitaki kueleza nini hasa kilitokea katika chaguzi hizo kwa kuwa kila mtanzania anayefikiri sawasawa anafahamu, hivyo ni wajibu wa viongozi wetu wa dini kuhubiri haki katika nyumba zao za ibada ili haki hiyo izae mtoto amani.

Tunapozungumzia haki katika uchaguzi, tunamaanisha uwepo wa mifumo ya kisheria (legal frameworks) inayotoa haki kwa kundi moja na kukandamiza kundi lingine, au mifumo inayotoa fursa kwa vyombo vya Dola kuingilia uchaguzi.

Tangazo la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948 kuhusu haki za binadamu linatahadharisha kwamba watu wanaweza kulazimika kuasi ili kupinga dhuluma, maonevu na ukandamizali ambayo hutokea pale haki inapokuwa haipo.

Siku zote haki huletwa na utawala wa sheria na kwamba ni wazi kwamba utawala wa sheria unapotoweka, matokeo yake ni machafuko, fujo na maasi na Tanzania kuna dalili za kuelekea huko, lakini namshukuru Rais amekemea juu ya hili.

Waswahili wana usemi kuwa mtu aliyefiwa na mpendwa wake huwezi kumpangia namna ya kulia, ndivyo ambavyo inatokea kwa Chadema na ACT-Wazalendo wamechagua kulia na mifumo ya uchaguzi kuwa haitoki haki kwa upinzani.

Vipo vyama vya siasa ambavyo vimeamua kuchagua ule upande ambao Askofu Desmond Tutu aliusema, kwamba wao hawaoni tatizo kwenye chaguzi zote nilizozitaja na wanaridhika na mabadiliko ya sheria yaliyofanyika 2024.

Ni kipofu pekee ambaye anaweza asione kile kilichotokea 2019 na 2020 hadi Rais Samia akaja na 4R ili kutibu majeraha ya chaguzi hizo, lakini dawa aliyoiweka katika kidonda ni kama ilizidisha maumivu kwa kile kilichotokea 2024.

Kwa hiyo ni kama mtu aliyeumwa na nyoka, kwamba hata akiguswa na jani anashtuka, kwa hiyo sisi wapenda haki tungetamani kuona utofauti wa kauli hii ya Rais ya haki na kauli kama hii aliyoitoa wakati tunaenda uchaguzi wa 2024.

Viongozi wetu wa dini, baadhi kama nilivyosema, wasiwe wepesi tu wa kushangilia na kuimba wimbo wa amani bila kuimba kwanza haki ili haki imzae mtoto Amani. Viongozi wetu watoe kauli kali kukemea waliovuruga chaguzi nilizozisema.

Wengi wa watanzania ni waamini wa dini na ninaamini wengi tuna hofu ya Mungu, hivyo huu ni wakati muafaka wa viongozi wetu wa dini kusimamia uwepo wa maridhiano ya kweli kati ya viongozi wa Serikali ya CCM na upinzani.

Leo tunaweza kutafsiri kauli mbiu ya Chadema ya “No Reforms, No Election” kama ina lengo la kuvuruga amani, lakini hebu tuulizane, ni chama gani makini cha upinzani kitaendelea kukaa kimya kisidai haki kwa yaliyotokea 2019,2020 na 2024.

Ni kweli kwa mazingira ya kisiasa ya Tanzania, Chadema hawawezi kuzuia uchaguzi asilani, lakini hiki wanachokifanya ni “wakeup call” (iwaamshe watawala) kuwa kuna vuguvugu la watanzania linakuja kama haki itaonekana haitendeki.

Serikali ya CCM ijue ndio imeshikilia dhamana ya amani ya nchi yetu, ni ni wao wataamua kama nchi yetu itumbukie kwa machafuko ama la, kwa kuhakikisha inatenda haki kwa sababu hakuna mwenye hati miliki ya mama Tanzania.

Kwa hiyo viongozi wetu wa dini wanapohubiri amani, wajue kinachotangulia ni haki, hivyo waimbe wimbo wa haki hata mara 1,000 ili somo liwaingie watawala kwa sababu bila hivyo, amani inayohubiriwa inaweza kuwa ndoto siku zijazo.

0656600900

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *