UCHAMBUZI WA MALOTO: Lissu, Slaa wanavyoigeuza Chadema chama cha ‘wash and wear’

Nayaweka mawazoni maneno ya mwanasiasa wa New Zealand, Michael Laws kuwa “hakuna kitu kinaweza kukupa kichwa kikubwa cha habari kama kukishambulia chama chako cha siasa.”

Naukumbuka mkutano wa Dk Willibrod Slaa na waandishi wa habari, Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, Agosti 2015.

Kamera zilikuwa nyingi. Kuna televisheni ziliurusha mkutano huo moja kwa moja, kinyume na utamaduni uliozoeleka. Sababu ni kuwa Slaa alikuwa anakishambulia chama chake, Chadema.

Slaa alikuwa Katibu Mkuu Chadema. Chama hicho kikiwa kinaingia kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015, Slaa alikataa kukaa kimya. Alianika msimamo wake dhidi ya chama chake. Akatangaza kustaafu siasa.

Chadema, walimkaribisha Waziri Mkuu wa Nane Tanzania, Edward Lowassa, wakampa tiketi ya kugombea urais. Kitendo hicho, Slaa alikitafsiri sawa na “kuingia mkataba na shetani”. Chama kilichosaini mkataba na shetani ni chama cha kishetani.

Tafsiri; Slaa alimaanisha kuwa Chadema ni chama cha kishetani. Taasisi ya kishetani inakuwa imemwasi Mungu. Slaa, kwa kuwa yeye ni mtakatifu, akajiweka kando.

Haitoshi, Slaa aliwaambia Watanzania wamchague mgombea wa CCM, Dk John Magufuli. Aliwaonya kuhusu Lowassa. Aliwapa tahadhari zenye kuzunguka nyuzi 360 kuwa Chadema imeshasaliti mapambano ya kudai haki, maana imekuwa taasisi ya kishetani.

Slaa alipoona “dozi” haijakolea, akaandika kitabu. Jina lake ni “Nyuma ya Pazia”. Humo ndani amewatuhumu viongozi wa Chadema kuwa ni wasaliti. Sura ya 18 ya kitabu, Slaa ameipa kichwa: “Kuingia Mkataba wa Shetani; Mkataba wa Shetani ni wa motoni.”

Jina la kwanza ambalo Slaa ameanza nalo kwenye sura hiyo ya Mkataba wa Shetani, ni la Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu. Slaa ameandika kuwa Lissu alimpa kichefu, akamshangaa na kumdharau, kwa sababu aliutetea mkataba wa Shetani.

Slaa amemchambua Lissu kama mtu asiye na msimamo, mwenye kusukumwa zaidi na masilahi, hasira, kinyongo na hisia. Uchambuzi huo wa Slaa, umemweka Lissu katika kundi la watu wasio na maadili na hatari zaidi kwa taifa.

Kipindi Lissu aliposhambuliwa kwa risasi 38, Dodoma, 16 zikipenya mwilini na kusababisha afanyiwe oparesheni 24, Slaa alisema kuwa Chadema kuna vikundi vya utekaji, vinavyodhuru watu. Alitaka umma wa Watanzania uitazame Chadema kuhusu shambulio la Lissu, kupotea kwa Ben Saanane, na matukio mengine ya aina hiyo.

Septemba 15, 2007, viwanja vya Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam, Slaa alimtaja Lowassa kwenye Orodha ya Mafisadi (List of Shame). Kuanzia wakati huo, Lowassa alitambulika kama alama ya ufisadi Tanzania. Lissu ndiye mwandishi wa List of Shame, iliyosomwa na Slaa.

Agosti 2015, Lowassa alihamia Chadema. Lissu aliambatana na Lowassa, akimsafisha tuhuma zote za ufisadi ambazo chama hicho kilimtupia mwanzo. Hadithi ya “mchawi mpe mwanao akulelee”, walimwita Lowassa fisadi, naye akaenda kugombea urais kwao. Wangemfanyiaje kampeni? Ikabidi wamsafishe.

Mchezo huo, Lowassa alinufaika nao vizuri kabisa. Hata pale Lowassa alipoondoka Chadema na kurejea CCM, hakuna aliyefungua kinywa kumwita fisadi. Lowassa alifariki dunia Februari 10, 2024, na kila mtu alisema mema ya kiongozi huyo.

Sakata la Lowassa ni kumbukumbu kuwa Lissu aliyeandika waraka wenye kumtaja Lowassa kama fisadi, kupitia mgongo wa taasisi yake, Chadema, alizunguka majukwaani akimsafisha, akamtetea, kwamba mengi alisingiziwa.

Kisha sasa, kuna Slaa. Alitangaza kustaafu siasa, akainanga Chadema kila upande, akawabagaza na kuwaita majina mabaya viongozi wake, hususan Lissu. Machi 23, 2025, alirejea rasmi Chadema, akaomba radhi. Lissu, Mwenyekiti, akampamba kuwa enzi Slaa akiwa katibu mkuu, chama hicho ndiyo kilikuwa na nguvu.

Kutoka hadithi ya Lowassa, hadi Slaa, muktadha ni kuwa upo mchezo wa kuifanya Chadema kuwa chama chenye siasa za “wash and wear”. Yaani rahisi kusafishwa na kuwa msafi tena. Ukimuuliza Slaa leo, je, Lissu hana maadili? Ni kigeugeu? Mbinafsi anayeongozwa na maslahi, vinyongo na hasira? Majibu yatakuwa tofauti.

Je, Chadema kuna vikundi vya kuteka na kudhuru watu? Slaa hawezi tena kutamka maneno hayo. Kurejea kwake Chadema, kuna maana sasa chama hicho kimekuwa kisafi, vilevile Lissu, mwenyekiti, ni msafi.

Wash and wear ni nguo ambazo zimeundwa na malighafi, ambazo ni rahisi kuzifua, kukauka na kuvaa bila hata kupiga pasi. Lissu kwa Lowassa, na Slaa kwa Lissu, kupitia taasisi hiyohiyo, Chadema, wanathibitisha kwamba mtu awe mchafu kiasi gani, anaweza kugeuzwa msafi kama malaika ndani ya siku moja.

Ukiwa mchafu wa kutapikwa, Chadema wakiamua unakuwa msafi, mwadilifu na unayefaa kwa matumizi ya kikamanda. Inawezekana Lissu kamkaribisha Slaa Chadema ili kumsuta kwa maneno yake. Bila kufungua kinywa, lakini anamsema kwa kejeli: “Tamka tena sisi Chadema ni watekaji na mimi ni kigeugeu nisiye na maadili.”

Slaa ameomba radhi, lakini hajasema aliyoyaandika kwenye kitabu chake alikosea au ni uongo. Akisema hivyo, kesi itakuwa kubwa zaidi, kwani kumbe aliwatapeli watu walionunua kitabu na kusoma taarifa za uongo.

Somo kwa jumla, linanielekeza kifanya marejeo ya Dhambi Saba za Kijamii (Seven Social Sins), kama zilivyoandikwa na mchungaji wa Kanisa la Anglikana, Uingereza, Frederick Donaldson, Machi 20, 1925.

Dhambi hizo zimeorodheshwa kama ifuatavyo; Utajiri bila kazi, furaha bila dhamira, biashara bila maadili, elimu bila uhusika, sayansi bila ubinadamu, dini bila sadaka na siasa bila misingi. Lissu kumtakasa Lowassa na kumpokea Slaa, licha ya mengi mabaya aliyoyasema. Lissu kurejea Chadema pamoja na yote aliyoyasema na kuyaandika, ni matokeo ya siasa bila misingi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *