UCHAMBUZI WA MALOTO: Kazi na utu inampambanua Samia kwenye njia za Magufuli

Kaulimbiu za kampeni ni silaha yenye nguvu kwa chama cha siasa au mgombea. Donald Trump alijitengenezea mtaji mkubwa haraka, alipoinuka na kaulimbiu, “Make America Great Again” – “Fanya Marekani Iwe Kuu Tena”.

Barack Obama, alipokuwa anawania urais wa Marekani mwaka 2008, alitumia kaulimbiu ya “Hope” – “Matumaini.” Hata hivyo, umma ulichukua maneno yake, “Yes We Can” – “Ndiyo, Tunaweza”, yakawa maarufu na yaliyotumika zaidi, kuliko hata mwaliko wake wa mabadiliko, “Change We Can Believe In” – “Mabadiliko Tunayoweza Kuyaamini.”

Mwaka 2012, Obama alikuwa na kaulimbiu, “Forward” – “Mbele”. Ni sawa na Rais wa Nne wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete, aliingia na kaulimbiu, “Ari Mpya, Nguvu Mpya, Kasi Mpya”, muhula wa pili, akatumia, “Ari Zaidi, Nguvu Zaidi, Kasi Zaidi.”

Aghalabu, kila mwanasiasa hujipambanua kupitia kaulimbiu yake. Rais wa Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, alitumia, “Ukweli na Uwazi”. Rais wa 46 wa Marekani, Joe Biden, aliibuka na “Build Back Better” – “Jenga Tena Vizuri”, alipomaanisha kuwa Marekani ilihitaji ujenzi mpya baada ya kuharibiwa na Trump.

Rais wa Tano wa Tanzania, Dk John Magufuli, alitumia kaulimbiu, “Hapa Kazi Tu”. Ilikuwa inampambanua yeye binafsi kama kiongozi mchapakazi, asiyependa uvivu na kubweteka.

Rais Samia Suluhu Hassan, ameshaiboresha kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu” mara mbili. Awali, alianza na “Kazi Iendelee”, sasa anatembea na “Kazi na Utu”. Kuna faida nyingi kupitia uboreshaji huo.

Rais Samia alipokea kijiti katika mazingira magumu. Mtangulizi wake, Dk Magufuli, alifariki dunia. Yeye, Makamu wa Rais, akaapishwa kushika madaraka, kutii matakwa ya kikatiba, ibara ya 37 (5).

Aliposema “Kazi Iendelee”, ilikuwa na tafsiri kwamba “Hapa Kazi Tu” ya Magufuli haikupaswa kuishia njiani, hivyo akaiendeleza. Miaka minne ya urais wa Samia, imetafsiri mwendelezo wa Kazi.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, Rais Samia akiwa mgombea wa CCM, tayari kaulimbiu yake, “Kazi na Utu”, imeshazinduliwa. Ndani ya Kazi na Utu, unamwona Magufuli anaendelea, lakini ni Magufuli mwenye vionjo vya Samia.

Kukamilika kwa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), chini ya uongozi wa Rais Samia, ni kielelezo cha mwendelezo wa Hapa Kazi Tu, kupitia Kazi Iendelee. JNHPP ni alama ya Magufuli, japo alipofariki dunia, mradi huo ulikuwa asilimia 37. Samia ameukamilisha.

Desemba 20, 2023, Rais Samia alihudhuria utiaji saini baina ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Shirika la Ujenzi wa Reli la China (CRCC), kwa ajili ya kukamilisha kipande cha reli ya standard gauge, Tabora hadi Kigoma.

Rais Samia aliwapa watu tabasamu, hususan wale waliohisi mradi wa ujenzi wa reli ya standard gauge (SGR), ungekwama kwa sababu ya kufariki dunia kwa Magufuli.

Daraja la Kigongo – Busisi, linalotarajiwa kukamilika Aprili 30, 2025, ni mwendelezo wa Kazi. Miradi yote mikubwa, Rais Samia ameikamilisha kwa ufanisi. Wapo wanaosema amefanya kwa kasi kuliko Magufuli. Yote kwa yote ni ukweli wa kutembea na kaulimbiu, “Kazi Iendelee”.

Kazi na Utu

Rais Samia amekuwa chemchemi ya utu kwa jinsi anavyofanya mageuzi mengi ya utawala bora na ustaarabu wa kisiasa, tofauti na hali aliyoikuta alipoingia ofisini. Hili limesababisha wapenzi wa demokrasia na utawala bora, wamwone ni kiongozi mwafaka katika mazingira yaliyopo.

Mathalan, Rais Samia alikosoa fedha za makubaliano ya msamaha wa jinai (plea bargain), baina ya Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali na watuhumiwa, kuingizwa kwenye akaunti binafsi na nyingine kufichwa China.

Ni kwa sababu kipindi cha uongozi wa Magufuli, kesi nyingi za uhujumu uchumi ziliibuliwa, kisha ikaelezwa watuhumiwa walibanwa kutoa fedha kupitia jina la plea burgain ili wawe huru. Katika mazingira hayo, inaelezwa dhuluma kubwa ilifanyika.

Kitendo cha Rais Samia kutamka waziwazi kuwa kuna matendo yasiyofaa yaliyofanyika kwenye mchakato wa plea bargain, kiliamsha shamrashamra kwa waliopitia msoto wa kutoa fedha ili kugharimia uhuru wao.

Kisha, Rais Samia aliunda Tume ya Haki Jinai, ambayo wajibu wake ilikuwa kuchunguza na kutoa mapendekezo ya jinsi ambavyo haki za jinai zinapaswa kuchakatwa ili kusiwepo uonevu. Eneo hili pia linapambanua uongozi wenye utu wa Rais Samia. Kesi za kubambikiana ni nyingi. Rais Samia katika nyakati za mwanzo kabisa ofisini, alianza kushughulikia kesi za kubambikia kuanzia polisi mpaka Takukuru na akaagiza zifutwe. Na nyingi zilifutwa.

Rais Samia alitoa onyo kwa polisi, tabia ya kuwategeshea watu wasio na hatia dawa za kulevya na kuwapa kesi. Halafu, Machi 8, 2023, Rais Samia aliweka rekodi alipohudhuria kama mgeni rasmi, kongamano lililoandaliwa na Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha). Ilikuwa mara ya kwanza tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa urejeshwe mwaka 1992, Rais kuhudhuria shughuli ya kisiasa ya chama cha upinzani.

Matukio ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, na mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Godbless Lema, kurejea nchini salama baada ya kuishi uhamishoni tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu 2020, ni kielelezo cha siasa za utu za Rais Samia.

Mei 2022, Rais Samia alipokuwa Bukoba, Kagera, aliagiza mamlaka za kodi kuachana na madeni ya muda mrefu, badala yake wasimamie makusanyo kuanzia mwaka 2021. Kauli hiyo ilipokelewa kwa tabasamu pana na wafanyabiashara kwa kuwa wengi wao waliona walikuwa wakibambikiwa madeni ya nyuma pasipo haki.

Tabasamu kwa wafanyabiashara limechanua mpaka kwa wanaoanza na wanaotarajia kuingia kwenye ujasiriamali, baada ya tamko la Wizara ya Viwanda na Biashara, kueleza kuwa Rais Samia ametoa ruhusa kwa biashara mpya kutotozwa kodi mpaka angalau zifikishe miezi sita.

Ruhusa ya mikutano ya hadhara ya kisiasa ambayo ilitolewa na Rais Samia, Januari 2023, ilichanua tabasamu la kila mwanasiasa na mwanademokrasia.

Rais Samia pia amekuwa liwazo la wanasiasa waliokuwa na kinyongo kwa matukio ya chuki za kisiasa na ukandamizaji uliofanyika kipindi cha mtangulizi wake.

Wafanyakazi kuanza kupata nyongeza ya mishahara baada ya kuikosa kwa miaka saba, vilevile kupandishwa madaraja. Waliofilisiwa kupitia uvamizi wa maduka ya kubadilisha fedha, kurejeshewa fedha zao.

Wanafunzi wajawazito kupewa fursa nyingine kurudi shuleni baada ya kujifungua. Wagonjwa kufikiwa mmoja mmoja na kulipiwa matibabu hadi nje ya nchi, mfano hai akiwa mwanamuziki na mbunge wa zamani wa jimbo la Mikumi (Chadema), Joseph Haule “Prof Jay.”

Mifano hiyo, inafafanua pasina shaka kuwa Rais Samia anaendeleza Kazi, kwa kasi sawa au kuzidi ya mtangulizi wake, Magufuli, lakini kwa kuzingatia utu. Hivyo, kauli mbiu, “Kazi na Utu” inamtosha Rais Samia, bila shaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *