UCHAMBUZI: Afcon 2025 mzigo upo hivi

Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ itakuwa katika kundi C kwenye fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) zitakazofanyika Morocco kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026.

Droo ya upangaji wa makundi ya fainali hizo iliyofanyika Rabat, juzi Januari 27, 2025 iliipeleka Taifa Stars katika kundi hilo ambalo litakuwa pia na timu za Nigeria, Tunisia na Uganda.

Kwa mujibu wa ratiba ya fainali hizo, Taifa Stars itafungua dimba ikicheza na Nigeria, Desemba 23 katika Uwanja wa Fez, kisha Desemba 27 itakabiliana na Uganda katika Uwanja wa Al Barid, Rabat na mechi ya mwisho itakuwa ni dhidi ya Tunisia, Desemba 30.

SHUGHULI PEVU

Taifa Stars imekuwa na historia ya unyonge dhidi ya timu zote tatu ambazo imepangwa nazo kwa kuzingatia kumbukumbu ya mechi za kimashindano baina ya timu hizo huko nyuma.

Dhidi ya Nigeria, Taifa Stars haijawahi kupata ushindi katika mara zote ambazo zimewahi kukutana ambapo timu hizo zimecheza mechi nane za kirafiki na kimashindano, Nigeria ikipata ushindi mara tano na zikatoka sare tatu.

Katika mechi mbili ambazo Taifa Stars imewahi kucheza na Tunisia, imepoteza moja na kutoka sare moja na imekutana na Uganda mara 61 ambapo Taifa Stars imepata ushindi mara 13. sare 15 na Uganda imepata ushindi mara 33.

DABI TANO ZA MOTO MAKUNDI

Makundi sita ya Afcon 2025 yaliyopangwa juzi, yameibua mechi tano ambazo zitakutanisha timu za kanda moja kisoka jambo ambalo huenda likafanya mechi hizo kuwa na mvuto na ushindani wa hali ya juu.

Katika kundi A kutakuwa na mechi inayozikutanisha timu mbili zinazotoka Ukanda wa Soka wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (Cosafa) ambazo ni Comoro na Zambia iliyopangwa kuchezwa Desemba 26, katika Uwanja wa Mfalme Mohammed wa VI, Casablanca.

Kwenye kundi C kuna hiyo mechi ya Uganda dhidi ya Tanzania ambazo ni timu zinazotoka Ukanda wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Kundi B litakuwa na mechi tatu za dabi ambazo zitakutanisha timu tatu kutoka Cosafa. Desemba 22, Afrika Kusini itakumbana na Angola, Desemba 26, Angola itacheza na Zimbabwe kisha Desemba 29, Zimbabwe itacheza na Afrika Kusini.

Kundi F kutakuwa na dabi ya timu zinazotoka Ukanda wa Afrika ya Kati (UNIFFAC), Cameroon dhidi ya Gabon ambayo itachezwa Desemba 24 na dabi nyingine ni ya Ukanda wa Afrika Magharibi (Wafu) baina ya Senegal na Benin, Desemba 30.

MARAFIKI LIGI KUU BARA KUGEUKA WAPINZANI

Upangaji wa makundi hayo utafanya baadhi ya wachezaji wanaocheza pamoja katika timu za Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa wapinzani kwa muda.

Mali na Zambia zilizopangwa kundi A, zitafanya kipa Djigui Diarra kuwa upande tofauti na Clatous Chama na Kennedy Musonda wa Zambia.

Kundi C litawakutanisha Khalid Aucho wa Uganda na Mudathir Yahya, Clement Mzize, Ibrahim Bacca na Dickson Job wa Tanzania ambao wote wanacheza Yanga, wakiwa tofauti siku hiyo. Mechi hiyo ya Uganda na Tanzania pia itawakutanisha Steven Mukwala, Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein na Kibu Denis wanaocheza pamoja Simba wakiwa upande tofauti.

USHIRIKI WA TAIFA STARS AFCON

Hii itakuwa mara ya nne kwa Taifa Stars kushiriki Afcon baada ya kufanya hivyo mwaka 1980 (Nigeria), 2019 (Misri) na 2023 (Ivory Coast) ambapo nyakati zote hizo imeishia makundi. Katika ushiriki huo wa Taifa Stars kwenye michuano ya Afcon, mara moja pekee ndiyo haikuambulia hata pointi moja. Ilikuwa mwaka 2019 lakini 1980 ilipata pointi moja na 2023 ikaondoka na pointi mbili. Mwaka huu itakuwaje?