Uchaguzi wanukia TPLB, Mnguto aking’atuka Coastal

Dar es Salaam. Uamuzi wa Steven Mnguto kutotetea nafasi ya uenyekiti wa klabu ya Coastal Union hapana shaka utailazimisha Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kufanya uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi ya mwenyekiti, mwaka mmoja kabla ya uchaguzi wake mkuu.

Kwa mujibu wa katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), mwenyekiti wa TPLB ambaye pia ni makamu wa pili wa rais wa shirikisho hilo ni lazima awe mwenyekiti wa klabu inayoshiriki Ligi Kuu hivyo Mnguto atapoteza sifa yake ya kuongoza bodi ya ligi kuanzia pale Coastal Union itakapopata mwenyekiti mpya.

Ilionekana kama Mnguto angetetea nafasi yake ya uenyekiti wa Coastal Union katika uchaguzi mkuu wa klabu hiyo utakaofanyika  Desemba 23 jijini Tanga lakini katika orodha iliyotolewa na mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya klabu hiyo, Emannuel Kiariro, jina la Mnguto alipo na mwenyewe amekiri kuwa hatogombea.

“Hadi hapo nilipofanya nashukuru, kuiongoza Coastal Union sio kitu kidogo, nimeamua kupumzika, sitakuwa sehemu ya wagombea waliopo sasa,” alisema.

Jana wakili Kiariro aliweka hadharani majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali za klabu hiyo huku ile ya uenyekiti ikiwa na wagombea wawili na ujumbe ikiwa na watia nia 21.

Majina yaliyopitishwa kuwania nafasi ya uenyekiti ambao mmojawapo atakuwa mrithi wa Mnguto ni Hassan Ramadhan Muhsin na Abdulrahman Fumbwe.

Nafasi ya makamu mwenyekiti wa klabu hiyo ya Tanga, ina wagombea wawili ambao ni Dk. Ally Fungo na Mohammed Kiruasha Mohammed.

Idadi ya watu  21 wamejitokeza kuwania nafasi za ujumbe wa kamati ya utendaji ambao ni Hussein Abdallah Moor, Khamis Seleh Khamis, Emmanuel Abdallah Mchechu, Khamis Karim Khamis, Saida Said Bawazir na Nassor Mohammed Nassor.

Wengine ni Ally Hussein Kingazi, Hafidh Nassor Suleiman, Abdullah Mbaruk Abdullah, Abdallah Zubeir Unenge, Mohammed Maulid Rajab, Baraka Mohammed Baraka, Injinia Baraka Fumbwe, Ahmed Awadh Ahmed, Salum Juma Mwawado.

Pia wapo Ally Saleh Sechonge, Omar Mtunguja Kombo, Thabit Mwinyi Abuu, Hussein Ally Mwinyihamis, Sudi Said Hilal na Wazir Mohammed Wazir.