
Dar es Salaam. Wakati kesho Jumatano Novemba 20, 2024 pazia la kampeni za kuwania uongozi katika uchaguzi Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji likifunguliwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesisitiza hakitajitoa katika mchakato huo.
Mbali na hilo, chama hicho kimewataka wagombea walioenguliwa kutokata tamaa, badala yake waendelea kupambana hadi haki yao ipatikane.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameeleza hayo leo Jumanne, Novemba 19, 2024 wakati akizungumza na wanahabari kuhusu hatima ya uchaguzi huo utafanyika Jumatano ya Novemba 27, 2024.
Katika maelezo yake, Mbowe amesema mchakato wa kuengua wagombea hasa wa upinzani unaudhi, ndio maana kumekuwa na maoni tofauti kutoka kwa makada wa chama hicho wakishauri Chadema ijitoe, wengine wakitaka isijitoe badala yake wakomae.
“Kuengeuliwa kwa wagombea kunaudhi na wanaolia ni wengi, baadhi wanasema mwenyekiti (Mbowe) tujitoe katika uchaguzi, wengine wanasema hapana tupambane hadi damu ya mwisho.
“Kikao cha Kamati Kuu cha Machi 6 2024, mjini Mtwara, kilitoka na azimio la kushiriki uchaguzi huu, licha ya mapungufu yote, kwa sababu ndani ya miaka mitano haikuwa na mwenyekiti wa Serikali. Hivi kweli maelfu ya wagombea wa vyama upinzani hadi leo wana shida ya kujaza fomu?” amehoji Mbowe.
Changamoto ya wagombea kuenguliwa imekuwa kilio kwa kila vyama hasa vya upinzani vilivyodai wagombea wao kuondolewa katika mchakato huo kwa makosa madogo, ikiweamo kutokuwa na udhamini wa chama ngazi ya chini, muhuri, kukosea majina na suala la ujasiriamali.
Hatua hiyo ilisababisha CCM kupitia katibu mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi kuiomba Tamisemi kuyapuuza makosa madogo yaliyojitokeza wakati wa ujazaji wa fomu ili kuwepo wagombea wengi katika uchaguzi huo.
Novemba 12, 2024 Waziriwa Nchi, Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa aliongeza muda wa uwasilishaji wa rufaa hadi Ijumaa Novemba 15, saa 12 jioni, akizitaka kamati za wilaya kuitisha fomu za wagombea wote walioenguliwa ili kufanya mapitio na kujiridhisha na sababu zilizochangia wagombea kutoteuliwa ili haki itendeke kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi huo.
Novemba 16, 2024 akitoa tathimini ya mwenendo wa uchaguzi huo, Waziri Mchengerwa taarifa alizozipata za halmashauri mbalimbali hadi siku hiyo jumla ya rufaa 6,309 zilipokewa kati 5,589 zilizokubaliwa.
Hata hivyo, Mbowe ambaye ni mbunge wa zamani wa Hai mkoani Kilimanjaro amesisitiza pamoja na changamoto mbalimbali safari, Chadema haitajitoa kama ilivyofanya mwaka 2019 katika uchaguzi ambao CCM ilishinda kwa asilimia zaidi ya 90.
“Safari hii hatujitoi, tutakwenda nao mlalo mlalo hadi tufike safari yetu, rai yangu kwa viongozi na wanachama wetu mliopo kila eneo lina mazingira tofauti hakikisheni mnaandaa ilani za uchaguzi kulingana na maeneo yenu kwa sababu changamoto za mitaa hazifanani,” amesema Mbowe.
Amesema baada ya wagombea wao kuenguliwa katika ngazi ya vijiji, wamebaki 4,175 kati ya vijiji 12,333 na kwenye mitaa wamepata wagombea 2,686 kati ya mitaa 4,269 na wagombea 14,805 wa vitongoji wamebaki kati ya vitongoji 64,274.
“Hata hawa tuliowapata sio kazi ya kitoto, katika mazingira yaliyopo, licha ya wengine kuenguliwa pasipo utaratibu kufuatwa, lakini viongozi wetu walipambana katika kuijenga demokrasia,”amesema Mbowe.
“Kwa hiyo mambo yote yanayofanyika yanalindwa na kanuni ya 50 (uhalisia 49), hawawezi kuchukulia hatua yoyote au kufukuzwa kazi wala kushtakiwa wanalindwa na kanuni,” amesema Mbowe.
Akumbuka miaka saba ya JPM
Mbowe amesema baada ya kupitia changamoto mbalimbali katika utawala wa hayati John Magufuli, chama hicho, kilianza kujipanga upya, kuanzia katika vitongoji baada ya Serikali kuruhusu shughuli za kiasiasa kuendelea.
“Tangu vyama kuruhusiwa kufanya kazi kwa muda wa miezi 22, wapambanaji wanawake na wanaume walipambana, usiku na mchana ili kuirejesha heshima ya Chadema,”amesema.
Hata hivyo, Mbowe amesema anafarijika kama mwenyekiti kupata viongozi wa chama hicho katika ngazi za vitongoji, vijiji wilaya, mkoa hadi kanda na hatua inayofauta ni uchaguzi mkuu wa ndani chama hicho utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.
Amefafanua kuwa michakato ya uchaguzi ya ndani ya chama hicho, iliyofanyika ni kwa ajili ya kukiandaa chama katika chaguzi za Serikali, mitaa, vijiji, vitongoji na uchaguzi mkuu.
Naye, katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika amesema Chadema haijakubaliana na maeneo yoyote na Tamisemi, kuhusu mchakato wa uchaguzi wa Serikali ikiwamo uandikishaji, ratiba ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa wagombea hadi uchaguzi huo kusimamiwa na ofisi hiyo.