Dar es Salaam. Mwangwi wa Maalim Seif Sharif Hamad bado unasikika Zanzibar inapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2025, ukiwa ndio kwanza tangu uanze mfumo wa vyama vingi visiwani humo.
Vilevile, chama chake cha ACT – Wazalendo nacho kinatazamiwa kushiriki uchaguzi huo, bila mwanasiasa huyo anayetajwa kama alama ya demokrasia ya vyama vingi na ushindani katika siasa za visiwa hivyo.
Pamoja na uhalisia huo, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu anasema misingi iliyojengwa na Maalim Seif imebaki kuwa silaha ya ushindani kwa chama hicho Zanzibar.
Maalim Seif alifariki dunia Februari 17, 2021, akiwa makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, wadhifa aliokalia kwa miezi mitatu tangu alipoapishwa Desemba 8, 2020.
Maalim aliteuliwa kuwa kushika wadhifa huo kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) visiwani humo, baada ya kuibuka mshindi wa pili katika matokeo ya urais wa Zanzibar mwaka 2020.

Katika uchaguzi huo, Maalim Seif aliyegombea kwa tiketi ya ACT Wazalendo, alipata kura 99,103, nyuma ya Dk Hussein Mwinyi wa CCM aliyeshinda kwa kura 380,402, sawa na asilimia 76.27.
Tangu zianze siasa za vyama vingi mwaka 1995, Maalim Seif ndiye aliyekuwa mshindani mwenye nguvu katika chaguzi zote visiwani humo, kuanzia alipokuwa CUF na baadaye ACT Wazalendo.
Safari ya kisiasa ya mwanasiasa huyo ilianzia CCM miaka ya 1980 hadi aliposhika wadhifa wa Waziri Kiongozi kabla ya kuondolewa na hatimaye kufukuzwa uanachama.
Katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, Maalim Seif akiwa mgombea wa CUF, alishika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 49.76 dhidi ya asilimia 50.24 alizopata Dk Salim Amour wa CCM.
Matokeo hayo, yalifungua ukurasa wa ushindani wa mwanasiasa huyo katika siasa za Zanzibar, na tangia hapo kila uchaguzi alishika nafasi ya pili, ingawa hakuwahi kukubaliana na matokeo.

Katika uchaguzi wa mwaka 2000, Maalim aliwania urais kwa tiketi ya CUF dhidi ya Amani Abeid Karume wa CCM na matokeo yalipotangazwa, Maalim Seif alipata asilimia 32.96 huku Karume akitangazwa kushinda kwa asilimia 67.04.
Matokeo hayo yaliwatia hasira wafuasi wa chama hicho na Januari 28, 2001 waliandamana kupinga matokeo katika tukio lililosababisha mauaji na baadhi ya Wazanzibari kukimbilia nje nchi.
Hata uchaguzi wa mwaka 2005 aliibuka wa pili nyuma ya Karume; sawa ana ambavyo ilikuwa mwaka 2010 na 2015 nyuma ya Dk Ali Mohamed Shein. Baada ya uchagizi wa mwaka 2010, ndipo Maalim Seif aliteuliwa makamu wa kwanza wa Rais chini ya Dk Shein hadi 2015.
Kutokana na matokeo ya uchaguzi mkuu wa marudio 2015 ambao Maalim Seif aliususia baada ya ule wa awali kufutwa, Maalim alibaki nje ya SUK hadi mwaka 2020 aliposhiriki tena, safari hii akiwa ACT Wazalendo.
Katika uchaguzi wa mwaka 2020, ACT-Wazalendo pamoja na timu yake, Maalim Seif aligombea tena na kama kawaida akaibuka wa pili, nafsi iliyompa fursa nyingine ya kuwa makamu wa kwanza wa Rais.
‘Ametujengea msingi’
Akizungumzia uchaguzi huo bila Maalim Seif, kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Saibu amesema mwanasiasa huyo alijenga msingi wa kupendwa kwa chama hicho visiwani Zanzibar, kupitia kampeni yake ya ‘Shusha Tanga, Pandisha Tanga, Safari Iendelee’.

Kwa mujibu wa Shaibu, katika kipindi hicho chama kilipokea wanachama wengi na hatimaye ACT Wazalendo ikachukua nafasi ya CUF katika visiwa hivyo.
“Maalim amekwenda akiwa ametuachia msingi imara, tuna wanachama, tuna wapenzi na tuna imani ya Wazanzibari,” amesema.
Baada ya mwanasiasa huyo, Shaibu amesema kwa sasa amekuja Othman Masoud, ambaye kuingia kwake ndani ya chama hicho kumefananishwa na mpango wa Mungu.
Amesema Othman atakwenda kufanya shughuli ya umaliziaji akianzia pale alipoishia Maalim Seif na anafahamika kwa misimamo yake.
“Anasimamia anayoyaamini na unakumbuka alipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar alisimamia haki ya Zanzibar katika mchakato wa kuandika Katiba mpya bila kujali gharama ya kupoteza nafasi yake,” ameeleza.
Shaibu ameeleza tayari Masoud ameweka wazi msimamo wake, kuwa iwapo haki ya Wazanzibari itaporwa katika uchaguzi wa mwaka 2025, hatawarudisha nyuma wananchi wa visiwa hivyo katika kupigania haki yao.
“Watu watarajie mapambano makali, watu watarajie Wazanzibari wakimalizia pale ambapo Maalim Seif aliishia kujenga,” amesema Shaibu.
Amesema Masoud ndiye mwanachama pekee aliyetia nia ya kugombea urais wa visiwani humo kwa tiketi ya ACT Wazalendo tangu chama hicho kulipofungua pazia la kutangaza nia.
Chachu ya siasa itapungua
Wakati Shaibu akisema hayo, mwanazuoni wa utawala bora, Dk Lazaro Swai amesema mwanasiasa huyo ndiye aliyekuwa chachu ya siasa za ushindani visiwani humo.
Ushindani huo, amesema hakuuonyesha kwa upande wa Zanzibar pekee, hata alipokuwepo bara, akihutubia alionyesha mikikimikiki.
Kwa kuwa uchaguzi utafanyika bila kuwepo kwake, amesema ile chachu iliyosababishwa naye itapungua na hakutashuhudiwa mikikimikiki wala mihemko ya kisiasa.
“Haiba yake ilibeba zaidi ya ule upepo wa kisiasa na mioyo ya watu wa Zanzibar. Wengi walimuona kama jemedari na hata wangetaka jambo liingie kwenye mabadiliko, basi Maalim Seif alitazamwa kuwa anafaa kuliongoza,” amesema.
Kwa mtazamo wa Dk Swai, lile joto la siasa za Zanzibar lililokuwa likishuhudiwa enzi za Maalim Seif halitakuwepo tena, badala yake kutakuwa na ubaridi.
Kwa sababu hiyo, ameeleza kwamba kunahitajika juhudi za vyama vya upinzani kuhakikisha anapatikana mwanasiasa mwenye kaliba ya Maalim Seif, angalau kuamsha ushindani katika visiwa hivyo.
Act yajiandaa na uchaguzi
Sambamba na hilo, Shaibu amesema msimamo wa chama hicho kuhusu kushiriki uchaguzi iwapo sheria hazitabadilishwa, utatolewa baada ya kikao cha Halmashauri Kuu kitakachofanyika Februari 23, 2025.
Hata hivyo, amesema anaona kuingia katika uchaguzi mkuu bila mabadiliko ya sheria, ni sawa na kubariki yajirudie yaliyotokea katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Pamoja na mtazamo huo, amesema chama hicho kitaendelea kushinikiza mabadiliko ya sheria, bila kuacha kujiandaa kwa uchaguzi.
“Tunachofanya tunalenga kuhakikisha mabadiliko yakifanyika yatukute tumeshajiandaa, tusiwe na wa kumlaumu. Utasema sijiandai napambania mabadiliko ya sheria, kwa mfano yakifanyika karibu na uchaguzi wakati hukujiandaa utatafuta wa kumlilia,” amesema Shaibu.
Pia, ameongeza kuwa chama hicho kinaendelea kuratibu ushirikiano na vyama vingine katika safari ya kudai mabadiliko ya kisheria, sera na Katiba wanapoelekea, katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.