
Hai. Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha mapinduzi (UVCCM), Rehema Sombi ameagiza viongozi wa jumuiya hiyo katika mikoa yote nchini kufanya makambi ya vijana ngazi za mikoa na wilaya ili kuwaandaa vyema kukitafutia chama hicho ushindi kwenye uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba 2025.
Mbali na hilo, Sombi amewataka vijana kuacha tabia ya kubeba mabegi ya wagombea badala yake nao kujitokeza kugombea nafasi za ubunge na udiwani ili kuwa na wigo mpana wa vijana kuingia katika vyombo vya uamuzi.
Sombi ametoa rai hiyo leo Jumapili Machi 2, 2025, wakati akifunga kambi ya vijana 722 wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro iliyofanyika kwa siku sita wilayani Hai, ikiwa na lengo la kuwanoa na kuwaandaa vijana kuelekea uchaguzi mkuu.
Amesema uchaguzi ni mchakato na unahitaji maandalizi, hivyo kufanyika kwa makambi hayo kutawezesha vijana kunolewa na kufundishwa masuala mbalimbali kuelekea uchaguzi huo.
“Huu ukiwa ni mwaka wa uchaguzi na sisi ni waumini wa matokeo, nitoe maelekezo kwa wilaya zote kwenda kufanya makambi ya vijana kuwaandaa vijana kuelekea uchaguzi.
“Pia, nitoe maelekezo kwa umoja wa vijana mikoa yote nchini kufanya makambi ya vijana mithili ya kambi hii ya Kilimanjaro, ili kuendelea kuwaoka makada wetu vijana,” amesema Sombi.
Akizungumzia nafasi ya kijana katika uchaguzi, Sombi amesema hawapaswi kubaki nyuma katika michakato ya uchaguzi na kwamba kila mmoja anapaswa kujitoa kwa nafasi yake kuhakikisha chama kinashinda.
“Uchaguzi ni mchakato, uchaguzi ni kabla, kipindi cha uchaguzi na baada ya uchaguzi, hivyo tusibweteke, tushiriki hatua zote za uchaguzi na kukiwezesha chama chetu kushinda,” amesema Sombi.
Makamu huyo mwenyekiti ametumia fursa hiyo kuwaomba vijana: “Tuache kuwabebea mabegi wagombea, tunapokwenda kuwaunga mkono mjitose kwenda kuomba nafasi ili kuwa na wigo mpana wa vijana kuingia katika vyombo vya uamuzi.”
“Lakini mgombea atakayesimamishwa kupeperusha bendera ya CCM tunakwenda kusafisha kuhakikisha tunapata ushindi wa kishindo wa CCM, hakuna kulala mpaka kieleweke.
“Niwaombe viongozi wa jumuiya mkoa, wilaya na kushuka chini katika maeneo yenu kabla ya vikao mtangulize mafunzo ili kuwa na uelewa mpana wa jambo na kuweza kuwajibu vyama rafiki kwa hoja,” amesema Sombi.
Awali, Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa, Victor Makundi amesema UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro hawako tayari kuona chama hicho kinashindwa katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
“Kushindwa kujiandaa ni kujiandaa kushindwa, vijana CCM Kilimanjaro hatupo tayari kuona chama chetu kikishindwa, hivyo tukaona tuwaandae vijana wetu kuendelea kujiimarisha na kujiandaa kwa ushindi wa kishindo wa Rais Samia Suluhu Hassani, wabunge na madiwani,” amesema Makundi.
Kambi hiyo ambayo ilianza Februari 25, 2025 imehitimishwa Machi 2, 2025 na ilikuwa na mada mbalimbali ikiwamo nafasi ya kijana katika uchaguzi, athari za matumizi ya dawa za kulevya katika ujenzi wa Taifa, namna bora ya kijana kuwa mjasiriamali na faida na hasara za matumizi ya mitandao ya kijamii kwa vijana.