Uchaguzi Mkuu 2025: RC Chalamila atoa maagizo kwa Ma DC, DED

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila ametoa maagizo kwa wakuu wa wilaya (DC) na wakurugenzi (DED) kukamilisha ujenzi wa vituo vya Polisi ili vianze kazi ya kujipanga na uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Amesisitiza ni muhimu vituo hivyo vikamilishwe haraka Polisi watawanywe watakaokuwa na jukumu la kulinda amani na kudhibiti wale wote wenye nia ya kutaka kuvuruga amani, na kuwaondoa watu kwenye malengo ya kuwachagua viongozi wanaowataka.

Maagizo hayo ameyatoa leo Jumatano, Aprili 9, 2025 alipokuwa anakagua ujenzi wa Shule ya Sekondari Goba Golagwa Wilaya ya Ubungo, katika ziara yake inayolenga kukagua miradi ya maendeleo na baada ya hapo atakuwa na mkutano wa kusikiliza kero.

“Sasa hivi tunakabiliwa na uchaguzi hapo mbele na moja ya silaha ya uchaguzi ni ulinzi kwa hiyo tufanye kila linalowezekana vituo vya Polisi vinavyojengwa viishe mapema na tuweke askari polisi.

“Polisi hao watakuwa na majukumu mawili moja wahalifu na pili kulinda raia wasiokuwa na hatia. Ni lazima watakaovuruga amani watiwe kwapani ili kuhakikisha kila raia mwema anakuwa salama.

“Tunapoelekea kwenye uchaguzi mizaha inakuwa mingi anaweza popote pale akaja tu akavuruga amani ili tu kuwahamisha kwenye malengo yenu sasa kituo cha Polisi kikiwa mbali hilo nalo litakuwa tatizo,” amesema Chalamila.

Amesema jambo hilo ni muhimu litekelezwe kwani hata moja ya kikao walichofanya ukumbi wa maofisa wa Polisi Mesi Oysterbay, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliwaagiza Wizara ya Mambo ya Ndani kufanya kazi kwa kushirikiana na Serikali za mitaa,” amesema mkuu huyo wa mkoa.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Lazaro Twange amesema maagizo ameyapokea na atayatekeleza kwa kushirikiana na watendaji wake wengine, ili vikamilishwe ikiwemo kituo cha Polisi cha Kata ya Goba.

“Mkuu maagizo yako nimeyapokea na nitayafanyia kazi kwa kushirikiana na watendaji wenzangu, vikamilike na vianze kufanya kazi,” amesema Twange

Hoja ya kushamiri vibaka Dar

Chalamila amesema licha ya kushamiri kwa vibaka katika maeneo mbalimbali jiji hapa, tatizo hilo linapaswa kudhibitiwa ngazi ya mitaa kupitia ulinzi shirikishi (Sungusungu).

“Tumeshasema lakini mkisema bunduki zitumike gharama ya kununua itakuwa kubwa lakini tabia hii mnadhibiti wenyewe kwenye maeneo yenu. Kibaka maana yake ni tabia za ndani mnavyozoeana wenyewe, mtu kaiba nguo mmemuona hamsemi mnakaa kimya baadaye anaanza kuua mtu na kuiba huyu anakuwa amejibadilisha kishakuwa jambazi.

“Sasa vibaka wanatakiwa kudhibitiwa kwenye maeneo yenu, tushirikiane kwa pamoja kulisaidia jeshi letu la Polisi haliwezi kutawanyika kila mahali. Polisi libaki kwenye yale maeneo ya kimkakati makubwa makubwa akipatikana jambazi basi polisi kazi yao,”

“Lakini kusema Polisi washughulike na vibaka vibaka mtakuwa mnawaonea risasi ikipigwa watazimia sasa hiyo itakuwa si vizuri,” amesema Chalamila.

Tahadhari kwa wananchi

Chalamila amewataka wananchi kuwa makini wanapoelekea kwenye uchaguzi mkuu 2025 kwani watapata fursa ya kufika watu mbalimbali kuwasikiliza sera zao, wapo watakaozungumza kweli na uongo.

“Mfano wa uongo ni yule atakayezungumza Tanzania haijafanya chochote, huo ni uongo kwa sababu mimi baada ya miaka mitano nilikuwa hapa na Goba hii naikumbuka walikuwa akina Mzee Ibrahimu Kisoki, wakati huo kulikuwa hakuna Kata ya Wazo ila ilikuwa Kunduchi.

“Wapo watakao lalamika mbona hakuna barabara lakini ukweli ni kwamba Mtanzania akitaka kuja kujenga nyumba huku huwezi kumzuia unamuambia nenda halafu nitakuletea maendeleo, kwa hiyo barabara zinajengwa kukufuata wewe, umeme unakufuata wewe, maji yanakuja yanakufuata wewe,” amesema.

Chalamila amewasihi wananchi wasikubali kudanganyika na lugha nyepesi nyepesi kwamba hakuna kilichofanyika uongo wa namna hiyo waukatae, lakini wakiwa wabishi vinginevyo mdahalo ufanyike.

“Haiwezekani ukipita wewe ndani ya miaka 15 hujajenga hata ofisi yako, halafu unaaminisha wenzako Tanzania hakuna maendeleo huo ni mdomo wa uchonganishi na lazima tuudhibiti kwa kuonyesha maendeleo yaliyofanyika.

Kabla ya kukagua mradi huo wa shule ya sekondari alitembelea mradi wa Maji Luguruni, kisha kukagua na kuweka jiwe la msingi katika jengo la wodi ya mama na upasuaji katika Kituo cha Afya Mpiji Magohe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *