
Dodoma. Homa ya uchaguzi imeendelea kutanda bungeni ambapo Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma ameshauri watumishi wa umma wanaotaka kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, wafanyiwe ukaguzi maalumu ili kuepuka Bunge kuwa sehemu ya vichaka vya kujificha watu wasio waadilifu.
Musukuma ametoa angalizo hilo kipindi ambacho vuguvugu la uchaguzi katika majimbo limepamba moto huku viongozi mbalimbali wakiwemo wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi, makatibu tawala wa mikoa na wilaya, wakurugenzi wa taasisi na mamlaka mbalimbali wakionyesha nia ya kuwania ubunge.
Katika baadhi ya maeneo, minyukano imekuwa mikubwa, hali iliyowafanya viongozi wakuu wa CCM, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, kwa nyakati tofauti kuonya kuhusu kampeni za mapema, huku wakisisitiza watakaobainika watachukuliwa hatua.
Machi 11, 2025 akifungua Mkutano Mkuu wa 39 wa viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat), Rais Samia aliwataka wakuu wa wilaya (DC), wakurugenzi wa halmashauri (DED) na watumishi wengine wa Serikali wanaotaka kujitosa katika uchaguzi mkuu kutoa taarifa mapema, la sivyo watakosa vyote.
“Kuna Ma-DED wangu, wakuu wa wilaya… wana hamu sana kurudi kwa wananchi. Nilimwambia Katibu Mkuu Kiongozi apeleke mwongozo wa serikali za mitaa, nadhani Waziri (Mohamed Mchengerwa – Tamisemi) umeupata kwamba yeyote mwenye nia ya kugombea atuambie mapema,” alisema Rais Samia.
Leo Jumatano, Aprili 16, 2025, Musukuma alikuwa akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais-Tamisemi kwa mwaka 2025/26 ya Sh11.78 trilioni bungeni jijini Dodoma amesema Rais Samia aliwataka watumishi wanaotaka kugombea katika uchaguzi mkuu mwaka 2025, wamuandikie barua na kwamba ameona msururu kidogo ni mrefu ambapo wengi wamemuandikia na wengine wamekuandikia Mchengerwa.
“Hatuwaogopi, tunawakaribisha bungeni lakini mheshimiwa Spika naomba nikushauri, hii ni nyumba ambayo kidogo tunatakiwa kuwa wasafi, sio kichaka cha watu kujificha,” amesema.
Lakini ghafla alikatishwa na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akisema baadhi ya wabunge wanashangaa Musukuma ameiona wapi hiyo orodha.
“Waheshimiwa wabunge anayetaka kujua nani kiongozi katika eneo lake anataka kugombea mtamuona mheshimiwa Musukuma atawapeni,” amesema Dk Tulia na kuliacha Bunge zima kuibuka na kicheko.
Wakati huo mjadala ukiendelea, baadhi ya wakuu wa mikoa, makatibu tawala za mikoa na wakuu wa wilaya walikuwamo bungeni. Musukuma akasema intelejensia inakuwa kwa baadhi ya watu na si kwa watu wote.
“Nilikuwa nashauri kwako wale wanaotaka kuingia katika game (mchezo) tunawakaribisha na ni suala la Kikatiba. Lakini kabla ya kuwapa idhini ya kwenda kugombea nikushauri hebu wapelekee special audit (ukaguzi maalumu),” amesema mbunge huyo.
Amesema ukaguzi huo maalumu ulenge katika kuwasafisha kwanza ili waingie katika kinyang’anyiro wakiwa wasafi.
“Naona kama tunataka kujikaanga wenyewe, tunatoa kulia tunaweka kushoto na mtu akishaingia humu amevaa kinga hawezi kuitwa. Kabla mtu hajaachia kiti chake kuja kugombea ubunge peleka special audit,”amesema.
Amesema hatua hiyo itasababisha wale ambao hawatakutwa na changamoto kwenda kugombea nafasi za ubunge.
“Hawawezi kukwapua huku halafu wakaja kugombea ubunge, nilikuwa naomba hilo na vyombo vyote mlizingatie na mheshimiwa waziri kabla hujawaruhusu kuja kugombea, wawe na barua zinazotuonyesha kuwa watu hao ni wasafi,” amesema.
Musukuma amesema wakiletewa kiongozi katika mkoa wake, mtu wa kwanza kwenda ofisi kwake ni yeye na anamtaka kumpa mipango yake ya baadaye kwenye mkoa huo.
“Unataka kwenda kwenu kugombea ubunge ama unataka ukurugenzi, mimi bahati nzuri naletewa watu wanaokaribia kustaafu hakuna mtu anayesumbua watu kwenye ubunge. Kwa sababu najua kahalmashauri kangu ni kachanga ukianza kukakwapua tena kwenda kutunza za ubunge utanimaliza,”amesema.
Amesema kwa manufaa ya wabunge wote anaomba ushauri huo ufanyiwe kazi ili watakaoingia katika Bunge hilo wawe wasafi.
Aidha, Musukuma amekishukuru chama chake kuwa watu watakwenda kuchukua fomu Juni 28, 2025 hadi Julai 2,2025 kwa kuwa sasa kitawafanya wabunge kuelekeza mawazo yao ndani ya Bunge.
“Tufanye kazi ya kibunge tukutane hiyo tarehe 28 nataka kuwaambia sera yetu tunasonga mbele. Hao wanaosema No reforms, no election hata kama kuna namna ya kuwapitisha mlango ya nyuma waruhusuni wasaini tukutane nao (kwenye uchaguzi,” amesema.
Amesema kama walitafuta mlango wa kutokea, wapewe hata kwa ziada ili mradi wakutane nao katika majukwaa ya kampeni za uchaguzi kwa sababu kwa kazi ambazo zimefanywa na Rais Samia Suluhu Hassan wapinzani hawana hoja.
“Yaani unakwenda kuzuia uchaguzi kwa sababu ya madaraka, hapana wasitupe jezi hapana, wasikimbie tarehe 28 likiachiwa wote tukutane kitaa (mtaani),”amesema.