Songea. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amewataka wanachama wa chama hicho na wadau wengine wa siasa kutokilazimisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025.
Dk Nchimbi amesema kwa mujibu wa sheria za nchi chama cha siasa kina uhuru wa kushiriki au kutoshiriki uchaguzi huku akisisitiza,”hakuna mtu yeyote anayeweza kuuzuia hata awe Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu.”
Mgombea mwenza huyo mteule wa urais CCM, amemwomba Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu na marafiki zake kama hawatashiriki uchaguzi huo basi, “watupigie kura ili wasipoteze haki hiyo ya kuchagua kama kuchaguliwa hawatashiriki.”
Dk Nchimbi amesema hayo leo Ijumaa, Aprili 4, 2025 wakati akifungua mkutano mkuu maalumu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) unaofanyikia Songea, Mkoa wa Ruvuma, utakaomalizika kesho Jumamosi kwa kufanya uchaguzi wa viongozi wa jukwaa hilo.
Amesema tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961, imekuwa inafanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano kulingana na Katiba ya Tanzania na hakuna kiongozi anayeweza kuuzuia uchaguzi akiwamo Rais.

Kauli hiyo imekuja alipozungumzia kampeni ya Chadema ya ‘No Reforms No Election’ (hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi) iliyopitishwa kwenye vikao mbalimbali vya Chadema ukiwamo mkutano mkuu uliofanyika Januari 21, 2025.
Tayari kampeni hiyo imezinduliwa Kanda ya Nyanza katika mikutano mbalimbali ya hadhara ikiongozwa na Lissu na Makamu Mwenyekiti Bara, John Heche.
Leo Ijumaa, Aprili 4, 2025 kampeni hiyo inazinduliwa Kanda ya Kusini yenye mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.
Chadema imekuwa ikisisitiza kuwa, pasipo kufanyika kwa mabadiliko hayo wataungana na wananchi kuuzuia uchaguzi huo wa madiwani, ubunge na urais au hawatashiriki.
Katika hilo, Dk Nchimbi ametumia sehemu ya hotuba yake ya dakika 20 ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa TEF, akisema hawezi kutoka kwenye hadhira hiyo pasipo kuzungumzia ‘No Reforms No Election’ akisema
nchi ina utaratibu wa kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano.
“Unapofika wakati wa uchaguzi hakuna mtu yeyote anayesema uchaguzi hautafanyika, iwe Rais, Makamu wa Rais na au Waziri Mkuu, nataka niwahakikishe wahariri na Watanzania kuwa uchaguzi utafanyika,” amesema.
Dk Nchimbi amesema hakuna sheria inayotaka kulazimisha chama kuingia kwenye uchaguzi.

“Msiwalazimishe. Kama hawatashiriki huu wa 2025 kuna mwingine wa 2030, 2035, 2040, 2045, wakikosa huu watapata mwingine. Mtu yeyote asiwalaImishe kuingia kwenye uchaguzi, kwa mujibu wa Katiba yetu chama hata kikiwa kimoja tutafanya uchaguzi.”
“Namwambia rafiki yangu Tundu Lissu kuwa ana haki kabisa kushiriki au kutoshriki, lakini kuna haki ya kuchagua na kuchaguliwa basi kama hachaguliwi (kwa maana ya Chadema kutoshiriki uchaguzi) naomba kura yake na rafiki yangu Tundu Lissu na wenzake wataitumia vyema nafasi hiyo ya kuchagua kama hawatashiriki,” amesema.
Aidha amewaomba wahariri:”Tutumie nguvu yetu ya kalamu kuhamasisha na kukemea wanasiasa wa pande zozote awe chama tawala au upinzani.”Ametamka kauli za kuleta uvunjifu wa amani wasizipe kipaumbele, “mtu akiongea kitu cha ovyo tuviache.”
Dk Nchimbi amesema mkifanya uchaguzi huru na wa haki mnakuwa mfano mzuri kwa nchi yetu:”Na mnatufundisha na sisi kuzingatia matakwa ya Katiba zetu na taasisi zisizofanya uchaguzi zinafubaa, zinadumaa na zinakufa.”
“Zipo taasisi zingine hazifanyi uchaguzi na nusu ya taasisi tulizonazo nchini hazifanyi uchaguzi na kwa ninyi wahariri kufanya uchaguzi mnakuwa na ujasiri wa kulisemea hilo kwa nguvu zote,” amesema Dk Nchimbi ambaye amewahi kuwa naibu waziri na waziri wa habari.
Amesema anauelewa wa tasnia hiyo na ugumu wanaoupitia na kwa kazi wanayoifanya wamechangia kuzielezea kwa kina 4R za Rais Samia Suluhu Hassan na wananchi wamezielewa.
“Mtu anaweza asielewe kirahisi lakini kazi mnayoifanya ni kubwa sana. Kama mngekuwa hamfanyi vizuri tungekuwa na makesi mengi mahakamani, lakini ni mara chache sana mmekuwa mnateleza ila kwa niaba ya hama cha Mapinduzi na Watanzania wapenda amani tunawapongeza sana,” amesema Dk Nchimbi.
Amesema vyombo vya habari ni muhimili wa nne na ni kioo wa Bunge, Serikali na Mahakama na kupitia kwao vinajiona wapi wamekosea na wapi warekehishe.
Kuhusu hali ya uchumi wa vyombo vya habari, Dk Nchimbi amesema watahakikisha Ilani ya uchuguzi ya CCM ya mwaka 2025/2030 suala hilo linakuwamo na linapewa kipaumbele kikubwa.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwijuma maarufu Mwana FA amesema Serikali inatambua changamoto inayozikumba vyombo vya habari, ikiwemo uchumi wa vyombo vya habari.
“Serikali inafanyia kazi, ikiwemo Rais Samia kubadilisha mitizamo ya tasnia ya habari na waandishi wafanye kazi yao kwa uhuru.”

Naibu Waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa Muheza (CCM), amesema huu ni mwaka wa uchaguzi wa madiwani, ubunge na urais, hivyo amewaomba wahariri kuhakikisha wanasisitiza amani, ushiriki wa wananchi kwenye uchaguzi:”Tuwahamasishe wananchi washiriki uchaguzi na si kususia uchaguzi.”
Aidha, naibu waziri huyo amewatakia kila la heri wagombea wote wa TEF na hata wale watakaoshindwa.
Maelezo ya TEF
Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile amesema uendelevu wa kiuchumi, uhuru wa habari na upatikanaji wa matangazo na Serikali inatambua hilo, imekuwa inafanya mikakati mbalimbali.
Balile amesema ukweli ni kwamba uchumi wa vyombo vya habari ni mgumu na hiyo inaweza kuwa hatari kwa wananchi na jamii.

“TEF inaendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha uweledi kwa habari na waandishi wa habari na matumizi ya njia za kidijitali yanazingatiwa,” amesema Balile.
Amepongeza Serikali kwa kuanzisha Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari na kati ya wajumbe sita wanayoiunda, watatu ni wajumbe wa TEF na hiyo ni dalili nzuri kwa tasnia hiyo.
Bodi hiyo inaongozwa na Mwenyekiti wake, Tido Mhando ambaye ni mwandishi nguli ndani na nje ya Tanzania.
Amesema mkutano huo maalumj pamoja na mambo mengine utafanya uchaguzi wa kupata viongozi watakaloliongoza kwa miaka minne ijayo. Uchaguzi huo utafanyika kesho Ijumaa, Aprili 5, 2025. Nafasi zinazowaniwa ni mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe saba.
Balile amesema nafasi ya uenyekiti aliyechukua na kurejesha fomu ni yeye pekee, sawa na umakamu ambaye ni Bakari Machumu. Wote wanatetea nafasi hiyo.
Nafasi ya ujumbe wapo wagombea 12, akisema kwa vyovyote vile watano watashindwa:”Lakini nikuhakikishie tutatoka salama tukiwa imara kabisa.”
Wanaochuana kwenye kinyang’anyiro cha ujumbe ni Reginald Miruko, Anna Mwasyoke, Tausi Mbowe, Angelina Akilimali, Jane Mihanji, Salim Said Salim, Bakari Kimwanga, Peter Nyanje, Yasin Sadik, Stella Aron, Esther Zelamula na Joseph Kulangwa.
Kuhusu Dk Nchimbi kuwa mgeni rasmi amesema ni mwendelezo wa kukutana na wadau mbalimbali bila mipaka na wataendelea kufanya hivyo bila woga.
Amesema wameshakutana na viongozi wa Chadema kwa nyakati tofauti na kuzungumza nao ambao ni Tundu Lissu, mwenyekiti wa chama hicho na Freeman Mbowe, mwenyekiti aliyemaliza muda wake.
Alichokisema Dk Ndumbaro, RC
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amesema yeye ni sehemu ya waanzishaji wa TEF na ndiye aliyeiandika katiba ya jukwaa hilo wanayoitumia, amekuwa waziri wa habari na mdau mkubwa wa wana habari, hivyo uwepo wake kwenye mkutano huo ni faraja.
Dk Ndumbaro ambaye pia ni mbunge wa Songea Mjini, amesema Dk Nchimbi ni mbunge wa kwanza wa mkoa wa Songea kujenga shule ya sekondari inayoitwa Dk Emmanuel Nchimbi na katika kipindi chake cha ubunge (2005-2015) alifanikisha ujenzi wa barabara za lami, kwani alikuta barabara moja pekee ya lami.
Amesema wakati Dk Nchimbi akiwa mbunge yeye (Dk Ndumbaro) alikuwa mpigakura wake, lakini kwa sasa Dk Nchimbi ni mpigakura wake:”Kwa hiyo Dk Nchimbi naomba kura yako wakati ukifika nitakuja kukuomba kura.”
Kuhusu uteuzi wa Dk Nchimbi kuwa mgombea mwenza, Dk Ndumbaro amesema alikuwa miongoni wa walioshangilia ukumbini pale Dodoma.
“Nilipanda juu ya meza kwa sababu nchi imepata mtu sahihi wa kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.
Kuhusu tasnia ya habari, Dk Ndumbaro ambaye kitaaluma ni mwanasheria amesema Serikali inahakikisha inaweka mazingira mazuri na wananchi kupata habari.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema kundi la waandishi wa habari ni muhimu katika maendeleo ya nchi na viongozi wa Serikali wanapopata bahati ya kukutana na kundi la waandishi unapaswa kujivunia kwa sababu kazi wanayoifanya.
Amesema kufanyika kwa mkutano huo mkoani Ruvuma ni faraja, kwani watu mbalimbali wanafurahia uwepo wa mkutano huo, kwa namna moja au nyingine utachochea maendeleo.
Kanali Ahmed amesema kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pato la mkoa ni Sh8.2 Trilioni na asilimia 3.8 inachangiwa kwenye Pato la Taifa.