Ubunge unavyozusha tafrani Mbeya

Mbeya. Kivumbi cha kusaka nafasi ya kuwania ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya, kimeendelea kuchukua sura mpya baada ya mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo, Patrick Mwalulenge kudai imefikia hatua baadhi ya makada wameanza kujiingiza kwenye ulozi kutafuta madaraka hayo.

Mvutano huo umekolea zaidi na Halmashauri ya Jiji la Mbeya kupendekeza kugawanywa Jimbo la Mbeya Mjini na kuzaliwa kwa Jimbo jipya la Uyole kama ambavyo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kutangaza mchakato wa kuyagawa majimbo.

Mnyukano katika mkoa huo unazidi kukolea katika kipindi ambacho chama hicho kinajiandaa kuingia kwenye kura za maoni kusaka mgombea atakayepeperusha bendera kupitia chama hicho kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu, Machi 17, 2025 na Mwalulenge kwenye kikao cha ndani kilichofanyika mkoani humo katika ukumbi wa Eden, ambacho Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Stephen Wasira alikuwa mgeni rasmi.

Mwalulenge amesema mwaka huu wanakwenda kwenye uchaguzi mkuu, lakini hali na aina ya siasa zinazofanyika ndani ya mkoa huo hazimfurahishi.

“Wito wangu tushikamane tunavyoelekea huko tuhepuke vitendo vya rushwa, rushwa ni adui wa haki tujue leo tutapokea rushwa ya mtu ambaye tunamuhitaji CCM, lakini inawezekana wananchi mtu huyo wasimtake tutapata shida na kukigharimu chama,” amesema.

“Tuache majungu, binafsi si muumini wa majungu lakini tambueni kuna rushwa ya majungu na ufitini, fitini majungu ni rushwa kubwa, utaniletea majungu kwa ajili ya mtu fulani lakini utasababisha nisifanye maamuzi sahihi kwa sababu ya majungu,” amesema.

Katika maelezo yake Mwalulenge amesema rushwa ya kutoa fedha na majungu na ufitini vinafanana:”Niwaombe wana-CCM wenzangu tuacheni majungu muda ukifika tukatende haki kwa kutenda haki kwenye kura za maoni yule anayependwa na watu aletwe,” amesema.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira akizungumza na wanachama, viongozi wapenzi wa CCM Mkoa wa Mbeya katika mkutano uliofanyika leo Machi 17, 2025 katika Hoteli ya Eden Highland, Mbeya.

Kulingana na Mwalulenge amesema CCM, ngazi ya mkoa huo wameshajipambanua wazi hakuna mtu watakayembeba na hakuna mtu atakayesema anaungwa mkono na mwenyekiti wala Katibu au Mjumbe wa Halmashauri Kuu.

“Hayupo tutatenda haki kadri mapendekezo yatakavyo kuja ya wananchi kwa maana ya wanachama wa chama, mabalozi  na sasa wigo umekuwa mpana kwa kuongezeka idadi ya wapiga kura ili kusiwe na manung’uniko  mtu atakayeletwa hatutapindisha maneno,” amesema.

Amesema hakuna mtu wa kuwaonga rushwa ya maneno, fedha au majungu huku akiwataka wanachama hao kwenda kufanya kazi kwa kumtanguliza Mungu huku akieleza kuna wakati ndani ya chama hicho wanajisahau wanahisi kama Mungu hayupo.

“Tunaamini chama ni kila kitu watu tumekuwa wanyama tunataka kutoa roho za watu kwa sababu ya madaraka jambo ambalo si sawa, uongozi ni vijiti kupokezana unaanza wewe atakuja mwingine inakuwaje mwingine amchukie mwingine, inanishangaza inakuaje unataka kutoa uhai wa mwenzako kwa sababu ya madaraka,” amesema.

“Unaweza kupata nafasi wa hila lakini mwisho wa siku wananchi wakakuzomea, unazomewa kwa sababu si chaguo la wananchi tujue baada ya uongozi kuna maisha tutakuja kutoa hesabu zetu mbele ya Mungu hilo ni ombi langu kwenu,” amesema.

Akizungumza huku akipigiwa makofi, Mwalulenge amewataka wanachama hicho kubadili aina ya kufanya siasa kwa kuwa hicho ni chama kikubwa na kina miaka 60 sasa, kufanya siasa kwa ustaarabu na kujali wengine ni mfumo mzuri wa kukiheshimisha chama hicho.

“Tuache nongwa sawa wana-CCM wenzangu inawezekana nisiwe na maneno mazuri sana nilazima tuelezane ukweli, jambo lingine mgeni rasmi kigezo cha mwisho nawaambia viongozi wa wilaya ni mtu anayeshughulika na shida za watu na ni kiongozi tunayemtaka katika mkoa wa Mbeya,” amesema.

Amesema ilivyo sasa viongozi wengi mkoani hapo hawashughuliki na shida za watu bali wanazingatia maslahi yao binafsi “Inakuwaje kiongozi tumekupa bendera ya kushughulika na shida za watu, mgeni rasmi tunaenda kuleta mtu anayeshughulika na shida za watu,”amesema.

Alichokisema Wasira

Kufuatia kauli hiyo, Wasira amesema hakuna mwenye haki miliki na nafasi ya ubunge wakati ukifika duka linakuwa wazi na kwa wale wanaohitaji madaraka ya aina hiyo waanzishe duka lao.

“CCM ni duka la wote na wenye kuuza wanabadilika leo yule kesho mwingine, lakini tunashida ndani ya hiki chama tunaacha kazi ya kujenga chama chetu tunamatatizo ya wakulima wachai pale wanasema hawalipwi fedha fedha kule Rungwe,” amesema na kuongeza kwa kusema.

“Watu wanaanza kujadili mwenyekiti anakaa wapi siku hizi hatuwezi kuunda chama kikubwa namna hii alafu tunaanza kushughulika na matatizo ya aina hiyo, tunataka vikao vyetu vya chama vizungumze matatizo ya wananchi na rudia vikao vyetu vizungumze matatizo ya wananchi,” amesema.

Kulingana na Wasira amesema kuna matatizo mengi wamachinga, bodaboda ni muhimu kuzungumza matatizo ya watu hao ili wanachi wajue wakiwa na kero wakimbilie ndani ya chama hicho.

“Mambo ya ubinafsi yanahusiana na nini dani ya chama chetu, uchaguzi ukiisha kwa sababu fulani kashinda unanuna miaka mitano yote na tambueni madaktari wanasema ukinuna kwa muda mrefu utakufa bure lazima ukubali matokeo,” amesema.

Wasira amesema kuna baadhi wanakuja na hoja kwamba wanaungwa mkono na wanachama wengi akidai kauli hiyo si sahihi kwani wanachama wote wanamilikiwa na Chama hicho: “Unasemaje wa kwako kwani uliwaumba? Wakawako? Unamatatizo kweli tuache hayo.”

Amesema wengine wakishindwa kwenye kinyang’anyiro wanaanza kudai warudishiwe fedha zao: “Kwani hizo fedha ulinikopesha shauri yako uliacha kunua mboga ukaenda kununua kura.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *